Prime
Bakwata Ilala yashinda kesi ya Msikiti wa Bangulo, Imam aamriwa kuondoka
Muktasari:
- Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi, imeamua kuwa eneo la Msikiti wa Bangulo uliopo Kituo cha Pugu, Wilaya ya Ilala, ni mali ya waqf iliyotolewa kwa Waislamu wa Bangulo chini ya usimamizi wa wadhamini waliosajiliwa wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Wilaya ya Ilala.
Arusha. Mahakama Kuu ya Dar es Salaam, Kitengo cha Ardhi, imetambua rasmi kuwa wadhamini waliosajiliwa wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Wilaya ya Ilala, ndiyo wamiliki na wasimamizi halali wa eneo la Msikiti wa Bangulo, lililopo Kituo cha Pugu, Dar es Salaam.
Hukumu hiyo imetolewa Mei 6, 2026, na Jaji Emmanuel Kawishe, akisisitiza kuwa Kassim Juma, aliyekuwa Imam na mwalimu wa madrasa katika msikiti huo, ni mvamizi wa eneo hilo. Baada ya kuisha kwa mkataba wake wa ajira mwaka 2021, Kassim aliendelea kuishi kwenye msikiti akidai umiliki wake binafsi, huku akizuia shughuli za ibada na usimamizi wa Bakwata.
Mahakama imesema Kassim alikaa eneo hilo kama mtumishi wa msikiti na si mmiliki, hivyo hana haki ya kudai umiliki wa ardhi hiyo iliyotolewa kwa waislamu wa Bangulo kupitia Waqf chini ya usimamizi wa Bakwata. Nakala ya hukumu hiyo imewekwa pia kwenye mtandao wa Mahakama.
Chanzo cha mgogoro
Kwa mujibu wa hati za Mahakama, kesi hiyo ilifunguliwa na wadhamini waliosajiliwa wa Bakwata Wilaya ya Ilala, wakimtuhumu Kassim kuvamia na kuhodhi eneo la msikiti bila uhalali.
Bakwata ilidai kuwa eneo hilo lilitolewa mwaka 2016 na Ramadhani Jalaka kupitia waqf kwa ajili ya kujengwa msikiti wa Waislamu wa Bangulo. Kassim Juma alikuwa ameajiriwa kama Imam, lakini ajira yake ilisimamishwa mwaka 2021. Baada ya hapo, alikataa kuondoka na kuanza kudai umiliki binafsi wa msikiti na ardhi husika.
Bakwata iliiomba Mahakama itambue kuwa Kassim ni mvamizi wa ardhi, iondoe madai yake na kuipa taasisi hiyo haki ya kuendelea kusimamia msikiti kwa niaba ya Waislamu wa Bangulo, pamoja na kulipa fidia na gharama za kesi.
Kassim alipinga madai hayo akidai kuwa yeye ndiye mmiliki halali wa eneo hilo kutokana na kuhusika katika kuanzisha na kujenga msikiti. Alidai alipata waqf kutoka kwa Ramadhani na kuomba mahakama itupilie mbali madai ya Bakwata.
Ushahidi Mahakamani
Bakwata ilileta mashahidi watano. Shahidi wa kwanza, Ramadhani Jalaka alisema alinunua ardhi hiyo ekari mbili mwaka 1991 na baada kugundua kuwa eneo hilo halikuwa na msikiti wa karibu, alitoa kipande cha ardhi 20x20 kwa Waislamu wa Bangulo kupitia Waqf rasmi na baadaye kuongeza kipande kingine cha hatua 10.
Amesisitiza kuwa hakumkabidhi Kassim umiliki binafsi, wala hakukuwa na makubaliano ya kumfanya mmiliki.
Shahidi wa pili na wa tatu, mke na mwanaye wa Ramadhani, walithibitisha kuwa ardhi hiyo ilikuwa mali ya familia yao kabla ya kutolewa kwa msikiti.
Shahidi wa nne, Juma Ibrahim alisema jukumu la Bakwata ni kusimamia mali za Waislamu, ikiwamo misikiti na mali zinazotolewa kupitia Waqf.
Mahakama ilipewa ushahidi kuwa Kassim alikataa kukabidhi ofisi yake baada ya ajira kumalizika, jambo lililosababisha mgogoro. Juhudi za usuluhishi kupitia viongozi wa dini na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala hazikuzaa matunda.
Uamuzi wa Mahakama
Mahakama ilibaini kuwa ardhi hiyo ilitolewa kwa Waislamu wa Bangulo kupitia waqf na kuwa Bakwata ndiyo msimamizi halali. Jaji Kawishe alisema:"Mlalamikiwa anayedai yeye ndiye mmiliki wa ardhi kwa sababu ya kuwa kiongozi au kushiriki ujenzi wa msikiti hana msingi na anapingana na ukweli kwamba ardhi hiyo ilitolewa kwa Waislamu wa Bangulo.”
Mahakama imemuamuru Kassim kuondoka mara moja katika eneo hilo na kuzuiwa kuingilia usimamizi wa Bakwata, pamoja na kulipa Sh5 milioni kama fidia kwa usumbufu uliosababishwa.