Ukaribu wa Roman Abramovich na Vladmir Putin

Muktasari:
- Katika kuhitimisha mfululizo wa makala hizi, uhusiano wa karibu ulioko kati ya tajiri Roman Abramovich na viongozi wakuu wa Russia — kwanza na Rais Boris Yeltsin na sasa Vladmir Putin — umeufanya Umoja wa Ulaya kumwekea vikwazo vya kibiashara.
Katika kuhitimisha mfululizo wa makala hizi, uhusiano wa karibu ulioko kati ya tajiri Roman Abramovich na viongozi wakuu wa Russia — kwanza na Rais Boris Yeltsin na sasa Vladmir Putin — umeufanya Umoja wa Ulaya kumwekea vikwazo vya kibiashara.
Tangu mwanzo wa mfululizo wa makala hizi, tuliangazia maisha ya Abramovich tangu alipozaliwa katika hali ya umaskini, akaachwa yatima baada ya wazazi wake wote kufariki dunia kabla ya kutimiza umri wa miaka minne na namna alivyolelewa na bibi yake.
Pia tuliona alipoanza biashara ya kuuza midoli na matairi chakavu ya magari, hadi alipojipenyeza na kuwa mmoja wa watu wa karibu sana na marais wa Russia — Yeltsin na baadaye Putin.
Hata hivyo, ni wakati wa kilele cha mageuzi ya kiuchumi ndipo Abramovich alipoanza kujitengeneza kuwa tajiri kama alivyo leo baada ya kununua makapuni kadhaa nchini Russia kwa bei ya chini na kuyauza kwa bei kubwa, kiasi kwamba amekuwa tajiri na mwenye ushawishi mkubwa (oligarch).
Neno “oligarch” lina historia ndefu, lakini limepata maana maalumu zaidi wakati huu kuliko wakati mwingine wowote katika historia yake.
‘Oligarch’ kwa maana ya jadi ni mwanachama au mfuasi wa kundi la watu wenye ushawishi walio kwenye mfumo wa kisiasa ambao hutawaliwa na watu wachache. Kwa ufupi, ‘oligarch’ ni mjumbe katika utawala wa Serikali ya wachache.
Lakini sasa, linatumika zaidi kuelezea kundi la matajiri wa Russia ambao walipata umaarufu baada ya kuanguka kwa Muungano wa Sovieti mwaka 1991. Neno hilo kwa Kigiriki ni ‘oligoi’, ambalo linamaanisha ‘wachache’, na ‘arkhein’, linalomaanisha “kuongoza”. Hii ni tofauti na ufalme (utawala wa mtu mmoja, ‘monos’) au demokrasia (utawala wa watu, ‘demos’).
Kwa maana ya siku hizi, ‘oligarch’ ni mtu tajiri zaidi ambaye utajiri wake umetokana na yeye kufanya biashara na Serikali.
‘Oligarch’ anayejulikana zaidi nchini Uingereza ni Abramovich, mmiliki wa klabu ya Chelsea. Thamani ya utajiri wake inakadiriwa kuwa ni wastani wa dola bilioni 14.3 za Marekani (Sh33.6 trilioni) na alijitajirisha kwa kuuza mali ya awali ya Serikali ya Urusi (sasa Russia) ambayo aliipata kufuatia kuanguka kwa Muungano wa Kisovieti.
Kwa mfano alitengeneza mabilioni ya dola baada ya kuinunua kampuni ya mafuta iliyokuwa inamilikiwa na Serikali ya Russia katika mnada wa mwaka 1995 uliodaiwa kuwa na utata mkubwa.
Abramovich alilipa karibu dola 250 milioni (takriba Sh579.5 bilioni) kwa Sibneft, kabla ya kuiuza tena kwa Serikali ya Russia kwa dola 13 bilioni (Sh30.13 trilioni) mwaka 2005.
Abramovich ndiye mmiliki wa majumba mengi katika maeneo mbalimbali duniani. Tangu aanze kujikusanyia mali yake mwanzoni mwa miaka ya tisini, bilionea huyo amejikita katika maisha ya siasa. Aliwahi kuhudumu kama gavana wa Jimbo la Chukotka nchini humo mwaka 2000, baada ya kushinda asilimia 92 ya kura.
Abramovich anaaminika kuinunua klabu ya Chelsea kwa dola 233 milioni (Sh539,861 bilioni) Juni 2003 kutoka kwa Ken Bates, ambaye alikuwa ameinunua klabu hiyo mwaka 1982.
Alipoinunua Chelsea alianzisha mchakato wa kuipeleka kwenye mafanikio makubwa na matumizi makubwa ya kifedha kwa klabu hiyo, ambayo baadaye imeibuka kuwa klabu kubwa duniani. Chelsea imeshinda mataji karibu yote na kwa sasa ndiyo bingwa mtetezi wa Ligi ya mabingwa Ulaya na mabingwa wa dunia kwa ngazi ya klabu.
Hata hivyo, wakati Russia ikijiandaa kuivamia Ukraine, Abramovich alitangaza mpango wa kuiuza Chelsea na kwamba huo kwake ni “uamuzi mgumu sana” na unamuumiza “sana”.
Bilionea Hansjorg Wyss, amepewa nafasi ya kununua klabu hiyo ya London Magharibi, aliliambia gazeti la Uswisi la Blick, kwamba Abramovich alitaka “kuiuza Chelsea kwa haraka” baada ya tishio la vikwazo kuibuliwa bungeni.
Abramovich anadaiwa kuwa na uhusiano mkubwa na Rais Putin, jambo ambalo hata hivyo amelikanusha.
Katika taarifa yake, Abramovich alisema: “Siku zote nimekuwa nikichukua maamuzi kwa nia njema ya klabu. Kwa hali ilivyo sasa nimechukua uamuzi wa kuiuza kwa sababu naamini hili ni kwa manufaa ya klabu, mashabiki, wafanyakazi, wadhamini na washirika wa klabu. Uuzaji wa klabu hautaharakishwa lakini utafuata taratibu zinazostahili. Sitaomba kulipwa mkopo wowote.”
Hata hivyo, Machi 10, mwaka huu, Abramovich aliwekewa vikwazo na Serikali ya Uingereza kama sehemu ya kupinga uvamizi wa Russia dhidi ya Ukraine.
Yeye ni mmoja wa wafanyabiashara saba matajiri waliowekewa vikwazo, ikiwa ni pamoja na kuzuiliwa kwa mali yao na marufuku ya kusafiri. Orodha hiyo pia inajumuisha mabilionea Igor Sechin na Oleg Deripaska, wote wanaoonekana kuwa washirika wakubwa wa Putin.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson alisema “hakuwezi kuwa na maeneo salama” kwa wale ambao wameunga mkono uvamizi huo.
Serikali ya Uingereza ilisema Abramovich ni “mmoja wa matajiri wachache kutoka miaka ya 1990 kudumisha uhusiano na ushawishi chini ya Putin.”
Tajiri mwingine ni Alisher Usmanov, mfanyabiashara tajiri mwenye ushawishi wa kisiasa anayependelewa zaidi na Rais Putin, akikadiriwa kuwa na utajiri wa thamani ya dola 17.6 bilioni, kwa mujibu wa jarida la Forbes.
Umoja wa Ulaya (EU) unamuelezea Usmanov kama “mfanyabiashara-rasmi” ambaye humsaidia rais (Putin) kutatua matatizo yake ya kibiashara.
Mwingine aliyekumbwa na kadhia hiyo ya vikwazo ni Deripaksa, ambaye wakati Putin alipoingia madarakani, alikuwa tajiri sana, utajiri wake ukipanda kwa takriban dola 28 bilioni.
Ingawa Marekani inasema alihusika katika utakatishaji wa pesa, hongo, wizi na madai yaliyoripotiwa kwamba aliamuru “mauaji ya mfanyabiashara na kuhusika na kikundi cha uhalifu cha Warussia,” yeye mwenyewe amekanusha madai hayo.
Igor Sechin ni tajiri mwingine ambaye uhusiano wake na Putin ni wa ndani na wa muda mrefu. EU ambayo ilitangaza vikwazo dhidi yake Februari 28, mwaka huu ilisema ni mmoja wa washauri wa karibu na wanaoaminiwa zaidi na Putin, akiwa pia ni rafiki yake binafsi, na wawili hao wanadhaniwa kuwa huwasiliana kila siku. Alexey Mille ni rafiki mwingine wa zamani wa Rais Putin. Alianza wakati alipokuwa naibu wa Putin katika kamati ya masuala ya kigeni ya ofisi ya Meya wa St Petersburg katika miaka ya 1990. Mwisho