Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wenye makaburi yaliyopitiwa na SGR walilia kifuta machozi

Mhandisi wa Kipande cha nne awamu ya tano ya Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) Mwanza hadi Isaka, Nastra Chusi (katikati) akitoa maelezo kwa Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alipotembelea na kukagua ujenzi wa reli hiyo kipande cha Mwanza-isaka chenye urefu wa kilomita zaidi ya 241l. Picha na Mgongo Kaitira.

Muktasari:

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Focus Sahani, ujenzi wa reli hiyo yenye urefu zaidi ya Kilometa 341 unaotekelezwa kwa gharama ya Sh3.062 trilioni umefikia asilimia 44.2, ukitarajiwa kukamilika Desemba 2024.

Mwanza. Baadhi ya wakazi wa Kitongoji Stesheni Kata ya Mallya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza ambao makaburi ya ndugu na wapendwa wao yalihamishwa kupisha mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) inayoanzia Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga wamelalamikia kutolipwa kifuta machozi kama ilivyoahidiwa na Serikali.

Ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa zaidi ya kilomita 341 unatekelezwa na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na China Railway Construction Corporation (CRCC) umefikia asilimia 44.2 huku ukitarajiwa kukamilika Disemba 2024 kwa gharama ya Sh3.062 trilioni.

Mbali na kifuta machozi, wakazi wa kitongoji hicho walidai kutopewa ajira katika mradi huo hata zile za kupeperusha bendera na kupanda nyasi kuzunguka tuta itakapolazwa reli hiyo jambo ambalo walidai kuwa linawafanya wasione tija ya utekelezwaji wa mradi huo katika eneo lao.

Akizungumza Novemba 24, 2023 kwa niaba ya wananchi hao Mwenyekiti wa  Kitongoji cha Stesheni Kata ya Mallya wilayani humo, Mugusi Shabani amesema kati ya makaburi 15 yaliyohamishwa eneo la Mwabagalu na Stesheni ni makaburi tisa pekee yaliyofidiwa huku wengine wakiambulia maumivu.

Shabani alimuomba Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kutoa maelekezo kwa Mkandarasi na TRC, ili wazawa wapatiwe ajira hata zisizohitaji ujuzi na kifuta machozi kwa waliokuwa na makaburi ya wapendwa wao eneo mradi ulipopita.

“Watu wanaumia na watu wao waliofukuliwa makabuli yale, mpaka sasahivi kuna baadhi ya watu majina yao hayajarudi, watu wao wamefukuliwa na kuhamishwa lakini mpaka sasahivi hawajalipwa kifuta machozi. Kwa mfano Mwabagalu kuna mama ambaye mwili wa mmewe ulifukuliwa lakini hajalipwa,”amesema Shabani

Akizungumza mbele ya waziri huyo, Mbunge wa Sumve (CCM), Kasalali Mageni amesema wananchi wa eneo hilo hakuna hata mmoja alioyepata ajira za vibarua.

“Wakasema hata zile za kushika bendera wamekosa, pia kuna lambo la maji lililoharibiwa na mradi lilianza kutengenezwa lakini halijakamilika zimekuwa ni stori tu. Wananchi wanaomba changamoto hizo zitatuliwe,”amesema

Akijibu kuhusu malalamiko hayo, Meneja wa mradi wa SGR Mwanza-Isaka kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), Christopher Kalisti amewataka wananchi hao kuwa na subira huku akiwahakikishia kwamba hakuna atakayeachwa bila kulipwa kifuta machozi.

“Tunajua kuna baadhi ya watu bado hawajakamilisha kwenye fidia na kuna wengine tayari wameshalipwa. Ni zoezi ambalo linaendelea na tunaahidi kila mtu tutamsikiliza na tutahakikisha kwamba anapata haki yake, taarifa zote tunazo hata kama kuna walakini huwa tunapita tena kuhakiki ili tumalize kabisa hiyo changamoto,”amesema Kalisti

Naye Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ameagiza TRC na mkandarasi anayetekeleza mradi huo kutoa ajira zisizohitaji ujuzi ikiwemo kupanda nyasi kwenye tuta la reli hiyo huku akionya urasimu na kutanguliza undugu katika ajira hizo.

“Yote mliyoyasema ninayachukua naenda kuyafanyia kazi ikiwemo kuhusu fidia, ajira na mengine. Hapa sitaweza kuyajibu lakini nawaaahidi nitayafanyia kazi kwa wakati,”amesema Profesa Mbarawa