Dk Manguruwe aandika barua kwa DPP, atakiwa kusubiri upelelezi ukamilike

Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya (40) maarufu kama Dk Manguruwe (anayecheka) akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kesi yake ya Uhujumu Uchumi kuahirishwa. Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Dk Manguruwe aliandika barua kwa DPP akiomba kukiri mashitaka apunguziwe adhabu katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili.
Dar es Salaam. Mkurugenzi wa kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya (40) maarufu Dk Manguruwe, amemuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), akiomba kukiri mashitaka na kupunguziwa adhabu katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili.
Hata hivyo, Serikali imemjibu maombi yake hayajakubaliwa mpaka upelelezi wa kesi utakapokamilika.
Mkondya na Mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo, Rweyemamu John (59), wanakabiliwa na mashitaka 28 yakiwamo ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji wa Sh90 milioni.
Hayo yameelezwa leo Desemba 17, 2024 na Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Wakili Kasala ametoa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu, kesi ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
"Mshtakiwa wa kwanza katika kesi hii, Mkondya ameleta maombi ya kufanya Plea bargaining (majadiliano na makubaliano kuhusu kosa), lakini maombi yake kwa sasa bado hayajakubalika mpaka upelelezi wa shauri hili utakapokamilika," ameeleza.
Amedai licha ya mshtakiwa kuandika barua kukiri mashitaka, upelelezi wa kesi bado unaendelea hivyo anaomba Mahakama ipange tarehe nyingine.
Katika hatua nyingine, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Rweyemamu amepata dhamana kutokana na mashitaka yanayomkabili kuwa na dhamana.
Rweyemamu aliwasilisha ombi la dhamana mwezi uliopita akiomba mahakama impatie masharti kwa kuwa hana shitaka la kutakatisha fedha.
Hakimu Magutu alitoa masharti ya dhamana akimtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka serikali za mitaa au taasisi inayotambulika kisheria.
Mshtakiwa pia anatakiwa kuwasilisha fedha taslimu Sh45 milioni au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Hakimu Magutu alisema iwapo mshtakiwa atatimiza masharti ya dhamana, atakuwa nje kwa dhamana.
Rweyemamu ametimiza masharti hayo leo Desemba 18, hivyo kuachiwa kwa dhamana.
Mkondya hana dhamana kutokana na mashitaka ya kutakatisha fedha yanayomkabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.
Hakimu Magutu ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 2, 2025 itakapotajwa. Mkondya amerudishwa rumande.
Katika kesi hiyo yenye mashitaka 28, kati ya hayo 19 ni ya kuendesha biashara ya upatu na tisa ni ya kutakatisha viwanja.
Katika moja ya mashitaka ya kuendesha biashara ya upatu, washtakiwa wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023, jijini Dar es Salaam walitenda makosa hayo.
Mkondya akiwa mkurugenzi wa kampuni hiyo na John akiwa mkaguzi wanadaiwa waliendesha biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu watapata pesa mara mbili hadi tatu kama faida zaidi ya walizotoa.
Washtakiwa wanadaiwa kujipatia Sh92.2 milioni kutoka kwa watu 19 walitoa kiasi tofauti cha fedha kwa kuwaahidi watapata faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizotoa.
Katika mashitaka tisa ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili Mkondya pekee, anadaiwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023 akiwa mkoani Dar es Salaam kwa wadhifa wa mkurugenzi wa kampuni hiyo alijipatia viwanja tisa vilivyopo kitalu namba AB eneo la Idunda, mkoani Njombe.
Anadaiwa kujipatia viwanja hivyo akijua ni zao la makosa tangulizi ya kuendesha biashara ya upatu.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa walifikishwa mahakamani hapo Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 31523 ya mwaka 2024.