Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mapinduzi ya viwanda yatajwa nguzo ukuaji wa uchumi Afrika

Waziri wa Fedha wa Tanzania, Balozi Khamis Mussa Omar.

Muktasari:

  • Imeelezwa kuwa nchi nyingi za Afrika bado hazijanufaika ipasavyo na fursa za viwanda kutokana na changamoto za kimfumo.

Banjul, Gambia. Waziri wa Fedha wa Tanzania, Balozi Khamis Mussa Omar amesema nchi za Afrika zinapaswa kuchukua hatua madhubuti za kisera na kikodi ili kuharakisha maendeleo ya sekta ya viwanda kwani ndiyo njia muhimu ya kukuza uchumi, kuongeza ajira na kupanua masoko ya bidhaa za Afrika.

Akizungumza katika mjadala kuhusu nafasi ya sekta ya viwanda katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa Afrika leo Jumatano, Julai 8,2026 uliofanyika pembeni mwa mkutano wa African Caucus wa mwaka 2026 mjini Banjul, Gambia, Balozi Omar amesema nchi nyingi za Afrika bado hazijanufaika ipasavyo na fursa za viwanda kutokana na changamoto za kimfumo.

Amesema viwanda vina mchango mkubwa katika kuongeza thamani ya mazao na malighafi zinazozalishwa barani Afrika hivyo kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji jumuishi wa uchumi.

“Tunahitaji sera na mifumo ya kodi inayowezesha uwekezaji na uzalishaji wa ndani ili viwanda viweze kutoa ajira zaidi, kuongeza uzalishaji na kuimarisha mauzo ya nje,” amesema.

Balozi Omar amesema Tanzania imeendelea kutekeleza sera na hatua mbalimbali za kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda, ikiwemo kutoa vivutio vya kikodi na kuimarisha mazingira ya biashara ili sekta binafsi iweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi.

Amesema Serikali tayari imeanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kukuza uchumi wa Tanzania kufikia dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050, huku sekta binafsi ikitarajiwa kuchangia asilimia 70 ya ukuaji huo kupitia uzalishaji na uwekezaji wa viwandani.

Hata hivyo, nchi nyingi za Afrika bado zinakabiliwa na changamoto zinazokwamisha kasi ya mapinduzi ya viwanda, ikiwemo uhaba wa mitaji, masoko, miundombinu ya nishati na usafiri pamoja na upungufu wa rasilimali watu wenye ujuzi.

“Changamoto hizi zikitatuliwa, Afrika inaweza kushuhudia mapinduzi makubwa ya viwanda yatakayochochea ukuaji wa uchumi na kubadili maisha ya wananchi,” amesema.

Amesema Serikali inaendelea kuimarisha maeneo maalumu ya uwekezaji na kutoa vivutio kwa wawekezaji pamoja na wafanyabiashara wachanga, ikiwemo kuwaondolea kodi kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kuwawezesha kukuza mitaji yao.

Alitumia nafasi hiyo kusisitiza kuwa mafanikio ya jitihada hizo yatategemea ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma na binafsi.

“Mazungumzo ya mara kwa mara kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kutatua changamoto za biashara na kuboresha mazingira ya uwekezaji,” amesema.

Alizitaka Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuongeza usaidizi kwa nchi za Afrika katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu inayochochea maendeleo ya viwanda na kuongeza thamani katika mnyororo wa uzalishaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi za kundi la kwanza la Afrika, Dk Zarau Wenderine Kibwe amesema taasisi hiyo iko tayari kuendelea kushirikiana na nchi za Afrika katika kufadhili miundombinu ya viwanda ili kuongeza ajira, uzalishaji na mauzo ya bidhaa na huduma ndani na nje ya bara hilo.

Mkutano wa African Caucus unawakutanisha mawaziri wa fedha, magavana wa benki kuu na viongozi wa taasisi za kifedha za kimataifa kujadili vipaumbele vya maendeleo ya uchumi wa Afrika na namna ya kuimarisha ushirikiano katika upatikanaji wa fedha za maendeleo.