Upelelezi kesi ya Dk Manguruwe 'ngoma nzito'

Muktasari:
- Mkondya na Rweyemamu wakabiliwa na mashtaka ya kuendesha upatu, kutakatisha fedha, matukio yanayodaiwa kuyatenda kati ya Januari mosi 2020 na Desemba mosi 2023 jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Serikali bado inaendelea na uchunguzi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya (40) maarufu kama Dk Manguruwe.
Mkondya na mwenzake, Mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo, Rweyemamu John (59), wanakabiliwa na mashtaka 28, yakiwemo ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha kinyume cha sheria.
Hata hivyo, mshtakiwa wa pili, Rweyemamu, yupo nje kwa dhamana kwa kuwa hana mashtaka ya utakatishaji fedha.
Wakili wa Serikali, Eric Davies, ameeleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Alhamisi, Februari 13, 2025, kuwa uchunguzi wa shauri hilo bado unaendelea.
Kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa, Davies aliwasilisha taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu.
Hata hivyo, mshtakiwa wa kwanza, Mkondya, hakuletwa mahakamani kutoka gerezani, wakati mshtakiwa wa pili, John, ambaye yuko nje kwa dhamana, alihudhuria.
Wakili Davies alidai upande wa mashtaka unaomba tarehe nyingine ya kutajwa ili kuangalia iwapo uchunguzi utakuwa umekamilika.
Hakimu Magutu ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 26, 2025, ambapo itatajwa tena, huku Mkondya akiendelea kushikiliwa rumande na John akiwa nje kwa dhamana.
Mashtaka yanayowakabili
Kwa mujibu wa hati iliyosomwa mahakamani Novemba 5, 2024, mashtaka 19 kati ya 28 yanayowakabili, yanahusu kuendesha biashara ya upatu na tisa yakihusu utakatishaji fedha.
Katika moja ya mashtaka ya biashara ya upatu, washtakiwa wanadaiwa kati ya Januari 1, 2020 na Desemba 1, 2023, jijini Dar es Salaam, waliendesha biashara hiyo kwa kuwaahidi watu kuwa wangepata faida mara mbili hadi tatu ya kiasi walichowekeza.
Washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia jumla ya Sh92.2 milioni kutoka kwa watu 19 tofauti, waliotoa fedha kwa ahadi ya kupata faida kubwa.
Katika mashtaka tisa ya utakatishaji fedha yanayomkabili Mkondya pekee, inadaiwa kuwa kati ya Januari 1, 2020 na Desemba 1, 2023, akiwa Dar es Salaam, alijipatia viwanja tisa vilivyopo katika kitalu namba AB, eneo la Idunda, mkoani Njombe.
Inadaiwa kuwa alijipatia viwanja hivyo huku akijua kuwa vimetokana na biashara ya upatu.