Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TRA yapata mwarobaini wa msongamano magari Holili

Baadhi ya magari ya mizigo yakiwa katika kituo cha mpaka wa Holili.

Muktasari:

  • Baadhi ya wafanyabiashara wanaotumia Mpaka wa Holili wamesema uwekaji wa mashine hiyo utaongeza ufanisi wa kazi.

Moshi. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro, inakusudia kuweka mashine maalumu ya ukaguzi wa mizigo katika magari mpaka wa Holili.

Mpaka huo ambao huchangia asilimia 55 ya makusanyo ya TRA Mkoa wa Kilimanjaro, umekuwa na msongano wa magari ya mizigo yanayoingia nchini yakitokea nchi jirani ya Kenya.

Jana, Jumamosi Aprili 27, 2025 Mwananchi ilifika katika mpaka huo na kushuhudia msongamano wa magari ya mizigo yaliyokuwa yakisubiri kukaguliwa.

Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, James Jilala amesema wapo katika mchakato wa kuweka mashine katika mpaka huo ili kurahisisha utendaji kazi na kupunguza msongamano ambao hujitokeza kwa sasa.

"Kwa sasa tuna mpango wa kuweka scanner katika kituo hiki cha Holili, mpango huu ukikamilika mambo yatakuwa mazuri na msongamano wa magari kama unavyoona utapungua kwa kiasi kikubwa sana, kwani hakutakuwa na utaratibu wa kushusha mizigo, tutashusha tu pale itakapobidi,” amesema Jilala.

"Mpango huo uko kwenye mchakato kwa sasa, tayari wataalamu wameshakuja kuangalia ni wapi wataweka hiyo scanner na ukikamilika gari zitakuwa zinapita na kukaguliwa bila kushusha mizigo.  Mpango huu utaongeza ufanisi na tutaondokana na msongamano huu wa malori.”

Akizungumzia makusanyo katika kipindi cha miezi tisa iliyopita, Jilala amesema katika Mkoa wa Kilimanjaro, waliwekewa lengo la kukusanya Sh217 bilioni na walikusanya Sh245 bilioni sawa na ufanisi wa asilimia 113.

"Julai mpaka Machi, tumefanikiwa kuyafikia malengo ambayo tulipangiwa, kwa kodi za ndani lengo lilikuwa ni Sh76 bilioni lakini tulikusanya Sh79 bilioni, ushuru wa forodha lengo likuwa ni Sh141 bilioni na tulifanikiwa kukusanya Sh166 bilioni. Niwapongeze walipa kodi wote kwa sababu kodi ni afya ya Serikali,” amesema.

Baadhi ya wafanyabiashara wanaotumia Mpaka wa Holili wakizungumza na Mwananchi wamesema uwekaji wa mashine hiyo utaongeza ufanisi wa kazi.

Mfanyabiashara Joyce Mosha amesema utaratibu wa sasa wa kushusha mizigo hutumia muda mrefu hali ambayo husababisha msongamano wa malori hasa kipindi ambacho kuna bidhaa nyingi zinazoingia nchini na kutoka kupitia mpaka huo.

"Wakiweka mashine hiyo itapunguza muda wa kukaa katika kituo hiki cha Mpaka wa Holili, kwa sababu gari likija sasa na mzigo litaskaniwa na mzigo kukaguliwa na kuondoka bila kulazimisha kushushwa mzigo, hivyo itarahisisha kazi,” amesema Mosha.

Mtumiaji mwingine wa mpaka huo, Abdalah Hassan ameiomba Serikali kuharakisha ufungaji wa mashine hiyo ili kuwapunguzia muda wa kusubiri mizigo yao kukaguliwa.

"Endapo Serikali ikifanikisha hili la scanner, kwa kweli itakuwa jambo la muhimu sana kwetu wafanyabiashara tunaotumia mpaka huu, kwa sababu itatupunguzia kusubiri kwa muda mrefu na kuturahisishia mambo yetu,"amesema mfanyabiashara huyo.