Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TCU yatoa siku tano waliokosa nafasi elimu ya juu

Muktasari:

  • Waombaji 130,116 wadahiliwa kujiunga taasisi za elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2023/2024, dirisha la mwisho lafunguliwa kuwapa fursa waliokosa na waliochelewa kuomba.

Dar es Salaam. Jumla ya waombaji 130,116 katika ngazi ya shahada ya kwanza wamedahiliwa katika vyuo vikuu kwa madirisha matatu yaliyofunguliwa ya mwaka wa masomo 2023/2024.

 Hata hivyo Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imelazimika kufungua dirisha la nne kufuatia kuwepo kwa waombaji ambao hawakufanikiwa kupata udahili katika awamu zote tatu.

Dirisha hili litakalodumu kwa siku tano limefunguliwa kuanzia leo Oktoba 13 hadi Oktoba 17 likiwa ni nafasi ya mwisho kwa wanafunzi wote wenye matumaini ya kujiunga na vyuo vikuu mwaka huu.

Kufunguliwa kwa dirisha hilo kumeenda sambamba na maelekezo kwa wanafunzi waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja kujithibitisha katika chuo kimojawapo ili kuacha wazi nafasi katika vyuo vingine kwa ajili ya waombaji wengine.

Akizungumza leo Oktoba 13, 2023 Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amesema wamelazimika kufungua dirisha hilo baada ya kupokea maombi kutoka kwa waombaji na vyuo vikuu ambavyo bado vina nafasi.

Amesema kwa mwaka huu wa masomo vyuo vikuu vina jumla ya nafasi 187,000 na hadi sasa waliodahiliwa ni 130,116 hivyo bado kuna nafasi ambazo ziko wazi.

Mbali na hilo amesema TCU pia imepokea ombi la kuongeza kutoka Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso) kutokana na kuwepo kwa waombaji ambao hawakufanikiwa kupata udahili katika madirisha yote matatu.

Kwa mujibu wa katibu mtendaji huyo katika awamu zote tatu yalipokelewa maombi 142,440 na waliopata udahili 130,116 hivyo kuna waombaji 12,324 hawajapata udahili.

“Hapa tunasisitiza ndani ya siku hizi tano wale ambao hawakuweza kutuma maombi au hawakufanikiwa katika awamu zilizopita watumie fursa hii kwa usahihi.

“Nitoe wito pia kwa taasisi zote za elimu ya juu zinazofanya udahili wa shahada ya kwanza kuendelea kutangaza programu ambazo bado zina nafasi,” amesema Profesa Kihampa.

Akizungumzia ongezeko la muda wa udahili rais wa Tahliso, Maria John amewataka waombaji ambao hawana uelewa wa kujaza maombi wawatumie watu sahihi na si vinginevyo.

“Niwaombe wawe makini katika uombaji wawatumie watu sahihi wa kuwaombea kuepuka changamoto. Wapo ambao wanaenda wanawatumia watu wa steshenari bila kujua kama wana uelewa wa kufanya maombi au lah.

“Hali hii imekuwa ikisababisha kufanyika kwa makosa na ndiyo maana unakuta mtu anaomba awamu zote anakosa, kama huelewi usione haya kuuliza kwa wanaoelewa tuwe makini kuitumia fursa hii ambayo inaenda kutusaidia kutimiza ndoto zetu,” amesema Maria.

Katibu Mtendaji pia alitumia fursa hiyo kuuleza umma kuhusu Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K Nyerere cha Kilimo na Teknolojia kilichopo Butiama ambayo ni taasisi mpya ya elimu ya juu inayoanza kudahili mwaka huu ikiwa na programu tatu.

Profesa Kihampa pia amewatahadharisha waombaji kuhakikisha maombi yao wanatuma kwenye vyuo husika na inapotokea changamoto wasisite kufanya mawasiliano na vyuo hivyo.

“Tunasisitiza epukeni kupotoshwa na watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hala nchini,” amesema.