Unesco, Korea zinavyochagiza elimu kwa vitendo nchini

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unisco) nchini, Michael Toto kulia akikabidhi moja ya vifaa vya mapishi kwa Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Ethel Kasembe. Picha na Juma Mtanda
Muktasari:
- Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) ikishirikiana na Jamhuri ya watu wa Korea imetoa msaada wa vifaa vyenye thamani ya Sh120.4milioni ili kusaidia kuanzishwa kwa mafunzo ya mitaala mipya ya stashahada ya ufundi katika fani ya uchakataji na usindikaji vyakula na usanifu wa ndani na utiaji nakshi katika chuo cha ualimu wa ufundi stadi Morogoro.
Morogoro. Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) ikishirikiana na Jamhuri ya watu wa Korea imetoa msaada wa vifaa vyenye thamani ya Sh120.4milioni ili kusaidia kuanzishwa kwa mafunzo ya mitaala mipya ya stashahada ya ufundi katika fani ya uchakataji na usindikaji vyakula na usanifu wa ndani na utiaji nakshi katika chuo cha ualimu wa ufundi stadi Morogoro.
Akizungumza leo Jumapili Novemba 19, 2023 katika tukio la kukabidhi vifaa hivyo mjini Morogoro, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) nchini, Michael Toto amesema Unesco itaendelea kuwa mdau wa sekta ya elimu Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa lengo la kuhakikisha wanaweka mazingira wezeshi kwa vijana kuongeza ajira ya kuajiriwa au kujiari.
Toto amesema shirika hilo limekabidhi vifaa hivyo vya kufundishia ufundi vyenye thamani ya zaidi ya Sh120.4 milioni kwa ajili ya mafunzo ya mitaala mipya ya kozi ya stashahada ya ufundi katika fani ya uchakataji na usindikaji vyakula na usanifu wa ndani na utiaji nakshi katika kozi zitazoanza Januari mwaka 2024.
“Huu ni mradi wa kukuza elimu bora Afrika ambao una lenga kunufaisha vituo vya kutolea mafunzo ya ufundi stadi katika chuo cha ualimu wa ufundi Morogoro lakini chuo kimenufaka kwa kufungiwa mitambo mbalimbali ya kufundishia ikiwemo mashine ya kuchakata na kusindika chakula, mashine ya kukoboa na kusaga mahindi, jokofu na kikaushio nishati jua ambapo wataalamu wa kutatoa ujuzi wa utumiaji wa vifaa hivyo na uendeshaji wake na vitatumia nishati ya umeme, gesi na jua.”amesema Toto.
Mkuu wa chuo hicho, Samwel Kaali amesema chuo hicho kitaanza kufundisha kozi mpya za programu za mafunzo katika stashahada ya ufundi katika fani ya uchakataji na usindikaji vyakula na usanifu wa ndani na utiaji nakshi kupitia mradi wa elimu bora kwa maendeleo afrika kozi zitakazoanza Januari mwaka 2024 ili kuwaongeza ujuzi zaidi vijana waweze kujiairi na kuajiriwa.
“Unesco ikishirikiana na serikali ya watu wa jamhuri ya Korea imefadhili programu mbili za mafumzo katika sekta ya kilimo biashara na Sanaa za ubunifu ambapo chuo kitakuwa na dhamana ya kufundisha fani za umalizaji sanifu wa ndani wa majengo na katika magari na upande wa kilimo biashara itafundisha fani ya uchakataji wa chakula na utunzaji wa chakula ikiwa kozi hizo ni mpya.”amesema Kaali.
Mkurugenzi Msaidizi wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi wizara ya elimu, sayansi na teknolojia, Dk Ethel Kasembe amesema Serikali imeweka lengo la kuongeza udahili wa wanafunzi kufikia 3,100 ifikapo mwaka 2027/28 hivyo kuna ulazima wa kuongeza idadi ya walimu wenye ujuzi na imekuwa ikijenga vyuo vingi.