Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TMA yatoa tahadhari mvua ya siku tano mfululizo

Muktasari:

  • Mvua zilizonyesha awali zimeathiri miundombinu katika maeneo mbalimbali nchini

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetahadharisha mvua kubwa kuendelea kunyesha katika siku tano zijazo huku ikiwashauri wananchi kwenye mikoa ya Morogoro, Lindi, Mtwara, Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe na Ruvuma kujiandaa.

Mamlaka hiyo imesema kuna matarajio ya hali mbaya ya hewa kuanzia leo Januari 31, 2024 katika maeneo machache ya mikoa hiyo.

Huo ni mwendelezo wa tahadhari ambazo TMA imekuwa ikizitoa tangu kuanza kwa mvua za msimu wa vuli zilizotarajiwa kuisha Desemba lakini zinaendelea hadi sasa kwenye maeneo mengi nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA leo Jumatano Januari 31, 2024, athari zinazoweza kujitokeza ni baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, pamoja na kuathirika kwa a shughuli za kiuchumi.

TMA imewataka watu kujiandaa na kuchukua tahadhari kwa siku tatu kuanzia leo Januari 31, hadi Februari 2, 2024 huku Jumamosi ya Februari 3 na Jumapili Februari 4 kukiwa hakuna tahadhari yoyote.

Jana, Januari 30, 2024, Meneja wa Utabiri wa TMA, Dk Mafuru Kantamla ameiambia Mwananchi kuwa, mvua zinazoendelea hivi sasa ni za nje ya msimu wa vuli zinazochangia pia uwepo wa viashiria vya El Nino ambayo inaonyesha ipo hadi Aprili.

Mvua hizo zimeathiri miundombinu na kilimo katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na kusababisha vifo, mafuriko na baadhi ya shughuli kusimama.

Jana, mjini Morogoro, Askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji walilazimika kuwavusha kwa kamba wananchi wanaotumia Barabara ya Mazimbu iliyopo kata za Kihonda na Lukobe baada ya barabara hiyo kujaa maji eneo la Kwa Bwanajela

Mkoani Njombe, mashamba na mazao yamekuwa yakisombwa na maji, huku mazao ya nyanya na maharagwe yakitajwa kuoza kutokana na kukithiri kwa maji ya mvua zinazoendelea kunyesha.

Ofisa Ugani wa  Lupembe, mkoani Njombe, Ibrahim Mhessi amesema katika eneo hilo mvua ni nyingi na wamewashauri wakulima kupanda mihogo, parachichi na mboga mboga kipindi hiki kwa kuwa kuna uwezekano wa kutokuwa na mavuno mazuri ya mahindi.