Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Umasikini, uelewa mdogo wa sheria watajwa chanzo cha wananchi kupoteza haki

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Musa Kilakala akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kampeni ya msaada ya kisheria ya (Mama Samia legal Aid Campaign) itakayozinduliwa kesho Desemba 13 na kumalizika Desemba 22 mwaka huu. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  • Timu ya wanasheria imepanga kuweka kambi na kutoa msaada wa kisheria Kwa wananchi wa mkoa wa Morogoro kupitia kampeni iliyoanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Sheria na Katiba itakayozunguka na kutoa huduma kwenye Halmashauri tisa, kata, vijiji na mitaa.

Morogoro. Umasikini na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu masuala ya sheria, ikiwemo sheria za ndoa na mirathi, vimetajwa kuwa sababu kubwa zinazochangia wananchi kukosa haki wanaposhiriki mashauri mbalimbali katika mahakama hapa nchini.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Desemba 12, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Musa Kilakala alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Kilakala amesema Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Sheria na Katiba, ameanzisha kampeni ya msaada wa kisheria iitwayo Mama Samia Legal Aid Campaign.

Kampeni hiyo itazinduliwa rasmi kesho, Desemba 13, katika viwanja vya stendi ya zamani ya daladala mkoani Morogoro.

Kwa mujibu wa Kilakala, kampeni hiyo inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu sheria, mifumo ya haki, masuala ya kisheria, na haki za binadamu.

Pia imejikita katika kufanikisha maono ya Rais Samia ya kuimarisha huduma za kisheria kwa wananchi wanyonge, hususan wanawake na watoto.

"Kampeni hii itachangia kudumisha amani, kuongeza kipato kwa wananchi mmoja mmoja, na kuimarisha mshikamano wa kitaifa. Mkoa wetu bado unakabiliwa na changamoto nyingi kama migogoro ya ardhi, mirathi, na ndoa. Nawaomba wananchi wenye changamoto za kisheria kufika kwenye uzinduzi huu ili wapate msaada wa kisheria," amesema Kilakala.

Baada ya uzinduzi, huduma za msaada wa kisheria zitaendelea kutolewa katika ngazi za halmashauri na wataalamu watafika katika kata, vijiji na mitaa mbalimbali, amesema.

Mkuu huyo wa wilaya amesema lengo pia ni kuwafikia wananchi wa vijijini ambao mara nyingi hawana uwezo wa kugharamia wanasheria kwenye mashauri yao.

Kilakala aliongeza kuwa kila halmashauri itachagua kata 10 na vijiji au mitaa 30 kwa ajili ya kampeni hiyo, huku akisisitiza kuwa kampeni inaweza kuendelea katika maeneo mengine pale inapohitajika.

Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Morogoro waliozungumza na Mwananchi kuhusu kampeni hiyo wameonyesha matumaini makubwa.

Saida Rashidi, mmoja wa wananchi hao amesema kampeni hiyo itakuwa mkombozi kwake kwa sababu amekuwa akihangaika kwa muda mrefu kutafuta haki juu ya mgogoro na mwekezaji anayenuia kuondoa makaburi ya familia yake kwa ajili ya ujenzi.

"Kila siku tunafuatilia ofisi za serikali kutafuta haki, lakini hatujafanikiwa. Namshukuru Rais Samia kwa kuleta kampeni hii. Nitahudhuria kwa matumaini ya kupata haki yangu," amesema Rashidi.

Naye Osward Nyamoga, mkazi wa Morogoro, alisema kampeni hiyo itasaidia kupunguza migogoro ya ardhi, ambayo ni changamoto kubwa katika manispaa hiyo.

"Sheria inahitaji uelewa wa kina. Bila elimu ya sheria au uwezo wa kifedha wa kuajiri wakili, mtu anaweza kupoteza haki yake. Rais Samia amefanya jambo kubwa kwa wananchi wa Morogoro," amesema Nyamoga.

Hata hivyo, Nyamoga amesisitiza kuwa kampeni hiyo inapaswa kuwa endelevu na ifikie maeneo ya vijijini, ambako kuna wananchi wengi wasio na uelewa wa sheria wala uwezo wa kifedha kugharamia msaada wa kisheria.