Ugonjwa wa ajabu ulioua watano Kagera watambulika

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu,

Muktasari:

  • Serikali imesema, ugonjwa uliambukiza watu wanane na kuua watu watano mkoani Kagera ni Marburg.

Dar es Salaam. Ugonjwa wa ajabu uliosababisha vifo vya watu watano kati ya wanane waliougua wilayani Bukoba Vijijini mkoani Kagera umetambuliwa kuwa ni Marburg.

 Imesema ugonjwa huo huambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine au kutoka kwa mnyama kwenda kwa binadamu.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 21, 2023 jijini Dar es Salaam.

Waziri Ummy amesema ugonjwa huo hauna tiba mahususi bali hutibiwa kwa dalili husika anazokuwa nazo mtu.

“Hadi kufikiwa leo siku tano tangu kuripotiwa ni watu nane ndio wameambukizwa na vifo ni vitano na watatu bado wanaendelea na matibabu,

“Tumefanikiwa kudhibiti ugonjwa huu haujatoka nje ya eneo lililolumbwa na ugonjwa huu,” amesema.

Machi 16, 2023 na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu siku chache baada ya ugonjwa huo kuripotiwa amesema umetokea katika vijiji vya Bulinda na Butayaibega vilivyopo katika kata za Marua Kanyangereko wilayani Bukoba

Leo Profesa Nagu amesema watu hao walipata dalili za homa, kutapika, kutokwa na damu maeneo mbalimbali ya mwili na figo kushindwa kufanya kazi.

Hivyo ili kudhibiti ugonjwa huo usisambae, amewataka watu kuepuka kumgusa mgonjwa au majimaji ya mwili mfano mate, machozi, damu, mkojo na kinyesi yatokayo kwa mgonjwa ama mtu mwenye dalili hizo.

Amesema iwapo mtu atalazimika kumhudumia mgonjwa kwa dharura, achukue tahadhari ya kujikinga majimaji yoyote kabla ya kumhudumia.