Uraia pacha ni shughuli pevu

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk Stergomena Tax
Dodoma/Dar. Suala la uraia pacha limeendelea kufukuta nchini, likichochewa na mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki uliofanyika jana bungeni.
Mjadala huo unakolea kipindi ambacho Serikali imelieleza Bunge kwamba mpango wake wa kutoa hadhi maalumu kwa watu wenye nasaba na Tanzania walioko nje (diaspora) utakamilika Desemba mwaka huu.
Pia, unakuja wakati kukiwa na kesi ya uraia pacha katika Mahakama Kuu iliyofunguliwa na Watanzania sita wanaoishi na kufanya kazi nje ya nchi, wakipinga Sheria ya Uraia, hasa vifungu vinavyozuia uraia pacha, wakidai vinakiuka haki zao nyingine za kikatiba.
Jana, Waziri wa wizara hiyo, Dk Stergomena Tax alifafanua suala hilo hadi lile la hadhi maalumu wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake ya Sh247.97 bilioni ambayo ilijadiliwa na kupitishwa papo hapo.
Waziri Tax alieleza hayo siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni kusema kuwa hadi Mei mwaka huu, Watanzania 66 waliukana uraia wa Tanzania na kupewa uraia wa mataifa mengine.
Masauni alisema kwa mujibu wa Sheria ya Uraia Sura ya 357 Rejeo la 2002, wote walioukana uraia wa Tanzania wanapoteza haki ya kuendelea kuwa Watanzania. Katika kipindi kama hicho mwaka 2021/22 Watanzania 40 waliukana Uraia wa Tanzani.
Hata hivyo, Waziri Tax katika hotuba yake, alisema wizara yake ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuwapatia hadhi maalumu diaspora wenye asili ya Tanzania na uraia wa nchi nyingine, ili kuwawezesha kuchangia miradi ya kitaifa.
Alisema wizara ilikusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kutoka kwa diaspora wenyewe.
Alisema, “maoni hayo yameainisha maeneo au masuala yanayopendekezwa kujumuishwa katika hadhi maalumu.”
Alisema Machi mwaka huu, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilitoa maelekezo kwa benki na taasisi za fedha nchini kuruhusu raia wa kigeni, wakiwemo diaspora wenye asili ya Tanzania na uraia wa nchi nyingine kufungua akaunti za fedha za kigeni kwa kutumia vitambulisho mbadala vya utambuzi, tofauti na hati ya kusafiria ya Tanzania na kitambulisho cha Nida.
Alisema nyaraka hizo mbadala za utambuzi ni pamoja na hati ya kusafiria na vitambulisho vingine vya nchi ya kigeni kama leseni za udereva, kitambulisho cha kupigia kura, cha kazi au cha mwanafunzi.
Alisema hatua hiyo itawawezesha diaspora kuweka fedha zao za kigeni katika benki za hapa nchini.
Walichokisema wabunge
Michango ya wabunge ilijikita kwenye eneo la uraia pacha. Mbunge wa Kilosa (CCM), Profesa Palamagamba Kabudi alisema suala lenye muafaka hapa nchini ni la hadhi maalumu na akaiomba wizara hiyo kukamilisha jambo hilo ili kuwasaidia diaspora kuondokana na usumbufu.
“Sasa hili ni bora kuliko lile ambalo tunaendelea kulisema, suala la uraia pacha halina muafaka hapa nchini, lakini pia halina muafaka duniani na hivyo tulishikilie hili lenye muafaka tulisukume liende mbele,” alisema.
Alisema utafiti alioufanya unaonyesha ni asilimia 49 ya nchi ndizo zenye uraia pacha, lakini asilimia 51 hazijaruhusu aina hiyo ya uraia.
Profesa Kabudi ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alisema suala la uraia pacha Tanzania lina hisia kali.
Kwa mujibu wa Kabudi, mwaka 1960 wakati wa Serikali ya madaraka, uliwasilishwa muswada bungeni kuhusu uraia wa Tanganyika na aliyekuwa Waziri Kiongozi, Mwalimu Julius Nyerere.
“Ulileta msuguano mkubwa na hasa baada ya mwaka 1958 Waingereza walipotupa masharti ya uchaguzi wa kura tatu, kwamba kila jimbo liwe na mbunge Mzungu, Mwafrika na Muasia.
“Na kundi kubwa la vijana walijitoa Tanu na kuunda chama cha Africa National Congres of Tanganyika, wakisema Tanganyika ni kwa Waafrika tu,” alisema.
Profesa Kabudi alisema katika muswada huo, Mwalimu Nyerere alisema, “tunachojaribu kufanya ni kuanzisha uraia wa Tanganyika ambao ndio utakuwa msingi wa uraia. Serikali iliyochaguliwa na watu wa Tanganyika tunasema uaminifu kwa nchi ndiyo msingi utakaoamua uraia wa Tanganyika.
“Ili kuwa na hakika, tuhakikishe kuwa raia wa Tanganyika wamezaliwa kuwa watiifu kwa Tanganyika na Tanganyika pekee. Tunasema ingawa nchi nyingine zinakubali, hatutakubali uraia wa nchi mbili (uraia pacha),” alisema Kabudi akimnukuu Mwalimu Nyerere.
Akichangia suala hilo, Mbunge wa Ubungo (CCM), Profesa Kitila Mkumbo alisema wanachopigania si mtu mwingine aje kuomba uraia wa Tanzania, bali wanachopigania ni kwa nini Mtanzania apoteze haki yake ya Kimungu.
“Kama itakuja kuwa uraia pacha au hadhi maalumu mimi kwangu si tatizo, hoja kubwa tunalindaje haki za watu wetu ambao ni Watanzania wanapoenda kutafuta fursa katika nchi nyingine,” alisema Profesa Kitila.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Fakharia Shomari alisema kwa Tanzania uraia pacha bado mapema, ni vyema kuendelea kukazania hadhi maalumu kwa sababu inawapatia kila kitu diaspora.
“Sasa hata ukipata uraia pacha itakusaidia nini? Muhimu ujulikane kwenu. Namuomba Waziri aendelee na mchakato huu, hadhi inatolewa na sera inatolewa vinakwenda sambamba,” alisema.
Akihitimisha hoja yake, Waziri Tax alisema bado suala la uraia pacha halina muafaka nchini wala nje ya nchi.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan alisisitiza kuhakikisha diaspora ambao wako nchi za nje ni raia wenye asili wote wanapata haki na kutoa msisitizo wafanye mchakato wa kutoa hadhi maalumu.
“Ukitoa uraia pacha kwa sasa hivi wakati hakujawa na muafaka kitaifa na kidunia, kuna wale wanaoweza kukosa fursa. Kuna nchi ambazo diaspora zipo na zile ambazo hazitambui uraia pacha. Sisi tukitoa uraia pacha wale hawatapata fursa ambazo tunatarajia kuzitoa,” alisema.
Alisema mchakato wa kutoa hadhi maalumu umefika mbali sana na hadi kufikia Desemba mwaka huu hadhi maalumu itakuwa imetolewa, hivyo kuwezesha diaspora kupata fursa nyingi.
Alisema diaspora walitoa mapendekezo 10 ambayo wameyazingatia na kwamba yote yataingizwa kwenye hadhi maalumu, lakini katika mapendekezo hakukuwa na la “haki ya Kimungu”.
Alisema diaspora wanachotaka ni kuingia nchini, kumiliki ardhi, kupata huduma kwenye taasisi za fedha na yote yamezingatiwa kwenye hadhi hiyo.
Katika hatua nyingine, Dk Tax alitangaza kumalizika kwa sakata la wafanyabiashara wa Tanzania kunyimwa vibali ili watoe mahindi Zambia.
“Lakini napenda kulitaarifu Bunge kuwa limetatuliwa na wafanyabiashara wamepewa vibali leo (jana),” alisema Dk Tax.