UDSM yamtunuku Rais AfDB udaktari wa heshima

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jakaya Kikwete akimtunuku tuzo ya heshima ya shahada ya udaktari wa sayansi Rais wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk Akinwumi Adesina.
Muktasari:
- Profesa Mukandala amesema kwa mujibu wa kanuni za tuzo za utoaji wa shahada ya heshima ya chuo hicho ya mwaka 2014, shahada ya heshima inaweza kutolewa kwa mtu mwenye shahada ya kwanza ambaye amechangia kipekee katika kuendeleza tasnia ya ujifunzaji.
Dar es Salaam. Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk Akinwumi Adesina ametunukiwa shahada ya heshima ya udaktari wa sayansi na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam 'honoris causa' kutokana na mchango wake wa Afrika kupitia sera za fedha na programu bunifu za maendeleo.
Dk Adesina ametunukiwa tuzo hiyo leo Ijumaa Juni 13,2025 na Mkuu wa chuo, Jakaya Kikwete ambaye ni rais mstaafu, katika mahafali ya 55 ( duru ya kwanza) yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Uwepo wa kutunukiwa tuzo hiyo ulidokezwa na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Balozi Mwanaidi Maajar aliyesema kama ilivyo desturi ya UDSM kutoa shahada ya heshima kila baada ya kipindi kisichopungua miaka mitatu.
"Leo tunatunuku shahada ya heshima ya falsafa kwa mmoja wa wataalamu waliochangia kiasi kikubwa maendeleo ya Afrika, huyu si mwingine ni Dk Akinwumi Adesina Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
"Tunamtunuku heshima hii kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kuibadilisha Afrika kupitia sera za fedha na programu bunifu za maendeleo," amesema Balozi Maajar.
Kabla ya kutunukiwa tuzo hiyo, Makamu Mkuu wa zamani wa Udsm, Profesa Rwekaza Mukandala akisoma wasifu mfupi wa Dk Adesina amesema kiongozi huyo amezaliwa mwaka 1960 nchini Nigeria katika familia ya watoto wa nne yeye akiwa wa pili.
Amesema baba yake, Adesina alikuwa mfanyakazi kazi wa shambani baadaye akaajiriwa Serikali ambapo akapata nafasi nzuri ya kuwasomesha watoto wake. Ingawa Dk Adesina alipenda kusoma udaktari kutokana na ushawishi wa baba yake lakini alijikuta akiangukia kwenye sekta ya kilimo.
"Aliomba kusomea udaktari wa binadamu mumara tatu, lakini mara zote alipangiwa kwenye kozi ya kilimo.Taalumu hii ndio baadaye ikawa wito wake wa maisha," amesema Profesa Mukandala.
Profesa Mukandala amesema Dk Adenisa ni mtaalamu wa uchumi kilimo mashuhuri Afrika na mwandishi mbunifu aliyeandika machapisho zaidi ya 70 kuhusu sayansi na maendeleo ya kilimo na sera zake za umma zimeleta mabadiliko chanja kwa mamilioni ya wananchi.
" Dk Adesina ni mfano halisi wa muunganiko nadra wa ubora wa kitaaluma, uongozi wa kimaono na athari chanya katika jamii, mambo ambayo shahada za heshima zimekusudiwa kuyatambua.
"Kutoka katika mwanzo wa maisha ya hali ya kawaida hadi viongozi mwenye ushawishi wa maendeleo Afrika Dk Adesina ameendelea kuonesha dhamira ya maisha yake katika kutatua changamoto halisi za dunia, ikiwamo usalama wa chakula," amesema
Vigezo vya kutoa shahada ya heshima
Profesa Mukandala amesema kwa mujibu wa kanuni za tuzo za utoaji wa shahada ya heshima ya chuo hicho ya mwaka 2014, shahada ya heshima inaweza kutolewa kwa mtu mwenye shahada ya kwanza ambaye amechangia kipekee katika kuendeleza tasnia ya ujifunzaji.
"Pili awe ametoa mchango mkubwa na wa kipekee katika matumizi ya maarifa ya kutatua tatizo halisi, sambamba kutoa mchango wa kutetea haki za binadamu," amesema Profesa Mukandala.
Kutokana na hilo, Profesa Mukandala amesema wakati wa uongozi wa Dk Adenisa, AfDB ilipitisha mpango mkakati wa kuchangia maendeleo ya Tanzania ukilenga kuboresha maisha ya Watanzania na kuendeleza ushirikiano wa kikanda.
"Mkakati huu una maeneo mawili ya kipaumbele ikiwemo miundombinu endelevu kwa ajili ya uchumi shindani na mazingira bora ya sekta binafsi ili kuongeza ajira.
"AfBD imeunga mkono miradi mbalimbali uendelezaji wa miundombinu ya kuboresha usafiri ikiwemo majini, reli 'SGR' na barabara na viwanja vya ndege.Pia benki imesaidia mageuzi ya kilimo na kuiwezesha Tanzania kuifikia asilimia 128 ya utoshelevu wa chakula," amesema Profesa Mukandala.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu , Profesa William Anangisye amesema jumla ya wahitimu 828 wamehitimu katika ngazi ya shahada za uzamivu (58), shahada za umahiri (588) stashahada za uzamili (9) shahada za awali (165),stashahada (5) na ashashahada(3).
"Mchanganuo unaonesha katika duru ya kwanza ya mahafali ya 55, wanawake katika shahada za awali ni asilimia 48, umahiri asilimia 49 na uzamivu asilimia 31 ya wahitimu wote," amesema Profesa Anangisye.
Profesa Anangisye amewataka wahitimu hao kutumia elimu walioipata kuirudisha faida ya elimu kwa jamii kwa vitendo, akiwataka kuthibitisha uwezo wao.
"Mabadiliko yanahitaji watu wanaothubutu, sasa ni wakati kuchukua hatua, kuandika kuzungumza kwa busara na kushughulikia changamoto za jamii kwa njia ya ubunifu na yenye maadili kwa kuzingatia utamaduni na mila za Mtanzania,"
"Elimu imewaongezea thamani kwa sasa mna nafasi ya kipekee ya kuwa mawakala wa mabadiliko katika sekta ya umma, binafsi, kijamii na kimataifa. Wazazi, walezi, rafiki na Taifa kwa hamu kubwa wanasubiri mchango wa mawazo yenu, vipawa na ujasiri,"
Katika hatua nyingine, amewakumbusha wahitimu hao kushiriki uchaguzi ambao ni haki ya kila Mtanzania mwenye umri wa kupiga kura.
"Niombe kila mmoja wetu ambaye yupo hapa na popote mnaponisikiliza ndani ya mipaka ya Tanzania, kushiriki katika mchakato wa kupiga kura," amesema Profesa Anangisye.
Alichokisema Dk Adesina
“Ninashukuru sana mkuu wa Chuo Kikuu, Makamu Mkuu wa Chuo, Baraza la Chuo Kikuu, walimu na wafanyakazi wote wa Chuo Kikuu kwa kunitunuku shahada ya heshima leo kutoka chuo kikuu mashuhuri zaidi hapa Tanzania,” amesema Dk Adesina.
Kwa mujibu wa Dk Adesina ana mapenzi ya dhati na Tanzania, jambo lililomfanya aendelee kurudi mara kwa mara akiwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), na hakuna rais mwingine wa benki hiyo aliyewahi kutembelea Tanzania mara nyingi zaidi yake.
“Tunaamini katika ahadi ya Tanzania, ahadi inayozaliwa kila siku hapa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mojawapo ya vyuo vikuu vinavyoongoza barani Afrika.
"Ninapowaangalia ninyi wahitimu wa mwaka 2025, nawaona kama kizazi kilichoandaliwa na kufundwa kwa maarifa makubwa. Kwa kuhitimu leo, mmepata uhuru wenu, uhuru wa kuikabili dunia, uhuru wa kuleta mabadiliko duniani,” amesema Dk Adesina.