Tume: Toeni mapendekezo kuboresha sheria nchini

Muktasari:
- Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Katibu Mtendaji wa tume hiyo, Griffin Mwakapeje alipokutana na Jumuiya ya Asasi za kiraia zinazoratibiwa na Taasisi ya mafunzo ya MS TCDC walipotembelea ofisini kwake jijini Dodoma.
Dodoma. Tume ya Kurekebisha Sheria nchini, yawataka wadau wa sheria, kuwasilisha mapendekezo yao ya maboresho mbalimbali ya sheria nchini ili kuyatafiti kabla ya kuishauri Serikali.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Katibu Mtendaji wa tume hiyo, Griffin Mwakapeje alipokutana na Jumuiya ya Asasi za kiraia zinazoratibiwa na Taasisi ya mafunzo ya MS TCDC walipotembelea ofisini kwake jijini Dodoma.
Ugeni huo ambao ulikuwa kwa ajili ya kuwasilisha maoni na mapendekezo kwenye sheria mbalimbali ambazo kwazo waliona zina changamoto mbalimbali.
“Tume ndiyo chombo pekee cha kisheria ambacho kimewekwa na Bunge kwa ajili ya kuisaidia serikali kufanya mapitio na kuangalia changamoto mbalimbali za kisheria na kuzifanyia utafiti.
Utafiti ambao sisi tunaufanya, tunahusisha jamii ili mwisho wa siku sheria inapokuja kutungwa wote tunakuwa kwenye uelewa mmoja,” amefafanua Mwakapeje.
Ameongeza kuwa sheria zikifanyiwa utafiti zinaweza kuishi miaka mingi zaidi badala ya kubadilishwa mara kwa mara.

Akizungumzia kuhusu kikao hicho Mwakapeje amesema jumuiya hiyo ilifanya utafiti kwenye maeneo mbalimbali ambayo ni pamoja na sheria za jinai na masuala ya uraia, masuala ya kikatiba, sheria za kimataifa na sheria za vyombo vya habari na upatikanaji wa taarifa.
“Baada ya utafiti wao waliona ni sahihi kuja kutushirikisha tafiti zao walizofanya kwa kujua kuwa Tume ya Kurekebisha Sheria ndiyo chombo pekee ambacho kinafanya utafiti na mapitio ya sheria zote. Hivyo wakaona waje watushirikishe mapendekezo yao ili na sisi tuweze kufanya utafiti na kuishauri serikali,” alisema Mwakapeje.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji (mstaafu) January Msoffe ameipongeza jumuiya hiyo na kuwaahidi ushirikiano zaidi, huku akitoa wito kwa wadau wengine kuweza kutoa mapendekezo yao ya maboresho ya sheria mbalimbali na hivyo kuifanya nchi iwe na sheria bora zaidi.
Kiongozi wa msafara wa jumuiya hiyo ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili (TLS), Wakili Harold Sungusia ameipongeza tume kwa kazi wanazofanya za utafiti wa sheria mbalimbali na kuahidi kuendelea kushirikiana zaidi kwa kutoa mapendekezo katika maeneo mbalimbali hasa katika mchakato wa Katiba unaoendelea.