Tanzania kuanza utafiti nguvu ya nyuklia kuzalisha umeme

Makamu Mwenyekiti wa kamati ya PIC (katikati), Augustine Vuma akitembelea Tume hiyo kujionea miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa maabara ya kisasa
Arusha. Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imesema imejipanga kuhakikisha maabara yake ya kisasa iliyopo mkoani Arusha inatumika kuzalisha matokeo ya tafiti, kujibu changamoto kwenye teknolojia husika na pia kuongeza fursa za matumizi ya teknolojia hii.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Oktoba 23, 2023 jijini Arusha na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu, Elimu katika Wizara ya Sayansi na Teknolojia, Profesa Ladslaus Mnyone wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ilipofanya ziara katika tume hiyo na kutembelea miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa maabara iliyojengwa kwa zaidi ya Sh10.4 bilioni.
Amesema wanajipanga ili waone jinsi gani Wataalamu wanafanyia utafiti Teknolojia ya Nyuklia ili iweze kutumika katika kuzalisha Umeme kama ambavyo nchi ya China inavyotumia teknolojia hiyo kuzalisha umeme.
"Hili linaweza kuwa eneo mojawapo ambalo wataalamu wetu wanaweza kulifanyia utafiti na kuangalia namna ya kulitumia kwani ni fursa kubwa kwetu kama ambavyo wenzetu wa nchi za nje wanavyonufaika na teknolojia hiyo," amesema Mnyone.
Aidha ameongeza teknolojia hiyo inaweza pia kutumika katika kudhibiti viumbe waharibifu ambao husababisha athari mbalimbali mfano mbung'o.
Mkurugenzi wa Tume hiyo, Profesa Lazaro Busagala amesema majukumu ya tume hiyo ni kudhibiti matumizi salama ya mionzi nchini, kuhamasisha na kuendeleza matumizi salama ya Teknolojia ya Nyuklia, kufanya utafiti na kutoa ushauri na taarifa mbalimbali juu ya Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia.
Amesema dhima ya tume hiyo ni kusimamia na kudhibiti matumizi salama ya mionzi ili kulinda umma, wafanyakazi pamoja na mazingira dhidi ya madhara ya mionzi na kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.
"Tume imekuwa na kazi ya kukagua vituo vyote vyenye vyanzo vya mionzi ili kusimamia utekelezaji wa sheria ya Nguvu za Atomiki na kanuni zake, pamoja na kupima sampuli za vyakula, mbolea, vyakula vya wanyama, tumbaku na mazao yake vinavyoingizwa na kusafirishwa nne ya nchi," amesema Profesa Busagala.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Augustine Vuma amesema matumizi ya mionzi imekuwa sehemu ya ajenda ya dunia katika sekta ya kilimo, afya, usalama na mengine kwa hiyo ujenzi wa maabara hiyo ya kisasa ni fursa kwa taifa kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
Aidha ameishauri serikali kuendelea kuwekeza katika Tume hiyo kwani juhudi zilizofanywa na serikali katika tume hiyo ni kubwa sana ikiwemo kupanua ofisi zilizokuwepo 12 na sasa hivi kufikia ofisi 58 hayo ni maendeleo makubwa sana hivyo waendelee kuongeza wataalamu wa mionzi ili kuongeza ufanisi wa kazi.
Inatajwa juhudi za kuongeza utoaji wa elimu katika jamii unaendelea kuhakikisha kwamba wananchi wengi zaidi wanapata uelewa wa faida na matumizi ya teknolojia ya nyuklia.