Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yaanza kupigania chakula chake kitambulike kimataifa

Viongozi Chama cha Wapishi Tanzania (TCA), pamoja na uwakilishi wa bodi ya utalii Tanzania kwenye picha ya pamoja leo Julai 20, 2026, mara baada hafla ya awali ya uzinduzi wa tamasha la kimataifa linalolenga kukitangaza chakula cha Kiswahili litakalofanyika jijini Arusha.

Muktasari:

  • Chakula cha asili cha Tanzania kutangazwa ili kuitambulisha dunia kama ilivyo lugha yake ya Kiswahili.

Dar es Salaam. Sekta ya upishi na utalii wa chakula nchini inatarajiwa kupata mwelekeo mpya kufuatia Chama cha Wapishi Tanzania (TCA) kutangaza maandalizi ya tamasha kubwa linalolenga kukiinua chakula cha Kiswahili na kukipa hadhi ya kimataifa.

Chakula cha Kiswahili kinacholengwa ni kile kilichotengenezwa na bidhaa za Tanzania kama kuku wa kienyeji aliyepikwa na viungo vya Tanzania kama vile vya kutoka Zanzibar, vyakula vya kitamaduni ambavyo havipatikani kwenye hoteli zilizopo nchini lakini ni maarufu.

Vyakula kama ugali, mlenda, mboga za majani kama matembele, mchicha, mihogo, viazi vitamu, vyakula vya mazao bahari, maharage yanayolimwa hapa nchini, mbaazi, choroko.

Tamasha hilo, linalojulikana kama Tanzania Chefs' Culinary Festival 2026, linatarajiwa kuwa jukwaa la kwanza nchini litakalowakutanisha wapishi wa obesity, wanafunzi wa vyuo vya upishi, wamiliki wa hoteli, migahawa pamoja na wadau wa sekta ya ukarimu na utalii.

Akizungumza wakati wa hafla ya awali ya uzinduzi wa tamasha hilo leo Jumatatu, Julai 20, 2026, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti na rais wa TCA, Abbas Said amesema dhumuni kuu ni kutambua vipaji, kujenga ushindani wenye afya na kuzalisha mabalozi watakaoitangaza ladha ya Tanzania duniani.

Amekiri kwamba kwa sasa nchi ina wapishi wazuri ndio maana asilimia 90 ya hoteli za Tanzania zina wapishi wazawa.

“Umoja wa Mataifa wanatambua Kiswahili ndio lugha ya Afrika kwa nini wasitambue chakula cha Kiswahili. Kwa hiyo kupitia tamasha hili tunataka kuipa thamani lugha na Chakula cha Kiswahili,” amesema.

Amesema lazima vyakula vya Kiswahili vipikwe kwenye hoteli zetu ili mgeni akija kwenye nchi ya Kiswahili basi akute chakula cha Kiswahili.

Katika kuongeza chachu na msisimko, tamasha hilo litahusisha mashindano ya Taifa ya wapishi yatakayotoa fursa kwa wataalamu hao kutoka kila kona ya nchi kuonyesha ubunifu na uwezo wao wa kuandaa vyakula vya asili kwa viwango vya kimataifa.

Kadhalika, sekta ya utalii na ukarimu nchini kupitia tamasha hilo inalenga kukiweka chakula cha Kiswahili katika hadhi ya nyota tano kuelekea Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).

Itambulike kila Taifa ukienda wanavyo vyakula vyao hivyo na sisi tunataka watu watambue vyakula vyetu kama ilivyo wao kama anavyosema Ofisa Utalii Mwandamizi Bodi ya Utalii Tanzania, Zainab Seleman.

Amesema ipo mikutano mikubwa kama ule wa Umoja wa Mabunge duniani (IPU) utakaofanyika Arusha Oktoba mwaka huu, Miss World, AFCON itakayofanyika nchini kwa hiyo ni heshima katika kuitangaza Tanzania kupitia chakula cha Kiswahili kujenga uchumi kupitia sekta ya chakula.

Aidha, tamasha hilo la siku nne, linaloratibiwa na kampuni ya Devan Communication Consultancy kwa kushirikiana na TCA, linatarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 6 hadi 9, 2026 jijini Arusha likiwa na kaulimbiu isemayo "Flavours of Tanzania: Connecting Culture, Tourism and Community."

Mkurugenzi wa Devan Communication Consultancy, Salima Mseta, amesema lengo kuu la tamasha hilo ni kuanzisha kampeni ya kitaifa ya “Taste Tanzania” ili kuonyesha kuwa nchi ina utajiri mkubwa wa vyakula vya kipekee mbali na vivutio vya asili.

"Hatuzindui tamasha pekee, tunazindua harakati za kitaifa za kuitangaza Tanzania kupitia chakula chake. Tunataka kuelekea AFCON 2027, wageni maelfu watakaokuja wasikute tu viwanja na hifadhi nzuri, bali wakute chakula cha Kiswahili kilichopewa hadhi ya nyota tano ili kila mgeni akiondoka aseme 'nimeionja Tanzania'," amesema Mseta.