TPSF yaunga mkono ukodishwaji bandari

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula
Muktasari:
- Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Angelina Ngalula amesema urasimu uzembe na kukosekana kwa ufanisi katika uendeshaji wa bandari, umekuwa ni mradi unaowapatia watu mabilioni ya fedha.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Angelina Ngalula amesema urasimu uzembe na kukosekana kwa ufanisi katika uendeshaji wa bandari, umekuwa ni mradi unaowapatia watu mabilioni ya fedha.
Hivyo basi TPSF inaipongeza Serikali kwa hatua ngumu iliyochukua ya kukaribisha sekta binafsi katika uendeshaji wa bandari hiyo, jambo ambalo wanadhani litaongeza ufanisi, na hivyo kuharakisha ukuaji uchumi kupitia raslimali hiyo.
“Bandari zinazotuzunguka zinafaidika kwa kiasi kikubwa kutokana na uzembe na kukosekana kwa ufanisi kwenye bandari yetu. Urasimu huu, umechochea rushwa na hivyo kuongeza gharama, hivyo sisi tuko na wewe katika hili,” amesema.
Hayo amebainisha jijini hapa leo Juni 9, 2023 kwenye ufunguzi wa Mkutano wa 14, wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), ambapo mgeni rasmi wa mkutano huo alikuwa Mwenyekiti wa Baraza hilo Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika hotuba yake hiyo Ngalula amesema miaka 15 iliyopita, wadau waliokuwapo kwenye sekta hiyo bandari za Beira, walikuwa wanaziita za majahazi lakini kwa sasa zimekuwa bandari shindani na zote hizo zimetumia fursa ya ufanisi mdogo wa bandari za Tanzania.
“Bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikidumaa kwa miaka mingi, huku ikitegemewa na nchi ambazo zinatuzunguka takribani nane, lakini tumeshindwa kuvuka hata tani 6 milioni kuzihudumia katika kuzihudumia pamoja na fursa kubwa inayokadiriwa kuwa tani 30 milioni zilizopo na tungeweza kuzipata,” amesema.