Toto Afya kadi ilitishia uhai wa NHIF

Muktasari:
- Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewasilisha bajeti yake ya mwaka 2023/24 na kufafanua juu ya kusitishwa kwa usajili wa mtoto mmoja mmoja kwenye huduma ya Toto Afya Kadi.
Dar es Salaam. Serikali imesema tathmini iliyofanywa kwa huduma ya Toto Afya Kadi inayotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ilionyesha wazi kuwa kundi hilo lina matumizi makubwa na hivyo kutishia uhai na uendelevu wa mfuko huo endapo hatua hazitachukuliwa.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameyasema hayo leo Ijumaa Mei 12, 2023 wakati akiwasilisha mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2023/24.
Amesema kwa lengo la kuimarisha uhai na uendelevu wa mfuko, Serikali kupitia NHIF imefanya tathmini ya wanufaika wa huduma zitolewazo kwa kundi la watoto walio chini ya miaka 18, ambao hupata huduma kupitia mpango ujulikanao kama Toto Afya Kadi.
Amesema mpango huu ulianzishwa mwaka 2016 ukiwa na lengo la kusajili angalau asilimia 10 ya watoto milioni 25 waliokuwepo kwa kuzingatia sensa ya watu ya mwaka 2012.
Ummy amesema hadi kufikia mwaka 2020/21, Mfuko ulikuwa umesajili watoto 205,796 ambao michango yao ilikuwa ni Sh5.99 bilioni na matumizi yao ni Sh40.58 bilioni sawa na uwiano wa asilimia 677.
Amesema kulingana na tathmini hiyo, kundi hili limekuwa likipata huduma zaidi katika vituo vinavyomilikiwa na sekta binafsi ikilinganishwa na umma na kupelekea mfuko kulipa asilimia 58 ya fedha zote.
Ummy amesema asilimia 22 ililipwa kwa mashirika ya dini na asilimia 20 kwa vituo vya Serikali kwa magonjwa kama malaria, kikohozi na homa, ambayo yangeweza kutibiwa katika vituo vya ngazi ya chini.
“Kutokana na tathmini hii, ni wazi kuwa kundi hili lina matumizi makubwa na hivyo kutishia uhai na uendelevu wa mfuko endapo hatua hazitachukuliwa,”amesema.
Hata hivyo, amesema Februari 2023, utaratibu wa kuandikisha kundi hilo kwa mtoto mmoja mmoja umesitishwa na msisitizo kuwekwa katika usajili kupitia vifurushi ambavyo vina utaratibu wa kusajili katika ngazi ya familia.
Amevitaja vifurushi hivi vijulikanavyo kama Najali Afya, Wekeza Afya na Timiza Afya vinatoa fursa kwa familia kusajiliwa kulingana na ukubwa wake pamoja na kipato.
“Watoto hawa wanaweza kusajiliwa kupitia shule wanazosoma, lengo ikiwa ni kusajili watoto wengi kwa umoja wao kulingana na misingi na dhana ya bima,”amesema.
Ametoa rai kwa wananchi wote kutumia fursa hii kwa kuandikisha familia zao mapema na wasisubiri kuugua na ndipo wajiunge, jambo ambalo ni kinyume na dhana ya bima.