Prime
Tuzo ya fidia ya Sh450 milioni aliyopata mkazi wa Tanga yayeyuka
Muktasari:
- Mwananchi huyo alifungua shauri la madai ya fidia dhidi ya Kampuni ya Airtel Tanzania PLC, akilalamikia mnara wa mawasiliano uliojegwa karibu na nyumba yake ya kuishi uliokuwa umefunga majereta mawili
Tanga. Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Tanga, imebadilisha hukumu na tuzo ya Sh450 milioni aliyopata mwananchi wa jijini Tanga, Marika Mwakichui kwa kile alichokuwa akilalamikia kuwa ni kelele zilizokuwa zinasababishwa na jenereta.
Mwananchi huyo alifungua shauri la madai ya fidia dhidi ya Kampuni ya Airtel Tanzania PLC, akilalamikia mnara wa mawasiliano uliojegwa karibu na nyumba yake ya kuishi uliokuwa umefunga majereta mawili.
Mwakichui alidai kero hiyo ya kelele ilikuwa mbaya kiasi cha kuathiri afya yake na hatimaye kumsababishia mateso yanayohusiana na magonjwa ya moyo na mishipa (cardiovascular complications), hivyo akafungua kesi hiyo.
Hukumu iliyompa tuzo hiyo ilitolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga.
Hata hivyo, furaha ya kupata tuzo hiyo ya fidia ya Sh450 milioni dhidi ya Kampuni ya Airtel Tanzania PLC, haikudumu kwa mwaka mmoja, baada ya Jaji Happines Ndesamburo katika hukumu yake ya Mei 5, 2026 kubatilisha hukumu hiyo.
Hii ni baada ya Kampuni ya Airtel Tanzania PLC kukata rufaa kupinga hukumu hiyo na tuzo akiegemea sababu nane, Jaji Ndesamburo alisema mwananchi huyo alishindwa kuthibitisha kesi yake kwa viwango vinavyokubalika kisheria.
Sababu za rufaa
Ikiwakilishwa na mawakili Gasper Nyika na Samah Salah, Kampuni ya Airtel Tanzania PLC ilijenga hoja kuwa hakimu aliyeamua kesi hiyo alikosea kisheria na ukweli katika kushikilia kwamba kesi hiyo ilifunguliwa ndani ya muda.
Kwa kufanya hivyo, mawakili hao walieleza kuwa, hakimu alishindwa kutambua kuwa msingi wa tatizo hilo kama alivyodai mwananchi huo ulianza mwaka 2004 wakati jenereta zilipowekwa na sio wakati wa taarifa ya matibabu ilipotolewa.
Pia, mawakili wa kampuni hiyo walieleza kuwa hakimu huyo alikosea kisheria kwa kushindwa kutambua kutokuwepo kwa Ripoti ya Tathmini ya Mazingira) (EIA) au ushahidi wa kiufundi unaohitajika chini ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na Tathmini na Ukaguzi wa Athari kwa Mazingira.
Walidai hakimu alikosea kisheria katika tathmini ya ushahidi kwa kushikilia kuwa ugonjwa wa moyo na mishipa uliongezeka au unasababishwa na kelele kutoka kwa jenereta wakati ripoti ya daktari haikufanya hitimisho hilo.
Mbali na sababu hiyo, walidai hakimu alikosea kumpa mjibu rufaa tuzo ya Sh450 milioni bila uthibitisho wowote mahususi wa hasara au gharama za matibabu zilizotumika, kinyume na kanuni inayosimamia malipo ya uharibifu.
Wakili wa mjibu rufaa, Ramadhan Rutenge alijaribu kupangua hoja hizo.
Uamuzi wa Mahakama
Jaji Ndesamburo katika hukumu yake iliyowekwa mtandaoni alisema katika kuamua rufaa hiyo, atajielekeza katika maeneo manne na moja ni kama shauri hilo lilifunguliwa nje ya muda wa kisheria unaotaka lifunguliwe ndani ya miaka mitatu.
Hoja zingine ni kama Mahakama ilihamishia mzigo wa kuthibitisha kesi kwa mrufani, kama mlalamikaji aliweza kuthibitisha kesi kwa viwango vinavyokubalika kisheria na kama tuzo ya Sh450 milioni aliyopewa mjibu rufaa ilikuwa na uhalali.
Kuhusu hoja kama shauri lilifunguliwa ndani ya muda, mlalamikaji alidai kuwa shauri hilo lilifunguliwa ndani ya muda kwani alianza kukumbana na matatizo ya kiafya mwaka 2016 na alifahamu suala la matatizo ya moyo mwaka 2021.
“Hakuna ubishi kuwa madai ya shauri hilo yamejengwa katika fidia ya kero. Ni sawa na ukweli kwamba vitendo vya aina hii viko chini ya muda wa kizuizi cha miaka mitatu chini ya Sheria ya Ukomo wa Sheria,”alisema Jaji Ndesamburo.
Jaji alisema kinachobishaniwa ni lini hasa mgogoro au kero hiyo ilianza.
“Kutoka kwa rekodi za kesi, ni dhahiri kuwa kero inayodaiwa inatokana na kelele zinazotolewa na jenereta zilizowekwa kwenye mnara wa mawasiliano wa Mrufani iko karibu na makazi ya mjibu rufaa tangu mwaka 2004,”alisema Jaji.
“Zaidi inaonekana kwamba jenereta zilizotajwa zimebaki kufanya kazi na kelele zimeendelea kuwepo hadi leo. Nina maoni yanayozingatiwa kuwa Sehemu ya tano ya Sheria ya Ukomo inapaswa kusomwa pamoja na Kifungu cha 7 cha Sheria hiyo,” alisema jaji huyo.
Alisema katika shauri haitakuwa sahihi kusema tatizo lilianza mwaka 2016 kama alivyosema mrufani au mwaka 2021 kama alivyosema mjibu rufaa.
“Kwa msingi huo na kwa kuongozwa na kanuni ya tatizo linaloendelea vibaya nakubaliana na wakili wa Mjibu rufaa ingawa kwamba shauri halikuwa limepitwa na wakati kwa hiyo hoja ya kwanza inakosa sifa na ninaitupa,”alisema Jaji.
Kwanini kesi haikuthibitishwa
Jaji aliruka hoja ya pili na kwenda hoja ya tatu ya kama mjibu rufaa alikuwa ameweza kuthibitisha madai yake kwa mizania inayokubalika kisheria.
“Chini ya suala hili, Mrufani alikosoa uamuzi wa Mahakama katika maeneo manne. Moja, kelele inayodaiwa haikuzidi viwango vinavyoruhusiwa na mbili ni kuwa ugonjwa wa mjibu rufaa haukusababishwa na kelele kutoka kwenye jenereta”
Jaji akataja sababu ya tatu kuwa ni uhalali wa mnara uliojengwa na nne Mahakama ilitegemea ushahidi usiothibitishwa na wa kubahatisha.
“Katika kesi hii kesi ya papo hapo, hakimu aliona kuwa mjibu rufaa amethibitisha kuwa kelele hiyo ilitoka jenereta za Mrufani zilizidi viwango vinavyoruhusiwa na hivyo kumsababishia ugonjwa wa moyo na mishipa,”alisema Jaji.
“Hii ilitokana na kushindwa kwa mrufani kutoa kibali cha ujenzi na kwa ushuhuda wa mashahidi waliothibitisha kuwepo kwa kelele katika eneo hilo,” alisema.
Zaidi, hakimu alisema ripoti ya matibabu ambayo ilikuwa kielelezo P5, ilihusisha ugonjwa huo na kelele zinazotoka kwa jenereta zilizotajwa,” alieleza Jaji.
“Nimepitia kwa uangalifu ushahidi pamoja na vielelezo vilivyotolewa na ninaona kwamba, kwa hakika kwamba jenereta za mrufani ziliwekwa karibu na makazi ya Mjibu rufaa ambayo ilitoa kelele katika eneo jirani,”alisema.
“Hata hivyo hakuna ripoti kutoka kwa mamlaka ya usimamizi wa mazingira iliwasilishwa kortini ili kuthibitisha kwamba kelele iliyotolewa ilizidi viwango vilivyowekwa na sheria,”
Kanuni ya 7 ya usimamizi wa Mazingira (Viwango vya Ubora vya Udhibiti wa Kelele na Mtetemo Kanuni za Uchafuzi, G.N No. 336 ya 2011), inaagiza vinavyoruhusiwa ambavyo havipaswi kuzidi na viko katika Kanuni ndogo ya (1) na (2).
“Katika suala hilo, mzigo wa kuthibitisha ulikuwa ni wa mjibu rufaa kupitia ushahidi makini wa kisayansi au ushahidi wa kiufundi, kwamba kelele iliyotolewa kutoka kwa jenereta ilivuka mipaka inayoruhusiwa kisheria,”alisema Jaji.
“Mzigo huo haukupaswa kuhamishiwa kwa mrufani kwa sababu tu mrufani hakufanya hivyo kwa sababu tu hakuwasilisha nyaraka zutetezi kama ilivyoelezwa na kuhitimishwa kimakosa na hakimu aliyesikiliza kesi hii.”
“Mbali na kushindwa kuthibitisha kwamba kelele ilizidi viwango, mjibu rufaa pia alikuwa na wajibu wa kuthibitisha kwamba ugonjwa wake wa moyo wake na mishipa ulisababishwa na kelele na jenereta na sio sababu nyingine yoyote.”
Katika suala hili, Jaji alisema Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga iliyosikiliza kesi hiyo ilitegemea ripoti ya matibabu na ushuhuda wa shahidi namba PW3.
“Hata hivyo, baada ya kutathmini upya ushahidi huo, naona hilo hakuna sehemu yoyote katika ripoti ya matibabu ilipoelezwa matatizo ya moyo na mishipa ilisababishwa na yatokanayo na kelele, wala si ugonjwa unaohusishwa haswa na kelele inayodaiwa kuzalishwa na Jenereta za mrufani,”alisema Jaji.
“Ripoti ilipendekeza tu kwamba mjibu rufaa anahitaji mazingira tulivu kwa ustawi wake,”alisema Jaji Ndesamburo katika hukumu yake hiyo.
“Sioni kama ni sahihi kwa Hakimu kutegemea tu mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti ya matibabu na hivyo kuhitimisha kuwa ugonjwa wa mjibu rufaa ulisababishwa na kelele kutoka kwa jenereta za mrufani,”alisisitiza Jaji huyo.
“Ushahidi wa shahidi namba 3 ambaye si daktari wa moyo kama daktari ambaye alitayarisha ripoti hiyo, haukueleza vya kutosha chanzo cha ugonjwa wa mjibu rufaa.”
Jaji alisema katika ushahidi wake, shahidi huyo alisema kuwa ugonjwa wa moyo na mishipa unaweza kutokea kutoka mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kelele, uvutaji sigara, uzito kupita kiasi, msongo wa mawazo na matumizi ya pombe.
Julingana na Jaji, kielelezo namba P5 kilionesha kuwa mjibu rufaa hakuwa mvutaji sigara na hanywi pombe na kwamba shahidi huyo hakueleza kwa nini alihusisha ugonjwa huo na kelele kinyume na sababu nyingine zinazowezekana alizozitaja.
“Katika mazingira haya, ninaona mjibu rufaa alishindwa kuthibitisha kwa mizani ya kwamba ugonjwa wake wa moyo na mishipa ulisababishwa na kelele zinazodaiwa kuzalishwa kutoka kwa jenereta za mrufani ili kuhalalisha tuzo ya uharibifu,” alisema.