Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Unyanyapaa, imani potofu vyakwamisha utambuzi wa mapema watoto wenye usonji

Baadhi ya wadau wakijadili masuala mbalimbali kuhusiana na tatizo la wenye usonji.

Muktasari:

  • Utafiti uliofanywa na kituo cha utafiti wa magonjwa yasiyoambukiza (KCRI), kuanzia mwaka 2022 hadi 2024 unaonyesha kuwa watoto wenye tatizo la usonji huchelewa kutambuliwa mapema  na kupatiwa huduma za awali kutokana na imani potofu kutoka kwa baadhi ya wanajamii.

Moshi. Familia zenye watoto wenye changamoto ya usonji zinaendelea kukabiliwa na unyanyapaa, huku tafiti zikionyesha familia nyingi hukimbilia kutafuta msaada kupitia maombi na tiba za jadi.

Hali hiyo huchangia kuchelewa kwa utambuzi wa mapema na kuanza kwa matibabu sahihi kwa watoto hao.

Hayo yameelezwa leo Jumanne, Aprili 28, 2026 na Mkuu wa Idara ya Utafiti na Mafunzo kutoka Kituo cha Utafiti wa Magonjwa Yasiyoambukiza (KCRI), Dk Theonest Ndyetabura alipokuwa  akiwasilisha matokeo ya utafiti wa mradi wa kuboresha mbinu za uchunguzi na utambuzi wa watoto wenye usonji katika Wilaya za Siha, Moshi na Hai, mkoani Kilimanjaro.

Utafiti huo ulifanyika kuanzia mwaka 2022 hadi 2024. Kwa mujibu wa Dk Ndyetabura, matokeo ya utafiti yanaonesha tatizo la usonji bado ni kubwa katika jamii, hali inayosababisha baadhi ya watoto kufichwa nyumbani na hivyo kucheleweshewa kupata huduma stahiki.

“Katika utafiti wetu wa kuanzia mwaka 2022 hadi 2024, tulibaini katika ngazi ya jamii, usonji unahusishwa na imani potofu kama vile kulogwa, uchawi na makosa ya wazazi. Hivyo, watoto wengi wenye changamoto hii hukumbana na unyanyapaa na familia zao mara nyingi hukimbilia msaada wa maombi na tiba za asili,” amesema Dk Ndyetabura.

Amesema katika hatua za awali, wazazi wengi huwapeleka watoto wao kwenye tiba hizo za jadi au maombi kabla ya kuwafikisha hospitalini, jambo linalochelewesha upatikanaji wa huduma za kitaalamu.

“Watoto wengi huanza kupelekwa kwa waganga wa jadi au kwenye maombi kabla ya kufikishwa hospitalini, hali inayosababisha kuchelewa kupata huduma sahihi za kitabibu,” amesisitiza.

Aidha, amesema utambuzi wa mapema wa usonji ni muhimu kwa kuwa humsaidia mtoto kupata matibabu kwa wakati na kuepuka madhara makubwa yanayoweza kujitokeza.

“Utambuzi unapochelewa huwa changamoto kubwa. Watoto wengi tuliokutana nao hugundulika wakiwa na umri wa miaka minne hadi sita, tofauti na viwango vya kimataifa ambapo utambuzi hufanyika kuanzia miaka miwili,” amesema.

Kwa upande wake, mtafiti kutoka KCRI, Dk Alex Gabagambi amesema kuchelewa kwa utambuzi kunachangia kuongezeka kwa ukubwa wa tatizo kwa mtoto.

“Takwimu za dunia zinaonyesha kuwa mtoto mmoja kati ya 100 anaishi na usonji. Hata hivyo, hapa nchini bado kuna upungufu wa tafiti za kutosha kubainisha ukubwa halisi wa tatizo hili,” amesema Dk Gabagambi.

Ameongeza kuwa usonji hauponi moja kwa moja, bali unahitaji utambuzi wa mapema na hatua za uingiliaji wa kitaalamu ili kumsaidia mtoto kuboresha hali yake.

“Ni muhimu mtoto atambuliwe mapema, hasa akiwa na umri wa miaka mitatu au chini ya hapo. Hatua za uingiliaji wa mapema humsaidia mtoto kuimarika na kuwa na maisha bora zaidi baadaye,” amefafanua.

Naye Daktari wa Afya ya Jamii kutoka Hospitali ya KCMC, Florida Muro amesema kuna sababu mbalimbali zinazochangia kuchelewa kwa utambuzi wa watoto wenye usonji, na kusisitiza umuhimu wa jamii kuchukua hatua mapema.

“Ni muhimu kwa jamii kuacha kufumbia macho tatizo hili na kuhakikisha watoto wanatambuliwa mapema ili waweze kupata msaada unaostahili,” amesema Dk Muro.

//block eskimi