Taylor Swift akiri albamu zake sita kuuzwa bila kujua
Muktasari:
Mzozo baina ya Swift na Braun ulidumu kwa miezi kadhaa mwaka jana baada ya tajiri huyo kununua Big Machine, chapa ambayo mwanamuziki huyo amekuwa akiitumia kwa zaidi ya miaka kumi.
New York, Marekani (AFP).Taylor Swift amethibitisha kuwa haki za albamu zake sita za kwanza zimeuzwa bila ya yeye kujua, katika mzozo mpya kuhusu mauzo ya nyimbo zinazogharimu mamilioni za nyota huyo wa muziki wa pop.
Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 30 amekuwa mmoja wa wanamuziki wanaotegemewa kuzalisha fedha nyingi duniani baada ya nyimbo zake, kama "Shake It Off" na "I Knew You Were Trouble" kutamba katika chati za muziki kwa zaidi ya miaka kumi.
Lakini mwaka jana alianza kugombana hadharani na mfanyabiashara tajiri wa muziki, Scooter Braun, ambaye ni meneja wa wapinzani wake katika muziki wa pop; Justin Bieber na Ariana Grande, baada ya uamuzi wa kampuni yake wa kununua sehemu kubwa ya hisa katika rundo la nyimbo alizorekodi.
Swift alisema katika ujumbe alioandika katika akaunti yake ya Twitter kuwa amekuwa akijaribu kurudisha umiliki wa rekodi zake halisi (master) kwa mwaka mzima uliopita, baada ya gazeti la burudani la Variety kuripoti kuwa Braun aliuza mali hizo kwa dola 300 milioni za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh600 bilioni za Kitanzania).
Lakini licha ya kujaribu kuzungumza na Braun, alisema timu yake "imepokea barua kutoka kampuni binafsi ya Shamrock Holdings" ikitangaza kuwa imenunua music, video and albumu.
"Hii ni mara ya pili muziki wangu umeuzwa bila ya mimi kujua," ameandika akiongeza kuwa ameanza kurekodi nyimbo zake za awali. Braun hajajibu ujumbe wa Swift katika Twitter.
Swift aliahidi mwaka jana kuwa atapambana kuhakikisha anamiliki tena albamu zake sita za kwanza kwa kutengeneza nakala halisi zake mwenyewe. Alisema hayo wakati ambao kimkataba alikuwa huru kufanya hivyo kuanzia mwezi huu.
Mzozo baina ya Swift na Braun ulidumu kwa miezi kadhaa mwaka jana baada ya tajiri huyo kununua Big Machine, chapa ambayo mwanamuziki huyo amekuwa akiitumia kwa zaidi ya miaka kumi.
Wakati fulani Swift alisema Big Machine ilimzuia kutumbuiza nyimbo zake katika televisheni au kutoa makala katika mtandao wa Netflix -- madai ambayo kampuni hiyo ilikanusha.