TRA yakusanya Sh5.92 trilioni mpaka Septemba

Muktasari:
- Makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 14.6 ya mwaka uliopita katika kipindi kama hicho
Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya Sh5.92 trilioni katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023 ulioanza Julai mwaka huu.
Makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 14.6 ikilinganishwa na makusanyo ya kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha uliopita iliyokuwa Sh5.17 trilioni.
Kiasi cha fedha kilichokusanywa ni sawa na asilimia 99.1 ya lengo la kukusanya Sh5.97 trilioni walilokuwa wamejiwekea.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa TRA na Kamishna Mkuu, Alphayo Kidata inaeleza ufanisi huo ni matokeo ya kuendelea kuimarika kwa matumizi ya mfumo wa kielektroniki katika usimamizi wa kodi.
“Kuboreshwa kwa mazingira ya ufanyaji wa biashara nchini, kuimarika kwa ulipaji kodi kwa hiari, utatuzi wa migogoro ya kikodi nje ya mahakama pamoja na kushughulikia malalamiko ya walipakodi kwa wakati na utoaji wa elimu kwa walipakodi,” alisema Kidata.
Pia kuimarika kwa uzalishaji viwandani vya ndani na biashara za kimataifa ni miongoni mwa vitu vilivyochangia mafanikio hayo.
Ili kuendelea kufikia mafanikio zaidi, TRA imewataka wafanyabiashara wanaotakiwa kutumia mashine za kielektroniki (EFD) kununua na kutumia kwa ukamilifu. “Kundi hili linajumuisha wafanyabiashara wote wenye wastani wa mauzo ghafi kwa mwaka yanayofikia au kuzidi Sh11 milioni,”
Wauzaji wote wa bidhaa na watoa huduma wahakikishe wanatoa risiti za kielektroniki zilizo sahihi katika mauzo wanayofanya huku wanunuzi wakitakiwa kudai risiti zao.
“Walipakodi pia wawasilishe ritani sahihi na kulipa kodi stahiki na wakati, wazalishaji na waagizaji bidhaa zinazotakiwa kubandikwa stempu za kodi kuzingatia matumizi sahihi ya stempu katika bidhaa hizo,” alisema Kidata.
Kwa mujibu wa taarifa ya TRA, Septemba ndiyo mwezi ulioongoza kwa makusanyo makubwa hadi kufanikiwa kuvuka lengo kwa asilimia 105.5.
Katika mwezi huo, lengo lilikuwa kukusanya Sh2.15 trilioni, lakini hadi unakamilika Sh2.27 trilioni zilikusanywa.
Julai makusanyo yake yalionekana kuwa chini, kwani lengo la ukusanyaji mapato lilifikiwa kwa asilimia 93.1 ikilinganishwa na asilimia 97.8 ya Agosti.
Jumla ya Sh1.76 trilioni zilikusanywa Julai mwaka huu huku Agosti TRA ikikusanya Sh1.88 trilioni.