Tanzania yatajwa miongoni mwa mataifa 10 yenye madeni madogo

Zanzibar. Hatua ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuitaja Tanzania miongoni mwa mataifa 10 ya Afrika yenye deni dogo la taifa imedhihirisha mafanikio ya mageuzi ya kiuchumi yanayoendelea nchini tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani karibu miaka mitatu iliyopita.
Chini ya utawala wake, Rais Samia ameongeza maradufu uwekezaji wa Serikali kwenye miundombinu na huduma za jamii, ikiwemo sekta za elimu, maji, afya, umeme na kilimo.
Uwekezaji wa Serikali, hususan kwenye ujenzi wa miundombinu, umechochea ukuaji wa uchumi nchini.
Kupitia mkakati wa Royal Tour, Rais Samia pia ameongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini na hivyo fedha za kigeni na ajira zimeongezeka nchini.
Serikali imeongeza bajeti kwenye sekta ya kilimo kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea tangu nchi ipate uhuru na hivyo kuongeza tija kwa wakulima nchini.
Sera rafiki za Serikali ya Rais Samia kwa sekta binafsi zimesaidia kuongeza kasi na ukubwa wa uwekezaji wa kampuni za nje na ndani ya nchi.
Rais Samia pia ameimarisha uhusiano wa kidiplomasia wa Tanzania na taasisi za kimataifa na nchi za nje ambazo zimeongeza utoaji wa misaada na mikopo yenye masharti nafuu kwa Tanzania.
Mikopo nafuu yenye riba ndogo na muda mrefu wa marejesho imepunguza mzigo wa deni la Taifa.
Pamoja na kwamba Tanzania imeendelea kukopa nje ili kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo, ukopaji makini wa Serikali ya Rais Samia wa kutumia mikopo nafuu badala ya mikopo yenye masharti ya kibiashara na ukuaji wa kasi kubwa wa Pato la Taifa (GDP), vimepunguza mzigo wa deni la Taifa.
Uwiano wa Deni la Taifa kulinganisha na GDP ambao hutumiwa na IMF na wachumi wengine duniani kupima uhimilivu wa deni la Taifa, uko chini Tanzania kulinganisha na wastani wa dunia.
Takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa jumla ya deni duniani sasa hivi ni Dola za Marekani trilioni 307, ambayo ni sawa na asilimia 336 ya GDP ya dunia.
Zifuatazo ni nchi 10 za Afrika zenye uwiano wa Deni la Taifa mdogo kabisa kwenye bara hilo kuilinganisha na pato la Taifa (GDP), kwa mujibu wa IMF.
DRC asilimia 11.1, Botswana asilimia 18.1, Ethiopia asilimia 31.2, Guinea Bissau asilimia 31.5, Equatorial Guinea asilimia 33.7, Comoros asilimia 36.9, Chad asilimia 38.7, Cameroon asilimia 39.6, Nigeria asilimia 41.3, Tanzania asilimia 41.8.
Nchi 10 duniani zenye kiwango kikubwa cha deni (uwiano wa Deni la Taifa kulinganisha na GDP) hizi hapa:
Japan asilimia 264, Singapore asilimia 160, Italia asilimia 145, Marekani asilimia 129, Hispania asilimia 113, Canada asilimia 113, Ufaransa asilimia 112, Uingereza asilimia 101, India asilimia 89 na Argentina asilimia 85.