Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uchimbaji holela madini chanzo kuongezeka kwa tope Ziwa Rukwa

Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Rukwa, Emmanuel Kisendi akizungumza na Mwananchi Digital Ofisini kwake leo Jumatano Julai 8,2026. Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

  • Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Rukwa imewaonya wachimbaji wa madini kuacha kutumia kemikali na kufanya shughuli za uchimbaji katika mito inayomwaga maji ziwani, ikisema hatua hizo zinaathiri mazingira na mfumo wa ikolojia wa bonde hilo.

Mbeya. Uchimbaji holela wa madini ya dhahabu katika Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, umetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia ongezeko la tope katika Ziwa Rukwa.

Pia kuna kuongeza kina cha maji na kuhatarisha maeneo ya wananchi wanaoishi pembezoni mwa ziwa hilo.

Akizungumza leo Jumatano, Julai 8, 2026 jijini Mbeya, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Rukwa, Emmanuel Kisendi amesema uchimbaji holela wa madini, matumizi ya kemikali, kilimo na shughuli nyingine za kibinadamu zisizozingatia sheria ndani ya hifadhi za mito, zinachangia uharibifu wa mazingira.

Kisendi amesema shughuli hizo pia zinasababisha ongezeko la tope linalosombwa na maji ya mito na kuingia Ziwani Rukwa, jambo linaloweza kuongeza hatari ya mafuriko kwa wananchi wanaoishi jirani na ziwa hilo.

"Shughuli za kijamii zimechangia kwa kiwango kikubwa kuathiri Ziwa Rukwa. Hali hiyo inaweza kusababisha mafuriko kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa ziwa kutokana na kuongezeka kwa kina cha maji," amesema.

Amesema takwimu za kipindi cha mwaka 2020 hadi 2023 zinaonyesha kiwango cha maji katika ziwa hilo kiliongezeka kwa takribani mita nne, hali iliyosababisha kupanuka kwa eneo la maji na kuongeza hatari kwa makazi yaliyopo jirani.

Hata hivyo, amesema bodi inaendelea na tafiti kubaini kiwango cha mchango wa mvua nyingi na shughuli za kibinadamu katika kusababisha ongezeko hilo.

"Uchimbaji wa madini ndani ya mito haukubaliki. Wenye vibali halali wanapaswa kuzingatia masharti ya sheria na kutotumia kemikali wakati wa uchenjuaji wa madini ili kulinda rasilimali za maji," amesema Kisendi.

Amesema uchafuzi wa maji unaotokana na shughuli za kiuchumi na kijamii unaendelea kuwa tishio kwa mazingira ya Bonde la Ziwa Rukwa, ikiwemo kupungua kwa ubora wa maji na kuathiri viumbe hai wanaotegemea mfumo huo.

Kisendi amesema changamoto nyingine inayolikabili bonde hilo ni uvamizi wa hifadhi za mito, ambapo baadhi ya wananchi wameendelea kufanya shughuli za kilimo na shughuli nyingine katika maeneo yasiyoruhusiwa.


Bodi yaeleza mikakati

Kisendi amesema bodi inaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria za rasilimali za maji ili kuhakikisha shughuli za uchimbaji wa madini, kilimo na nyinginezo hazisababishi madhara katika mito inayolisha Ziwa Rukwa.

Amesema pia wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda hifadhi za mito, huku wakiwahamasisha kuondoka katika maeneo hatarishi badala ya kutumia nguvu.

Aidha, bodi imeendelea kuweka alama za mipaka ya hifadhi za mito na ziwa ili kuwasaidia wananchi kutambua maeneo ambayo hayaruhusiwi kufanyiwa shughuli za kibinadamu.

Amesema iwapo wananchi wataendelea kukaidi maelekezo hayo, mamlaka zitachukua hatua kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Namba 11 ya mwaka 2009 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2022 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004.

"Sheria zinakataza shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka kingo za mito isipokuwa kwa kibali maalumu kutoka mamlaka husika," amesema.


Chunya yaeleza hatua

Kwa upande wake, Ofisa Mazingira wa Wilaya ya Chunya, Lucas Deodory amesema ofisi yake imeendelea kutoa elimu kwa wachimbaji na wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira licha ya changamoto ya uvamizi wa maeneo ya mito kwa shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

Amesema wamekuwa wakishirikiana na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Rukwa kufanya vikao vya uhamasishaji kuhusu marufuku ya kufanya shughuli za kijamii, hususan uchenjuaji wa dhahabu, ndani ya maeneo ya hifadhi za mito.

Amesema changamoto kama hiyo iliwahi kujitokeza katika maeneo ya uchimbaji wa madini ya shaba, ambapo baadhi ya wachimbaji walivamia maeneo yasiyoruhusiwa na kuharibu miundombinu, hali iliyosababisha mamlaka kuchukua hatua na kuweka alama za mipaka.

Mkazi wa Kibaoni, Wilayani Chunya, Fabian Lwitiko amesema elimu kwa wachimbaji na wananchi ni muhimu katika kupunguza uharibifu wa mazingira.

"Mimi ni mchimbaji mdogo. Changamoto ipo, lakini tunaomba mamlaka ziendelee kutoa elimu na kusimamia sheria bila kusita ili kulinda mazingira na vyanzo vya maji," amesema.

Naye Chausiku Mturo amesema shughuli za kibinadamu zinazofanyika ndani ya hifadhi za mito zimechangia kuharibika kwa mazingira na kupungua kwa viumbe hai, wakiwemo samaki na dagaa ambao ni chanzo muhimu cha chakula na kipato kwa wananchi.