TCRA: Bei ya data Tanzania iko chini

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabir Bakari
Muktasari:
- Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema tafiti zilizofanyika zimebaini kuwa gharama za data nchini ambayo ni Sh1, 666 kwa GB, kwamba ni moja ya zilizo chini ukilinganisha na nchi nyingine Afrika.
Dodoma. Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema tafiti zilizofanyika zimebaini kuwa gharama za data nchini ambayo ni Sh1, 666 kwa GB kwamba ni moja ya zilizo chini ukilinganisha na nchi nyingine Afrika.
Hayo yamesemwa Jumanne, Julai 18,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabir Bakari wakati wa mkutano waandishi wa habari wa utekelezaji wa majukumu na mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu kwa mwaka 2023/24.
Amesema kwa mujibu wa tafiti mbalimbali hadi kufikia Juni mwaka 2023, Tanzania imeendelea kuwa nchi yenye kiwango kidogo sana cha bei ya data kwa GB1 ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Amesema kwa kiwango hicho hicho, Tanzania inashika nafasi ya kwanza (1) kwa bei ndogo ya data kwa GB 1 ukilinganisha na nchi zote zilizopo Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
“Tanzania pia inashika nafasi ya saba kwa kuwa na bei ndogo ya data kwa Afrika hii ni kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa katika tovuti ya Statista,” amesema.
Amesema takwimu zinaonyesha kuwa barani Afrika, wastani wa gharama ya GB moja ni Dola za Marekani 3.51 hii ni sawa na Sh8, 157.
Miamala yaongezeka
Dk Bakari amesema idadi ya miamala imeongezeka kutoka Sh3.76 bilioni kwa kipindi kilichoishia Juni mwaka 2022 hadi kufikia Sh4.67 bilioni Juni mwaka 2023 sawa na asilimia 24.
Aidha, amesema akaunti za pesa kwa simu pia zimeongezeka kwa asilimia 24 kuanzia Julai mwaka 2022 hadi Juni mwaka 2023.
Gharama za simu zapungua
Dk Bakari amesema gharama za muunganisho wa simu kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine, zimekuwa zikipungua mwaka hadi mwaka.
Amesema mwaka 2015 gharama zilikua ni Sh30.58 na kwa sasa gharama zilizokokotolewa ni Sh1.86 kwa dakika.
“Hii inachangia kupunguza gharama za rejareja za upigaji wa simu na kuondoa ulazima wa wateja kuwa na simu zaidi ya moja,” amesema.
Aidha, Dk Bakari amesema gharama za kupata kibali cha kupitisha miundombinu kwenye barabara zimepungua.
Amesema awali watoa huduma walitakiwa kulipa ada ya malipo ya kujenga ya Dola za Kimarekani 1,000 kwa Kilomita 1 na kila mwaka kulipia Dola za Kimarekani 1,000 kwa Kilomita moja.
Amesema gharama hizi zilikuwa zinachangia gharama za uendeshaji kuwa kubwa na kwamba kuanzia julai, mwaka 2023 gharama zimepungua.
Amesema kwa kulipa ada ya malipo ya kujenga imekuwa Dola za Kimarekani 200 na malipo ya kila mwaka ni Dola za Kimarekani 100.
Dk Bakari amesema idadi ya dakika za simu za kimataifa zinazoingia nchini zimepungua kutoka dakika milioni 3.13 Julai mwaka 2022 hadi kufikia milioni 2.9 Juni mwaka 2023 ambayo ni sawa na asilimia 7.54.
Pia amesema idadi ya dakika za simu za kimataifa zinazotoka nchini pia zimepungua kutoka dakika milioni 2.40 Julai 2022 hadi kufikia dakika milioni 2.22 Juni 2023 ambayo ni sawa na asilimia 7.46.
“Kupungua kwa simu za kimataifa kunasababishwa na mabadiliko ya teknolojia na upatikanaji wa chaguzi mbadala za kupiga simu kupitia mitandao ya intaneti kama vile whatsap, facebook, telegram, zoom na kadhalika,”amesema.
Pia amesema idadi ya dakika za simu za kitaifa ndani ya mtandao mmoja zimeongezeka kutoka dakika milioni 6.17 Julai 2022 hadi dakika milioni 7.01 Juni 2023 ambayo ni sawa na 13.61.
“Idadi ya dakika za simu za kitaifa nje ya mtandao mmoja zimeongezeka kutoka dakika milioni 4.87 Julai mwaka 2022 hadi kufikia dakika milioni 5.06 kufikia Juni 2023 ambayo ni sawa na 3.81,”amesema.
Amesema ongezeko la simu za kitaifa linasababishwa na ukuaji wa sekta ya mawasiliano nchini.
Uhalifu mtandaoni
Dk Bakari amesema Juni mwaka 2023, TCRA ilifanya uchambuzi wa anwani za kompyuta zenye viashiria vya kushambuliwa na kutoa mashauri ya usalama mtandaoni kwa taasisi za umma na binafsi.
Amesema mashauri 812 yalichambuliwa ukilinganishwa na mashauri 920 kwa kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2021/22 ili hatua stahiki ziweze kuchukulia kuimarisha usalama wa mifumo yao.
Amesema kutokana na hatua zilizochukuliwa na Serikali, idadi ya simu za udanganyifu imeendelea kupungua kuanzia mwaka 2020 hadi Juni mwaka 2023.
Laini za matapeli zimesajiliwa
Dk Bakari amesema matapeli wanapokamatwa matapeli wa njia ya simu wanabainika kuwa laini zao zimesajiliwa kwa jina la mtu mwingine.
“Sio kwamba katika mitambo yetu hatuzifahamu simu zile na ndio maana tulitangaza wateja wahakiki ili kubaini kuwa simu inayotumika ni ya kwako, ili tufahamu zile ao hazijahakikiwa ndio zinazotumiwa na matapeli,”alisema.
Dk Bakari alisema utapeli unaoendelea hivi sasa unahusisha simu ambazo zimesajiliwa kwa kutumia vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Ametoa rai kwa wananchi kuhakiki ili kuhakikisha kuwa kitambulisho chake kinatumika kwa namba anazozifahamu.
Vifaa taka vya mawasiliano.
Dk Bakari amesema TCRA imeanza ukaguzi wa awali na utoaji wa cheti kwa vifaa vya mawasiliano vinavyoingia nchini ili kujiridhisha kwamba havijafikia mwisho wa matumizi yake.
Pia amesema kupitia utaratibu wa jinsi ya kuviteketeza pale vinapofikia ukomo wa matumizi bila kusababisha madhara kwa watumiaji kwa mujibu wa sheria.
“Ukaguzi huu unaenda sambamba na ukusanyaji wa awali wa gharama kwa ajili ya kugharamia utaratibu huu wa kuharibu vifaa vilivyoisha muda wake,”amesema.
Amesema gharama hii hutozwa kwa watengenezaji wa vifaa vya kieletroniki ambao wengi wako nje ya nchi.
Dk Bakari amesema zoezi la ukaguzi wa awali na ukusanyaji wa gharama hizi linafanywa na kampuni ya Bureau Veritas Tanzania Limited kwa niaba ya TCRA na kwamba limeanza rasmi Mei mwaka 2023.
Namba tambulishi zafungiwa
Dk Bakari amesema kuanzia Julai mwaka 2022 hadi kufikia Juni mwaka 2023 jumla ya namba tambulishi zilizofungiwa na mfumo huu ni 108, 395.
Amesema namba tambulishi hizo ni zile ambazo ziliripotiwa kupotea, kuibiwa au kuhusika katika matukio ya kihalifu, hivyo kuwezesha kupunguza matukio ya wizi na kusaidia upatikanaji wa vifaa vya mawasiliano vyenye ubora kwenye soko.