Ukosefu akaunti za benki chanzo wakulima kucheleweshewa malipo

Hamis Liwaka (kushoto) Mkazi wa Mmwindi Kata ya Mbawala akipokea malipo kutoka kwa mwakilishi wa kampuni ya ARA Petroleum Tanzania, Judith Kalugasha. Picha na Florence Sanawa.
Muktasari:
- Wananchi 203 wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara wamechelewa kupata malipo yao ya fidia za mazao wakati wa utafiti wa gesi Nanguruwe kwa kukosa akaunti za benki huku wengine wakiwasilisha akaunti za ndugu zao hali ambayo ilipekea malipo kukwama.
Mtwara. Zaidi ya wananchi 203 wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara wamelazimika kulipwa fedha taslimu baaada ya kushindwa kuwasilisha akaunti zao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa akaunti ya benki.
Akizungumza wakati akikamilisha malipo hayo ya Sh65 milioni yaliyosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kulipwa na Kampuni ya ARA Petroleum Tanzania, mwakilishi wa kampuni ya ARA, Judith Kalugasha amesema kuwa watu wengi walileta akaunti za ndugu zao hivyo majina hayakufanana hivyo kushindwa kupata malipo yao kwa wakati.
Amesema kuwa changamoto hiyo iliyojitokeza ambayo wengi hawakufungua akaunti huku wengine majina yao na akaunti yakiwa hayafanani hivyo pesa kurudi.
“Tumelazimika kulipa fedha taslimu wengi wao hawapo na wengine wametangulia mbele ya haki na mchakato wa mirathi bado tunashindwa kuwalipa kwakuwa hawajakamilisha taratibu.
Mchakato ulikuwa mrefu tumelipa kwa awamu nne hii ni ya mwisho kwakweli tunawashukuru wananchi wamekuwa wavumilivu licha ya mradi huo kuharibu mazao zaidi ya mwaka sasa lakini changamoto kubwa ilikuwa kwenye akaunti zao,” amesema Kalugasha.
Meneja wa mradi Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Patrick Kabwe amesema “Malipo sasa yamekamilika tuliona wananchi wanapata changamoto ya kupata malipo kupitia akaunti zao na sasa tumemaliza.
Unajua wakati wa utafiti wa huu mradi tulilazimika kutengeneza barabara ili kupitisha mashine ndio manaa ule uharibifu wa mazao ukatokea ambapo leo tunakamilisha malipo ya wananchi wote ambao tuliharibu mazao yao,” amesema Kabwe.
Naye Jacobo Haule kutoka katika Kitengo cha Mawasiliano TPDC amesema kuwa malipo ya walioharibiwa mazao yao wakati wa utafiti ulifanywa na TPDC wakishiriiana na ARA Petroleum Tanzania malipwa huku siku zikiongezwa kwa wale ambao hawakufika awamu ya mwisho ya nne.
"Tuko kwenye hatua ya mwisho waliobakia ni wachache ni vema walioathiriwa wote wakajitokeza na kwakuwa tumeongeza siku mbili kwa waliochelewa kupata taarifa ama ambao walihusika lakini kwenye orodha hawapo.
Hata hivyo changamoto kubwa kipindi cha uthamni wananchi waliwasilisha akaunti za NMB alafu salio wenaenda CRDB kuangalia salio jambo ambalo tunaamini kuwa ni walikuwa wanakosea hivyo tunawaelimisha.
Tulienda katika Kijiji cha Dihimba tukakuta watu 20 ambao walisema hawajalipwa baada ya kuangalia kumbe pesa tayari imeliipawa lakini hawajui kama wamelipwa,” amesema Haule.
Vilevile mkazi wa Nanguruwe Mtwara, Aziza Mwalimu amesema kuwa zoezi hilo amelisubiria kwa muda mrefu ambapo ambapo leo amepata malipo yake na kuridhika na malipo hayo.