Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama Kuu yatengua uamuzi wa awali katika shauri la uchaguzi Tunduru Kusini

Picha na Mtandao.

Muktasari:

  • Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songea imebatilisha uamuzi wake wa awali uliotolewa Desemba 29, 2025 katika shauri la uchaguzi la Jimbo la Tunduru Kusini, baada ya kubaini kuwa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) hakikuwa na uhalali wa kutoa msaada wa kisheria wakati wa kuendesha kesi hiyo.

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songea imebatilisha uamuzi wake wa awali uliotolewa Desemba 29, 2025 katika shauri la uchaguzi namba 29982/2025 lililohusu matokeo ya uchaguzi wa ubunge wa Jimbo la Tunduru Kusini.

Awali, Desemba 29, 2025, Mahakama hiyo ilikuwa imetupilia mbali pingamizi lililowasilishwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Tunduru Kusini pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), baada ya kueleza kuwa walalamikaji waliokuwa wakipata msaada wa kisheria hawakulazimika kulipa dhamana ya gharama za kesi.

Kutokana na uamuzi huo, shauri la uchaguzi liliruhusiwa kuendelea kusikilizwa.

Hata hivyo, Mei 5, 2026, Jaji James Karayemaha alitoa uamuzi mpya kufuatia maombi ya mapitio namba 8876/2026 yaliyowasilishwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo pamoja na AG dhidi ya Mohamed Raisi, Odax John na Fadhili Chilombe.

Katika maombi hayo, waombaji waliiomba Mahakama kufanya mapitio ya uamuzi wake wa awali. Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahakama ilibaini kuwa walalamikaji katika shauri hilo hawakuwa na msaada halali wa kisheria kupitia Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), hivyo walishindwa kutimiza sharti la kisheria la kuweka dhamana ya gharama za kesi.

Katika uamuzi wake, Mahakama ilisema:

“Walalamikaji katika shauri namba 29982/2025 kati ya Mohamed Raisi na Odax John dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tunduru Kusini, Chilombe na AG hawakuwa na msaada wa kisheria na wameshindwa kulipa dhamana ya gharama.”

Kutokana na sababu hiyo, Mahakama ilikubali maombi ya mapitio na kutengua uamuzi pamoja na amri yake ya Desemba 29, 2025, huku ikiagiza kila upande kubeba gharama zake wenyewe.

Kwa mujibu wa hati ya maombi ya mapitio iliyowasilishwa Mahakamani, waombaji walidai kuwa baada ya hukumu ya awali kutolewa, walipata ushahidi mpya unaoonyesha TLS haikuwa na usajili halali wa kutoa msaada wa kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Msaada wa Kisheria wakati wa kuendesha shauri hilo la uchaguzi.

Serikali pia ilieleza kuwa hali hiyo ilisababisha walalamikaji kushindwa kutimiza matakwa ya kisheria ya kuweka dhamana ya gharama za kesi kama inavyotakiwa chini ya sheria za uchaguzi.

Maombi hayo yaliwasilishwa chini ya Amri ya XLII Kanuni ya 1(1)(b), 3 na 4(2)(b), pamoja na Kifungu cha 88(1) na Kifungu cha 105 vya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai.


Msingi wa maombi ya mapitio

Chanzo cha mgogoro huo ni matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 9, 2025 katika Jimbo la Tunduru Kusini ambapo mgombea wa CCM, Fadhili Chilombe, alitangazwa mshindi wa kiti cha ubunge na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Baada ya kutoridhishwa na matokeo hayo, Mohamed Raisi na Odax John walifungua shauri la uchaguzi kupinga ushindi huo.

Hata hivyo, kabla ya kesi kuanza kusikilizwa, upande wa Serikali uliwasilisha pingamizi la awali ukidai kuwa walalamikaji hawakuwa wamewasilisha dhamana ya gharama za kesi ndani ya muda wa siku 14 kama sheria inavyotaka.

Desemba 2025, Mahakama ilitupilia mbali pingamizi hilo kwa maelezo kuwa walalamikaji walikuwa wakipata msaada wa kisheria kupitia Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), hivyo hawakulazimika kuweka dhamana hiyo.

Lakini katika maombi ya sasa ya mapitio, Serikali iliiambia Mahakama kuwa ilipata taarifa mpya kutoka Wizara ya Katiba na Sheria zikionyesha kuwa leseni ya TLS ya kutoa msaada wa kisheria ilikuwa imekwisha muda wake tangu Aprili 28, 2022.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizowasilishwa Mahakamani, TLS ilikuwa imepewa cheti cha usajili namba LAP 2019 0003 mwaka 2019 kwa muda wa miaka mitatu. Serikali ilidai kuwa baada ya muda huo kuisha, TLS haikuhuisha leseni yake hadi Desemba 22, 2025.

Wakili wa Serikali Mkuu, Marc Mulwambo pamoja na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Stanley Kalokola, waliieleza Mahakama kuwa ushahidi huo mpya ulipatikana baada ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuandika barua kwa Wizara ya Katiba na Sheria kuomba ufafanuzi kuhusu uhalali wa TLS kutoa msaada wa kisheria.

Katika majibu yake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria alieleza kuwa TLS ilikuwa na usajili wa muda uliokwisha Aprili 2022 na kwamba maombi ya kuhuisha leseni yaliwasilishwa Desemba 2025.

Waliojibu maombi hayo, Mohamed Raisi na Odax John waliwakilishwa na Wakili John Seka, huku Fadhili Chilombe akiwakilishwa na Wakili Gilbert Sawe.

Wakili Seka alipinga maombi hayo akidai kuwa yalikuwa ni rufaa ya kificho na kwamba Mahakama haikuwa na mamlaka ya kusikiliza na kuamua suala hilo upya.

Aidha, Wakili Seka alidai kuwa Mahakama tayari ilikuwa imeshatoa uamuzi kuhusu hadhi ya TLS, hivyo mapitio hayo yangekuwa sawa na Mahakama kujigeuza kuwa mahakama ya juu dhidi ya uamuzi wake yenyewe.

Pia alieleza kuwa ushahidi uliowasilishwa na Serikali ulikuwa na mashaka kwa sababu cheti halisi cha usajili wa TLS hakikuwasilishwa Mahakamani, akisisitiza kuwa barua kutoka Wizara ya Katiba na Sheria pekee haiwezi kuthibitisha kuwa TLS haikuwa na leseni halali ya kutoa msaada wa kisheria.

Vilevile, alihoji uhalali wa nyaraka zilizoonyesha kuwa TLS iliomba kuhuisha leseni yake Desemba 2025, akisema hazikuwa na uthibitisho wa moja kwa moja kutoka TLS yenyewe.


Uamuzi wa Mahakama

Katika uamuzi wake, Mahakama ilieleza kuwa mapitio ni utaratibu tofauti kabisa na rufaa.

Jaji James Karayemaha alisema hoja zilizotolewa na pande zote zimeibua masuala matatu makuu ya kuamuliwa na Mahakama.

Mojawapo ni iwapo waombaji walithibitisha kupata ushahidi mpya kama inavyotakiwa kisheria.

Masuala mengine yalikuwa ni iwapo ushahidi huo ulikuwa na uzito na ulikuwepo wakati uamuzi unaoombwa kufanyiwa mapitio ulipotolewa, pamoja na iwapo waombaji walitumia uangalifu unaostahili kuupata ushahidi huo kabla ya hukumu kutolewa.

Jaji Karayemaha alisema sheria inaruhusu Mahakama kufanya mapitio pale ambapo ushahidi mpya wenye uzito mkubwa unapatikana baada ya hukumu kutolewa.

Mahakama ilisema ushahidi uliotolewa na Wizara ya Katiba na Sheria ulikuwa wa kuaminika kwa sababu ulitoka katika mamlaka yenye jukumu la kusimamia usajili wa watoa huduma za msaada wa kisheria nchini.

Katika uamuzi wake, Jaji Karayemaha alisema Msajili wa Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria ndiye mwenye dhamana ya kuhifadhi kumbukumbu zote za taasisi zinazotoa huduma hiyo, hivyo taarifa zilizotolewa na Wizara haziwezi kubezwa.

Mahakama pia ilikubaliana na hoja ya Serikali kuwa vyeti vya watoa msaada wa kisheria vina muda wa miaka mitatu na vinapaswa kuhuishwa kwa mujibu wa Kanuni za Msaada wa Kisheria.

Kwa mujibu wa Mahakama, hakuna ushahidi uliowasilishwa kuonyesha kuwa TLS ilikuwa imehuisha leseni yake kabla ya Desemba 2025.

Jaji Karayemaha alisema kama ushahidi huo ungepatikana mapema kabla ya hukumu ya Desemba 2025, basi uamuzi wa Mahakama ungekuwa tofauti.

Mahakama pia ilibaini kuwa Serikali ilichukua hatua muhimu za kutafuta taarifa hizo mapema kwa kuandika barua kwa Wizara ya Katiba na Sheria hata kabla ya hukumu ya awali kutolewa.

Kutokana na mazingira hayo, Mahakama iliamua kuwa waombaji walitimiza masharti yote ya kisheria yanayoruhusu mapitio ya hukumu, hivyo ikakubali maombi hayo na kutengua uamuzi pamoja na amri yake ya Desemba 29, 2025.

Mahakama ilitangaza kuwa walalamikaji katika shauri hilo hawakuwa na msaada halali wa kisheria kupitia TLS na kwamba walishindwa kutimiza sharti la kuweka dhamana ya gharama za kesi, huku kila upande ukiamriwa kubeba gharama zake wenyewe.

Katika hitimisho lake, Jaji Karayemaha alisema: “Walalamikaji katika shauri namba 29982/2025 kati ya Mohamed Raisi na Odax John dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tunduru Kusini, Chilombe na AG hawakuwa na msaada wa kisheria na wameshindwa kulipa dhamana ya gharama.”