Serikali yaweka nguvu bonde la ziwa Rukwa
Mbeya. Naibu Waziri wa Maji Mhandisi, Maryprisca Mahundi amesema wizara yake imeelekeza jicho kwenye Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Rukwa kuwa kitovu cha usimamizi mzuri wa rasilimali za maji kati ya mabonde tisa nchini yanayosimamiwa na wizara.
Mhandisi Mahundi amesema hayo jana Jumanne, Septemba 12, 2023 mbele ya kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Abdallah Shaibu alipokuwa akikagua miundombinu ya katika chanzo cha Ivumwe kinachozalisha maji zaidi ya lita milioni 29 kwa siku kinachosimamiwa na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Rukwa.
“Kiongozi wa mbio za mwenge, Bonde la ziwa Rukwa limekuwa tegemeo kubwa katika wizara kati ya mabonde tisa nchini hivyo jicho letu kubwa tumelielekeza hapo na mafanikio haya yanatokana na usimamizi mzuri wa Mkurugenzi mtendaji Mhandisi, Grace Chitanda kwa kushirikiana na watendaji wake,” amesema
Amesema kuwa mafanikio hayo makubwa yanatokana na uwekezaji wa fedha za miradi zinazotolewa na Serikali katika kuhakikisha jamii inapata huduma muhimu za maji safi na salama.
“Ninapozungumzia miradi ya maji ukiwepo wa mto Kiwira ambao Serikali imetoa zaidi ya Sh117 bilioni sitoacha kumshukuru dada yangu, Spika wa Bunge na Mbunge Mbeya mjini, Dk Tulia Ackson amekuwa msaada mkubwa wa kuishawishi kuleta mabilioni ya fedha kwa ajili ya miradi mikubwa ya maji” amesema
Spika wa Bunge na Mbunge Mbeya Mjini , Dk Tulia Ackson amesema kitendo cha Serikali kutoa fedha zaidi ya Sh117 bilioni kwa ajili ya mradi wa maji Kiwira utakuwa mwarobaini wa Watanzania kuondokana na hadha ya maji.
“Mradi huo utakuwa msaada mkubwa kwa Wanambeya kupata huduma ya maji ya uhakika, sambamba na kupokea fedha kwa ajili ya kuboresha miradi ya elimu, afya na miundombinu ya barabara njia nne na hivi karibuni wanatarajia Serikali kuboresha kilometa 400 za miundombinu ya barabara katika Jiji la Mbeya,” amesema Dk Tulia
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Rukwa, Mhandisi ,Grace Chitanda amesema chanzo hicho kina uwezo wa kuzalisha maji lita zaidi ya milioni 29 na kuhudumia wakazi 116,253 huku kikiwa cha kwanza cha mfano Barani Afrika katika eneo tengefu lenye Gn 236.
“Chanzo cha Ivumwe ni kati ya vyanzo 24 vilivyotambuliwa na kuhifadhiwa kwenye eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 1,459,000 ambalo limekuwa tegemeo kubwa katika utunzaji na uhifadhi wa asili” amesema.
Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa ,Abdala Shaibu ameonya wananchi kuacha tabia ya kuendeleza shughuli za kilimo na ufugaji ndani ya mita 60 za hifadhi za maji ili kutunza ikolojia ,viumbe hai na uchumi wa Taifa.