Tanzania kunufaika ziara ya Rais Samia India

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar esa Salaam leo. Picha na Sunday George
Muktasari:
Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu (Oktoba 8 – 11) nchini India, akiambatana na mawaziri mbalimbali, ambapo Tanzania inatarajiwa kunufaika katika sekta za afya, kilimo na viwanda.
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba ametaja maeneo sita ambayo Tanzania itanufaika kutokana na ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini india.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Oktoba 5, 2023, jijini Dar es Salaam, Makamba amesema ziara hiyo ya kikazi ya siku tatu inayotarajia kuanza Oktoba 8 -11, inatokana na mwaliko maalumu wa viongozi wa Taifa hilo.
Kwa mujibu wa Makamba, maeneo ambayo Tanzania itanufaika ni katika sekta za viwanda, afya, kilimo, elimu, maji na usafiri wa majini.
"Kwa mfano, kwa upande wa elimu; kutokana na uhusiano mzuri wa diplomasia na kiuchumi baina ya nchi zetu, kumekuwa na mpango wa kubadilishana wanafunzi.
“Mpango huo unahusisha kozi mbalimbali, sasa kupitia ziara hii, kuna nafasi 1000 za mafunzo katika sekta mbalimbali ambazo kwazo watanzania watanufaika.
“Kama mnavyojua, India ni miongoni mwa mataifa yanayoongoza katika mapinduzi ya kidijatali, sasa matokeo ya ziara hii ni viwanda na wawekezaji kuja nchini,” amesema.
Matarajio mengine kutoka na ziara hiyo ya Rais Samia nchini India kwa mujibu wa Waziri Makamba, ni kuvutia wawekezaji katika Tehama.
"Tunatarajia viwanda vya simu janja kuwepo nchini, haya ni moja ya matokeo tunayoyatarajia baada ya ziara. Pia India imefanikiwa katika sekta ya afya tunatarajia kuimarisha na kuongeza wigo katika sekta hii, hasa ukizingatia maboresho makubwa yanayoendelea kufanywa na serikali kwenye sekta ya afya,” amesema.
India ni miongoni mwa mataifa ambayo vyanzo vikuu vya uwekezaji wake na biashara baina yake na Tanzania, imekuwa kwa kasi kwa miaka ya hivi karibuni, kwani wawekezaji kutoka nchi hiyo, wamekuwa wakiona Tanzania kama sehemu sahihi ya biashara.
"Inatarajiwa kuwa, baada ya ziara hii, kutaanzishwa taasisi ya upandikizaji wa figo nchini, pia kutaanzishwa kiwanda cha kutengeneza chanjo ya binadamu na wanyama, ambapo maandalizi hayo yanaendelea.
“Tutaongeza ushirikiano kati ya hospitali za Tanzania na India ikiwemo kuboresha uwezo na utalaamu na weledi wa matibabu katika taasisi hizi."
Amesema Tanzania itarahisisha upatikanaji wa dawa zenye ubora na kwa gharama nafuu nafuu, huku kwenye kilimo akisema, masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini yatapatikana.
"Kama mnavyofahamu tunazalisha korosho na mbaazi moja ya matokeo ya ziara ya Rais Samia ni kuhakikisha soko la bidhaa hizo linakuwa la uhakika na la kudumu hasa kwa zao la mbaazi ili wakulima wetu wasiwe na mashaka.
“Kwa ushawishi wa Rais Samia, tunaamini wawekezaji wakubwa watashawishika kuja nchini, ikiwemo kuanzia kongani ya viwanda. Tumejipanga kuanza na ekari 10,000 ambapo kampuni kubwa za India zitaanzisha viwanda nchini," amesema.
Agenda nyingine katika ziara hiyo, ni kuweka msukumo kwa Serikali ya India kuanzisha karakana ya usafiri wa vyombo vya maji nchini, na kwamba itawezesha Tanzania kuwa utaalamu na uwezo wa kutengeneza vyombo hivyo.
Makamba ambaye amewahi kuwa Waziri wa Nishati amesema wanatarajia ziara ya Rais Samia nchini India itawezesha kuanza kwa mradi mkubwa wa maji kutoka ziwa Victoria na kuyasambazwa katika miji 24.
Amesema jambo jingine ni kutafuta fursa mbalimbali kwa kuwavutia wawekezaji hasa katika katika sekta za kimkamati za viwanda, afya, biashara, elimu, ulinzi na usalama pamoja na uchumi wa buluu.
Makamba amesema miongoni mwa matukio mengine yatakayojitokeza ni Serikali ya Tanzania itabadilishana mikataba ya makubaliano na Serikali ya India ambayo yatasainiwa kama sehemu ya ziara hiyo.
“Kuna mikataba 15 itakayosainiwa katika sekta za afya, elimu maji, kongani za viwanda, lakini tunatarajia itaongezeka kwa siku chache kabla ya ziara kuanza,” amesema Makamba.
Akizungumzia ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Biashara Kilimo na Viwanda Tanzania (TCCIA), Mwanahamisi Hussein amesema itasaidia kuongeza uwekezaji utakaowezesha kukua kwa uchumi na hatimaye kupata fedha za kigeni.
“Tutaongeza ajira kwa sababu kupitia wawekezaji watakaokuja sambamba na kuongeza masoko ya bidhaa zinazozalishwa Tanzania.
“TCCIA ni moja ujumbe utakaokwenda katika ziara hiyo, tutakwenda kusaini makubaliano na chemba ya biashara na chakula za India," amesema Hussein.