Tanzania na Kenya zasaini makubaliano ya kuondoa vikwazo mpakani

Muktasari:
- Serikali za Tanzania na Kenya zimetia saini ya makubaliano ya kuondoa vikwazo vilivyokuwa vikiwazuia kufanya biashara kwa pamoja.
Arusha. Serikali za Tanzania na Kenya zimetia saini ya makubaliano ya kuondoa vikwazo vilivyokuwa vikiwazuia kufanya biashara kwa pamoja.
Akizungumza jana wakati wa kusaini makubaliano hayo na Kenya,Waziri wa Viwanda na Biashara Tanzania, Profesa Kitila Mkumbo alisema kuwa utiaji wa makubaliano hayo ni mojawapo ya jitihada za kuwezesha mahusiano ya biashara na nchi jirani kufuatia ziara iliyofanywa nchini Kenya na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Mei 4 hadi 5 ambapo katika ziara hiyo masuala kadhaa yalifanyika ikiwemo kongamano la biashara baina ya wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya.
Alisema kuwa, katika kongamano hilo ambalo lilizinduliwa kwa pamoja na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu na Uhuru Kenyatta wa nchini Kenya, ambapo kwa pamoja marais walielekeza mawaziri wanaosimamia sekta ya biashara nchini Tanzania na Kenya kukutana mara moja ndani ya mwezi kwa ajili ya kujadili masuala ya biashara vikiwemo vikwazo vya biashara vilivyokuwa vya kiushuru.
"Kutokana na mkutano huo , Tanzania imeratibu mkutano baina ya Tanzania na Kenya kwa ajili ya masuala mbalimbali ya biashara baina ya nchi zetu mbili, ambapo katika mkutano wa nne uliofanyika April 23 hadi 27, mwaka juzi jijini Arusha, jumla ya vikwazo 37 vilijadiliwa na kati ya hivyo vikwazo 19 viliondolewa na pande zote mbili zilikubaliana na kuweka mpango maalumu wa kutatua masuala yaliyobaki," aliongeza Waziri huyo.
Alisema kuwa katika mkutano huu wa tano wameweza kujadili masuala mbalimbali ya biashara katika sekta ya kilimo, forodha, uhamiaji na usafirishaji ambapo jumla ya masuala 64 yamejadiliwa ambapo kati ya hayo masuala 30 yametatuliwa na masuala 34 yaliyobaki yamewekewa mkakati maalumu na muda wa utekelezaji.
Aidha alisema kuwa miongoni mwa masuala makuu manne waliyotatua upande wa Tanzania ni pamoja na kuwezesha upitishaji wa bidhaa mpakani hususani vinjwaji baridi kama juisi kutoka Tanzania kwenda Kenya.
Aidha kuondolewa kwa tozo za ukaguzi zilizokuwa zinatozwa na mamlaka ya Kenya kwenye bidhaa za Tanzania ikiwemo unga wa ngano wenye alama ya ubora kutoka mamlaka husika Tanzania.
Waziri Mkumbo alisema kuwa miongoni mwa masuala mengine waliyotatua ni pamoja na kuwezesha upitishaji wa mahindi kutoka Tanzania kwenda Kenya pamoja na kuondoa ushuru wa asilimia 25 kwenye bidhaa za kioo kutoka Tanzania kwenda Kenya.
Waziri alisema kwa upande wa Kenya, mambo ambayo wameweza kukubaliana ni pamoja na kutoa upendeleo kwa bidhaa za saruji zinazozalishwa nchini Kenya ambazo zinakidhi matakwa ya vigezo vya uasili wa bidhaa za jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema kuwa jambo lingine ni kutoa upendeleo maalumu kwa vinywaji kutoka Kenya ikiwemo juisi za nanasi baada ya kukidhi vigezo vya bidhaa vya jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha jambo lingine ni kuhakikisha bidhaa zinazoharibika haraka kama vile maziwa zinapewa kipaumbele zinapovuka mipaka kutoka Kenya kuingia Tanzania kwa kuzingatia taratibu za sheria ya forodha, huku jambo lingine likiwa ni kuongeza muda wa kibali cha kuingiza bidhaa za mifugo kutoka siku 15 hadi siku 30.
Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Maendeleo ya ujasiriamali kutoka nchini Kenya, Betty Maina alisema kwa kufanya jambo hilo ni hatua nzuri katika maagizo ya viongozi wakuu wa nchi zetu mbili katika kuimarisha biashara kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi Tanzania na Kenya.