Ujenzi wa SGR Isaka-Mwanza wafikia asilimia 63

Muktasari:
- Ujenzi wa tuta na madaraja umekamilika na kazi za usimikaji wa reli na ujenzi wa stesheni zikiendelea kwa kasi.
Shinyanga. Meneja wa Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) LOT 5, kutoka Isaka hadi Mwanza, Mhandisi Christopher Kalisti, amesema kuwa kazi kubwa katika ujenzi wa mradi huo imekamilika, huku kazi nyingine zikifanyika kwa kasi.
Hayo yamebainishwa jana, Aprili 4, 2025, wakati wa ziara ya kutembelea mradi unaotekelezwa na kampuni za ujenzi kutoka China, CCECC na CRCC. Hadi sasa, mradi huo umegharimu jumla ya Sh3 trilioni.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mhandisi Kalisti ameeleza kuwa ujenzi wa reli ya kisasa wenye urefu wa kilomita 341, kutoka Isaka hadi Mwanza, ulioanza mwaka 2021, umefikia asilimia 63 ya utekelezaji wake.
Kazi kubwa zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa tuta na madaraja, huku kazi za usimikaji wa reli na ujenzi wa stesheni zikiendelea kwa kasi.
"Mradi huu umegharimu Sh3 trilioni hadi sasa, na utachangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha usafiri na uchumi wa taifa. Tunaendelea na kazi kwa bidii, ili kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati," amesema Mhandisi Kalisti.

Meneja mradi wa ujenzi wa reli ya SGR LOT 5 Isaka hadi Mwanza, Christopher Kalisti akizungumza na waandishi wa habari. Picha na Hellen Mdinda.
Meneja wa Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) LOT 5, Mhandisi Christopher Kalisti, ameongeza kuwa Serikali ilianza utekelezaji wa mradi wa reli ya kisasa inayotumia umeme (SGR) mwaka 2016, kwa lengo la kuboresha usafiri wa abiria na mizigo kwa njia ya reli, kuongeza ufanisi katika sekta ya usafirishaji, na kuchochea maendeleo ya uchumi nchini.
Mradi huo ambao unatekelezwa kwa awamu, umeundwa ili kurahisisha utekelezaji na kuhakikisha kila kipande kinakamilika kwa ufanisi mkubwa.
“Ujenzi wa reli ya kisasa SGR umeanzishwa kwa makusudi ili kuboresha miundombinu ya usafiri na kuimarisha uchumi wa taifa. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa mradi huu unatekelezwa kwa ufanisi mkubwa ili kuchochea maendeleo ya maeneo yote yatakayopitiwa na reli hii,” amesema Mhandisi Kalisti.
Pia, mmoja wa wakazi waishio karibu na maeneo ya mradi, Magdalena William, ameeleza namna ambavyo ujenzi wa mradi huo umewapa fursa mbalimbali za kiuchumi, hususan katika biashara za mamalishe
Magdalena, ambaye ni mjasiriamali katika eneo hilo, amesema wateja wake wengi ni wafanyakazi wa mradi wa SGR.
“Ujio wa mradi huu umekuwa na manufaa makubwa kwetu, hasa sisi kinamama. Biashara yetu ya mamalishe imeendelea vizuri, kwani wateja wetu wengi ni wafanyakazi wanaoshiriki katika ujenzi wa mradi huu wa SGR. Tumepata fursa ya kuongeza kipato na kusaidia familia zetu,” amesema Magdalena.
Mradi wa reli ya kisasa SGR unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha uchumi wa nchi na kuongeza ajira, huku ukiwafaidi wakazi wa maeneo mbalimbali wanaopata fursa za biashara na kazi kupitia utekelezaji wake.
Mkazi wa Kata ya Sekebugolo na mfanyabiashara, Halid Bakari, amesema kuwa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa utakapokamilika, utasaidia kurahisisha usafirishaji wa mizigo na mazao, hasa ya kibiashara, kutoka mkoani Shinyanga hadi mikoani.
“Mradi huu utarahisisha usafirishaji wa mazao kama pamba, dengu, na choroko, na hivyo kuongeza upatikanaji wa masoko kwa wakulima wetu,” amesema Bakari, akiongeza kuwa reli ya kisasa itachangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za usafirishaji.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulizi na Usalama katika Kata ya Sekebugolo, ambaye pia ni diwani wa kata hiyo, Fredinand Lubimbi, ametoa wito kwa wananchi kulinda na kuthamini miundombinu ya mradi huu.
Amesisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayekwamisha utekelezaji wa mradi huo.
“Niwatake wananchi wa kata hii kuwa walinzi wa miundombinu yetu. Kila mmoja ni jukumu lake kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kama ilivyopangwa. Yeyote atakayebainika kuwa anahujumu mradi huu kwa namna yoyote, atachukuliwa hatua kali za kisheria,” amesema Lubimbi.
Hadi sasa, wananchi wengi katika kata hiyo wanaonekana kufurahia fursa zinazokuja na mradi huu, na wameahidi kushirikiana na Serikali kulinda na kudumisha usalama wa miundombinu hiyo ya muhimu.
Mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) nchini Tanzania unatekelezwa kwa awamu tofauti, kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza, na umegawanywa katika vipande mbalimbali.
Awamu ya kwanza ilianza kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro (kilomita 300), awamu ya pili inahusisha kipande cha Morogoro hadi Makutupora (kilomita 422), awamu ya tatu ni kipande cha Makutupora hadi Tabora (kilomita 368), awamu ya nne ni kipande cha Tabora hadi Isaka (kilomita 165), na awamu ya tano inahusisha kipande cha Isaka hadi Mwanza kilomita 341.
Lengo la kuunganisha mikoa mbalimbali ya Tanzania na pia kuunganisha nchi za jirani kama Rwanda, Burundi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ili kurahisisha usafiri wa abiria na mizigo.
Utekelezaji wa mradi huo utachochea maendeleo ya uchumi katika maeneo yote yatakayopitiwa na reli hiyo, huku ikitarajiwa kuongeza ufanisi katika sekta ya usafirishaji.