Ummy azipa mbinu nchi za Afrika kupunguza vifo kwa wajawazito

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akizungumza kwenye mkutano wa Afya nchini Uswis jana
Muktasari:
- Waziri Ummy aeleza namna Tanzania ilivyofanikiwa kupunguza vifo kwa wajawazito, akisisitiza kuwa utashi wa kisiasa umechochea mafanikio hayo
Geneva. Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema ili kupunguza vifo vya mama na mtoto, nchi za Afrika zinapaswa kuhakikisha wanawake wanapata uwakilishi wa kutosha katika mchakato wa maandalizi ya sera ya afya.
Amesema Tanzania imepiga hatua katika kupunguza vifo vya wajawazito, kutoka 556 katika kila vizazi hai 100,000 hadi 104 kutokana na utashi wa viongozi wakuu wa Serikali na ushirikishwaji wa vyama vya kitaaluma umechangia mafanikio hayo.
Waziri Ummy ametoa kauli hiyo jana Mei 29,2024 Mjini Geneva nchini Uswis katika kikao cha kujadili mbinu shirikishi kupunguza vifo vya wajawazito.
Mkutano huo umeandaliwa na Shirika la Elizabeth Glaser Pediatric Aids Foundation (EGPAF) Shirika la Save the Children pamoja na Umoja wa Afrika.
"Nchi za Afrika zinaweza kuchukua hatua kupunguza vifo vya mama na mtoto, kwanza kwa kuunda sera na sheria zinazolenga kupambana na unyanyapaa na ubaguzi, kuhakikisha kuna uwajibikaji wadau wote,
Pia, ni muhimu kuhakikisha uwakilishi wa kutosha wa wanawake na wazazi katika mchakato wa kutengeneza sera na yanapofanyika maamuzi ya kisiasa ili kuhakikisha maslahi ya watoto yanawakilishwa vyema,"amesema Ummy.
Waziri huyo pia ameshauri uwekezaji kwenye elimu ya afya ya uzazi na kujenga jamii yenye usawa na haki.
Jambo lingine aliloshauri Waziri Ummy nchi za Afrika ziunde sera na sheria kupambana na unyanyapaa na ubaguzi kwa wanawake na watoto na kuweka mfumo wa kuwajibishana
Kwa Tanzania, kiongozi huyo amesema mafanikio hayo yamepatikana kutokana na hatua zilizochukuliwa ikiwamo sharti linalotaka kituo/Hospitali yoyote inayopata kifo cha mjamzito kufanya mapitio katika vituo vya umma ndani ya masaa 24 na kuweka mpango kazi ili kisitokee kifo kingine.
Jambo lingine ni uwekezaji katika miundombinu ya upasuaji kwa wajawazito, dawa za uzazi salama na uwepo wa mfumo wa rufaa wa dharua kwa wajawazito M-Mama, ushirikishwaji wa vyama vya kitaaluma vimefanikisha Tanzania kupata mafanikio makubwa katika kupunguza vifo
Akifungua kikao hicho, Kamishna wa Huduma za Afya Maendeleo ya Jamii kutoka Umoja wa Afrika Balozi Minata Samate, amesema AU itaendelea kushirikiana na nchi wanachama katika kuyafikia malengo ya kuwa na jamii yenye afya bora.
Akichangia mada katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Kitengo cha mama na Mtoto kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO)Dk Anshu Banerjee, amesema kazi ya kupunguza vifo vitokanavyo na wajawazito na watoto wachanga haipungui kwa kiasi kilichotarajiwa.
Amesema vifo vya wajawazito na watoto vinaweza kuzuilika kwa sababu mara nyingi vinasababishwa na magonjwa ya kuambukiza, lishe duni, changamoto za kufikia huduma za afya kutokana na umbali,miundombinu mibovu pamoja na upungufu wa watoa huduma za afya.
Dk Banerjee amesema wasiwasi wake ni juu ya kuongezeka kwa viwango vya vifo vya watoto wachanga, na kusema kuwa maendeleo yaliyopatikana yanarudi nyuma.