Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Upandaji miti ya parachichi wapunguza uharibifu mazingira Lushoto

Muktasari:

  • Tangu mwaka 2006 EAMCEF imekua ikitoa Sh600 milioni kwa mwaka kwa wananchi wanaopakana na hifadhi za misitu ya Amani, Magamba na Nilo ambazo ni sehemu ya safu za milima ya Tao la Mashariki kwa lengo la kuweka ulinzi wa bioanuwai katika hifadhi hizo.

Lushoto. Ili kupunguza uharibifu katika msitu wa Magamba uliopo wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga, wananchi katika vijiji 21 vinavyozunguka hifadhi hiyo vimewezeshwa kupanda miti ya parachichi na kufanya kilimo bora.

Miradi hiyo inafadhiliwa na Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki (EAMCEF) ni pamoja na ufugaji nyuki, samaki, kilimo cha miche ya viungo na majiko banifu kwa kaya na taasisi zikiwemo shule.

Vijiji vinavyotekeleza miradi ya upandaji wa miti ya parachichi ni pamoja na Magamba, Migambo, Irente, Kwesimu, Gorogoro na Nywelo.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, mratibu wa mradi wa upandaji miti kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Mfaume Mhonda amesema mradi huo  ulianza mwaka 2013 na hadi sasa kuna vikundi 11 vilivyoanzishwa na wanachama wa vijiji hivyo.

 “Baada ya kutambulisha mradi tunapitia na kutoa elimu ya uanzishaji wa vitalu vya miti, kisha tunafanya ufuatiliaji kama wataalamu ili miradi hii iwe endelevu na tunaona kasi ya kuingia msituni imepungua na wananchi  kupata kipato bila kutegemea msitu,” ameeleza.

Katibu wa kikundi cha upandaji miti cha umoja, Shafii Salehe amesema katika kipindi cha mwaka jana walipanda miche ya miti 10,000 ambapo kati ya hiyo waliuza  6,000 na  2,000 wakaigawa kwenye jamii inayowazunguka na fedha walizopata waligawana na nyingine walinunulia mbegu.

“Kwenye suala la uhifadhi sasa hivi tunatarajia miti ikikua itatusaidia kwenye kuni, mbao na pia kuhifadhi hali ya hewa na kupunguza watu kwenda msituni,” amesema.

Naye Joyce Shedafa ambaye ni mwanachama katika kikundi hicho amesema  mbali na faida ya kiuchumi waliyopata pia wameweza kupanda miti katika mashamba yao na wanatarajia kupata mbao na fito za kujengea, ambapo hapo awali walikuwa wanaenda kukata msituni.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kusini, Kimweri Mnyese amesema mradi huo unasaidia wananchi kutunza mazingira tofauti na ilivyokuwa awali.

Ofisa Miradi wa mfuko huo Kanda ya Kaskazini, Magreth Victor  amesema mradi wa upandaji miti unatekelezwa katika vijiji hivyo kwa lengo la kupunguza uharibifu kwenye msitu uliokuwa ukiharibiwa na shughuli za kibinadamu.

Amesema katika mradi huo wamekuwa wakitoa Sh15 milioni pindi kikundi kinapoandika andiko.

“Kijiji cha Magamba kimenufaika na kilimo cha parachichi za kisasa na ni moja ya miradi ambayo inasaidia kuongeza kipato kama ilivyo kwa wananchi wa Njombe na Iringa, huku kumeanza kuwa na mwamko pia na itapunguza kasi ya kuharibu msitu,” amesema Ofisa huyo.

Mwenyekiti wa kikundi cha utunzaji mazingira Yoghoi, kinachotekeleza mradi wa kilimo bora cha parachichi, Mchungaji Yohana Mtangi amesema walianza mwaka 2017 wakiwa wanajishughulisha miti ya mbao pekee, ila kwa sasa wameongeza na matunda hayo.

Amesema mwaka 2022 walipewa Sh10 milioni na Mfuko wa EAMCEF, wakapanda miche 15,000 ambapo waliuza wakagawana fedha, mingine wakagawa kwa wanavijiji wenzao na mwaka jana walipewa Sh10 milioni ambapo wamepanda mchie mingine 15,000.

 “Mbali na kuwagawia miche hii, tumetoa elimu kwa wananchi wenzetu na mashamba 52 ya kilimo cha parachichi yameanzishwa, sisi kama wanakikundi tunatarajia baada ya muda kuwa na mashamba makubwa na tuweze kuuza parachichi,” amesema.