Usiyoyajua juu ya Mrema ‘mtu wa matukio’

Muktasari:
- Mwenyekiti wa TLP Taifa, Augustine Mrema ambaye kwa zaidi ya miongo mitatu amekuwa akitamba kwenye vyombo vya habari nchini kutokana na matukio yake mengi yanayovuta hisia za Watanzania, wiki iliyopita Machi 24, alifunga ndoa katika Parokia ya Uwomboni-Kiraracha mkoani Kilimanjaro.
Mwenyekiti wa TLP Taifa, Augustine Mrema ambaye kwa zaidi ya miongo mitatu amekuwa akitamba kwenye vyombo vya habari nchini kutokana na matukio yake mengi yanayovuta hisia za Watanzania, wiki iliyopita Machi 24, alifunga ndoa katika Parokia ya Uwomboni-Kiraracha mkoani Kilimanjaro.
Itakumbukwa baada ya Mrema kutangaza nia yake ya kufunga ndoa hiyo, jina lake lilianza tena kutamba kwenye vyombo vya habari vya magazeti, radio, TV na katika mitandao ya kijamii.
Machi 21, mwaka huu, Mrema alitangaza kupitia mkutano wake na waandishi wa habari kuwa “Nimepata binti mwenye umri mdogo mweupe ambaye ni chaguo langu, tutafunga pingu za maisha siku chache zijazo baada ya kufuata taratibu za kanisa na ulipaji wa mahari.”
Mrema hakupotea kwenye vyombo vya habari, Machi 24, 2022 kabla ya kufungwa kwa ndoa yake mke wake mtarajiwa alitoka nyumbani kwake akiwa amejifunika kanga gubigubi ili asionekane sura yake na waandishi wa habari waliokuwa wakitaka kuona sura yake.
Waandishi wa habari walikuwa na hamu ya kuona sura ya ‘kipusa’ hicho kwa kuwa kulikuwa na picha za wanawake tofauti tofauti katika mitandao ya kijamii kila mmoja akihusishwa ndiye mke mtarajiwa wa mzee Mrema.
Siku ya harusi ilipowadia, Machi 24, wakiwa ndani ya kanisa tayari kufunga ndoa yao, mke wa Mrema, Doreen Kimbi alizungumza na waandishi wa habari huku akiwa amevaa miwani myeusi akijinasibu kuwa atamrudisha mwanasiasa huyo ujanani.
“Mpaka kufikia hivi alivyo nimemfanya hivi. Katika kipindi cha uchumba nimemweka kuwa sawa. Vitu vyote anavyohitaji anavipata. Kwa sasa amebadilika. Nimeamua mwenyewe na sijashurutishwa na mtu na watarajie kuona anapendeza. Nataka hadi awe kijana,” alisema Doreen.
“Mimi si mwanamke wa kupewa. Nimesimama mwenyewe na hata mali ninazo. Nilianza kujitafutia mimi, siendi kwake (Augustino Mrema) kutafuta mali. Lakini nikimlea vizuri akanipa mali si vibaya kwani mimi ni mke wake,” alisema Doreen.
Ndoa ya Mrema ilikuwa ikirushwa mubashara kupitia vituo mbalimbali vya habari mitandaoni na kufuatiliwa na watu kadhaa, ilionekana ni tofauti na ndoa nyingine ambazo pia ziliwahusisha watu maarufu hazikurushwa mubashara na vyombo vya habari.
Mrema amegoma kutokuwa nje ya vyombo vya habari, hataki asisikike. Kila analofanya ni habari na anajua namna ya kulifanya liwe habari. Mara baada ya kufunga ndoa alizungumza na waandishi wa habari akiwa nyumbani kwake na kuwatania vijana ‘Mnakwama wapi mpaka mimi nimewazidi kete kwa kuchukua kipusa hiki?” aliwahoji
Ndoa ya Mrema na Doreen inakuja miezi sita na wiki moja tangu mke wa mwanasiasa huyo, Rose alipoaga dunia Septemba 16, 2021 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu alipougua ghafla baada ya kupata mshtuko wa moyo kutokana na mishipa mitatu kuziba kwa muda mrefu.
Maziko yalifanyika Jumanne ya Septemba 21 nyumbani kwake kijiji cha Kiraracha-Vunjo Mkoa wa Kilimanjaro. Kuanzia hapo Mrema hakusikika hadharani hadi pale alipotangaza kuwa amempata binti mwenye umri mdogo mweupe ambaye ni chaguo lake.
Alivyoanza kusikika
Augustine Mrema amekuwa mtu wa matukio yanayovutia vyombo vya habari tangu alipojitokeza katika uwanja wa siasa mwaka 1985 alipogombea Jimbo la nyumbani kwake.
Katika uchaguzi uliofanyika Jumapili Oktoba 27, 1985 ndipo alipoibuka Augustine Mrema katika Jimbo la Moshi Vijijini. Mrema alishinda kwa kupata kura 38,984 na kumshinda Peter Macha aliyepata kura 34,709.
Huu ndio wakati pia ambao Frederick Sumaye alichaguliwa kuwa mbunge jimbo la Hanang baada ya kupata kura 12,796 dhidi ya Salistian Akunaay Deengw.
Katika mwaka huo uchaguzi ulicheleweshwa kwa wiki moja kutokana na uhaba wa mafuta ya petroli uliolikabili Taifa mwaka 1985. Uchaguzi ulifanyika katika majimbo 164 tu kati ya majimbo 169 kutokana na wagombea wa majimbo matano kupita bila kupingwa.
Ingawa Mrema aliingia ulingoni kwa mara ya kwanza, alikuwa miongoni mwa waliowabwaga wabunge waliokuwako katika bunge lililopita.
Miongoni mwa wabunge wa walioshindwa kutetea nafasi zao ni Nganga Kipuyo (Arusha), Salustian Deengw (Mbulu), Joseph Lemomo (Monduli), Aaron Mpamjije (Kasulu), Martha Weja (Ilala), Patrick Nwila (Mbeya Vijijini), Steven Yilanga (Mbeya Mjini) na Sylvia Kate Kamba (Masasi).
Wengine walioshindwa ni Said Katapala (Mtwara Vijijini), Jalala Kilewa (Kibaha), Bakari Gwaya (Tunduru), Simon Mwaliko (Manyoni), Joseph Monko (Singida Vijijini), Padri Paulo Misigalo (Tabora Mjini, Tobi Mweri (Pangani), Thomas Bwire (Bunda), Balozi Maggid (Tanga) Hussein Hading’oka (Kinondoni), Leons Ngalai (Rombo) na Daudi Makenga Nzukila (Nzega).
Waliotetea nafasi zao ni Austin Kapera Shaba (Mtwara Mjini), Luteni Kanali Ayoub Kimbau (Mafia), Paul Bomani (alikuwa mbunge wa kuteuliwa na Waziri wa Ardhi, Maliasili na Utalii), Amran Halfani Mayagila (Iringa Mjini), Joseph Mungai (Mufindi), Samwel Luangisa (Bukoba Mjini, Cleopa David Msuya (Mwanga na Waziri wa Fedha) na Kingunge Ngombale-Mwiru (alikuwa mbunge wa kuteuliwa na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, na katika uchaguzi huu alishinda kiti cha Kilwa).
Wengine walioshinda ni Guntran Itatiro (Ulanga, na alikuwa Waziri wa Nchi katika Wizara ya Mawasiliano na Ujenzi), Benjamin William Mkapa (alikuwa mbunge wa kuteuliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na sasa alishinda kiti cha Nanyumbu), Pius Ng’wandu (Maswa, Waziri wa Nchi katika Wizara ya Maji, Nishati na Madini), Hannington Mfaume (Shinyanga Mjini), Sumbu Gallawa (Singida Mjini) na John Machumba (Ukerewe, Waziri wa Kilimo).
Wengine walioshinda ni Samuel Sitta (Urambo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Ustawishaji wa Makao Makuu), Luis Kinyonto (Sumbawanga Mjini), Luka Kitandula (Mkinga), Mustafa Salum Nyang’anyi (Kondoa, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Ushirikiano wa Kimataifa), Lumuli Kasyupa (Kyela), Mathias Kihaule (Ludewa) na Basil Mramba (alikuwa mbunge wa kuteuliwa, Waziri wa Viwanda na Biashara na sasa alishinda kiti cha Rombo dhidi ya Leons Ngalai).
Mrema alizaliwa Jumatatu ya Desemba 31, 1944 katika kijiji cha Kiraracha akiwa mzaliwa wa pili katika familia ya watoto watano wa Mzee Lyatonga Mrema.
Kati ya mwaka 1955 na 1963 alisoma hadi shule ya kati katika na mwaka 1964 mpaka 1965 alisoma Chuo cha Ualimu cha Mtakatifu Patrick.
Baada ya kumaliza mafunzo yake ya Ualimu na kupata kazi, Mrema alianza kuchukua mafunzo yake ya sekondari ambapo mwaka wa 1968 alifanya mtihani wake wa kidato cha nne, wakati huo mitihani ikitoka Chuo Kikuu cha Cambridge cha nchini Uingereza.
Mwaka wa 1970-71 alijiunga kwenye mafunzo maalumu ya siasa na uongozi katika Chuo cha Kivukoni na mwaka 1980 na 81 alikwenda kusoma nchini Bulgaria ambako alitunukiwa Diploma ya Sayansi ya Ustawi wa Jamii na Utawala.
Mrema alianza kazi ya ualimu mwaka 1966 na kufundisha shule mbalimbali za mkoa wa Kilimajaro. Mwaka 1972 aliteuliwa kuwa mratibu wa elimu wa Kata hadi 1973.