Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TCRA kutoa elimu ya uchumi wa kidijitali kuanzia shule za msingi

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),  Dk Jabir Bakari akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya wadau wa mtandao ikiwa ni kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya usalama mtandaoni inayoadhimishwa Jumanne ya pili ya Februari. Picha na Elizabeth Edward

Muktasari:

  • TCRA yadhamiria kutengeneza kizazi kinachofahamu matumizi sahihi ya mitandao na kitakachochangamkia fursa za uchumi wa kidijitali, yasisitiza wadau kuona umuhimu wa kuelimisha jamii matumizi chanya ya mtandao

Dar es Salaam. Ili kuondokana na utegemezi wa mifumo ya Tehama na matumizi mabaya ya mitandao, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imekuja na mpango wa kuwafundisha watoto kuanzia ngazi za shule za msingi umuhimu wa uchumi wa kidijitali.

TCRA imebainisha kuwa itaanzisha klabu za Tehama kwa shule za msingi na sekondari ili kutengeneza kizazi chenye uelewa wa kutosha kuhusu mitandao na kikiandaliwa  kuzitumia fursa zinazopatikana mitandaoni.

Hayo yameelezwa leo Februari 2, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa TCRA, Dk Jabir Bakari wakati akifungua semina ya wadau wa masuala ya mtandao wa intaneti, ikiwa ni  kuelekea maadhimisho ya siku ya usalama mtandaoni inayoadhimishwa duniani kote Jumanne ya pili ya Februari.

Amesema licha ya intaneti na mitandao ya kijamii kuwa na fursa nyingi, bado kuna watu wanaoitumia vibaya hivyo ipo haja ya kuanza kutengeneza kizazi kitakachotambua matumizi sahihi na kushiriki kikamilifu kwenye uchumi wa kidijitali.

Dk Bakari amebainisha kuwa kwa ukubwa  na umuhimu wa Tehama sasa imefikia hatua kama nchi ioteshe mizizi ya kuandaa kizazi ambacho hakitaishia kuwa watumiaji, bali wajenzi wa mifumo ya kidijitali ili kujiondoa kwenye utegemezi.

“Nia yetu ni kuwa na kizazi chenye uelewa mzuri na kinaandaliwa kunufaika na uchumi wa kidijitali. Tunataka kukuza jamii kikamilifu kwenye uchumi wa kidijitali kuwa sehemu ya wajenzi wa mifumo ya Tehama na mitandao ya intaneti ambayo tutanufaika nayo badala ya kubaki kuwa watumiaji,” amesema Dk Bakari.

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa ni  muhimu elimu kuhusu usalama wa mtandao kutolewa kwa kila nyanja, ili kudhibiti wahalifu hao na pengine kuwajumuisha kwenye kundi la kutoa elimu ya usalama wa mtandao.

"Kupitia mitandao unaweza kuongeza kipato na pengine kuwa na ubunifu ama ajira jambo linaloweza kubadilisha maisha. Dereva wa bodaboda anayetumia Tehama anafikiwa na fursa nyingi kuliko asiyekuwa na nafasi hiyo,” amesema.

Mmoja wa washiriki katika semina hiyo, Dk Macca Abdalla amesema wanawake wanahitaji kupata elimu zaidi ya mtandao ili waweze kujikwamua kiuchumi.

 “Tunataka huduma za mawasiliano zilete tija kwenye shughuli za kiuchumi, kijamii na  watu wabadilike kutoka hatua moja kwenda nyingine ili kuchagiza ukuaji wa uchumi,” amesema Dk Macca.