Umuhimu wa kuchangia damu kwa afya, uhai wa jamii
Muktasari:
- Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Afya, Tanzania inahitaji takriban chupa 550,000 za damu kila mwaka ili kukidhi mahitaji ya kiafya.
Dar es Salaam. Katika kuunga mkono juhudi za kitaifa za kuokoa maisha, Benki ya Exim Tanzania kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) imeendesha kampeni ya kitaifa ya uchangiaji damu katika vituo saba nchini, ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kudumu ya kuboresha afya ya umma.
Zoezi hilo lililofanyika kwa wakati mmoja katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mtwara, Kahama na Mbeya, limekusudia kuongeza upatikanaji wa damu salama nchini, huku likiambatana na utoaji wa vifaa 110 vya kisasa kwa NBTS ili kuongeza uwezo wa ukusanyaji na uhifadhi wa damu katika hospitali za umma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika Makao Makuu ya Benki ya Exim jijini Dar es Salaam, Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano, Kauthar D’souza, alisema kuwa benki hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii kupitia kampeni za kiafya, elimu, mazingira, na uwezeshaji wa kiuchumi.
"Tunajivunia kuendesha kampeni hii chini ya kaulimbiu yetu ‘Changia damu na okoa maisha’. Hii ni sehemu ya mpango wetu wa ‘Exim Cares’, unaolenga kugusa maisha ya Watanzania kwa vitendo halisi,” alisema D’souza.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Afya, Tanzania inahitaji takriban chupa 550,000 za damu kila mwaka ili kukidhi mahitaji ya kiafya.
Hata hivyo, NBTS hukusanya wastani wa chupa 350,000 kwa mwaka, na kati ya hizo asilimia 15 huwa haziwezi kutumika kutokana na changamoto mbalimbali kama uhifadhi usio salama au uchunguzi wa kiafya wa damu.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Huduma za Wachangia Damu kutoka NBTS, Judith Charle, aliipongeza Benki ya Exim kwa kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu unaosaidia kuokoa maisha ya maelfu ya Watanzania kila mwaka.
“Kila tone la damu linaweza kuleta tofauti kati ya maisha na kifo. Ushirikiano huu unasaidia kuziba pengo kubwa la upatikanaji wa damu salama nchini,” alisema.
Damu ni hitaji la msingi katika huduma za dharura, upasuaji, uzazi, na matibabu ya wagonjwa wa kisukari, saratani na watoto wenye upungufu wa damu. Kukosekana kwa damu hospitalini huathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma bora za afya.
Mbali na kampeni ya damu, Benki ya Exim imeendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kujenga madarasa yenye samani kwa shule mbili katika wilaya ya Buhigwe, mkoani Kigoma, ikiwa ni sehemu ya mchango wake kwa maendeleo ya elimu nchini.
Kampeni hii ni wito kwa Watanzania wote kuendeleza moyo wa uzalendo na uwajibikaji kwa kuchangia damu mara kwa mara. Kwa kufanya hivyo, kila mmoja anakuwa sehemu ya kuokoa maisha ya mama mjamzito, mtoto aliyezaliwa njiti, au mgonjwa aliye katika hali ya dharura.