Tanesco, TRC zatakiwa kuwa na ‘Backup” umeme SGR

Kamati ya Kudumu ya Bunge Nishati na Madini, ikiwa kwenye kituo cha kuzalisha umeme Kinyerezi jijini Dar es Salaam leo Novemba 16, 2023.
Muktasari:
- Kamati ya kudumu ya Bunge Nishati imefanya ziara katika kituo cha uzalishaji umeme Kinyerezi jijini Dar es Salaam kuangalia maendeleo ya mradi wa uwekaji mtandao wa umeme katika reli ya kisasa ya SGR ambapo Kamati imeishauri Tanesco kukaa na TRC kuangalia namna ya kuwa na njia ya ziada ya uendeshaji treni ya umeme.
Dar es Salaam. Shirika la Umeme Nchini, (Tanesco) pamoja na Shirika la Reli (TRC), yatakuwa kuandaa mpango wa kitaalamu kwaajili ya nishati ya dharura 'Backup' endapo gridi ya taifa ikizima wakati wa treni ya umeme ikianza kufanya kazi.
Ushauri huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Nishati, Kilumbe Ng'enda pale walipofanya ziara katika kituo cha uzalishaji umeme Kinyerezi jijini Dar es Salaam kuangalia maendeleo ya mradi wa kuweka mtandao wa upatikanaji umeme katika reli ya kisasa SGR.
"Tumewashauri wakae waone namna ya kuwa na 'backup' (njia ya ziada), kama gridi ya taifa ikizima basi treni ya SGR iweze kufanya safari hata kama sio kikamilifu lakini iweze kuwafikisha abiria vituoni," amesema.
Hata hivyo Ng'enda ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini, amehakikisha upatikanaji wa umeme wa gridi ya taifa ni wa uhakika kwakuwa haukatiki.
Amesema wanaweka tu tahadhari ya kibinadamu na matukio yanayoweza kutokea lakini hawategemei treni itakosa umeme akitolea mfano ndani ya miaka 6 umeme umekatika maramoja tu tena kwa dakika zisizozidi 15.
"Gridi ya taifa sio umeme huu unaozalishwa tu hapa Kinyerezi hata wa bwawa la Nyerere ukizalishwa unaingia gridi ya taifa na gridi inalindwa kitaalamu kuhakikisha umeme unaingia kutoka vyanzo mbalimbali unapozalishwa," amehakikisha.
Aidha amesema kama kamati imeridhishwa na maendeleo ya mradi huo ambao umefikia asilimia 100 kipande cha Dodoma Morogoro, na asilimia 99 kutoka Dodoma hadi Kitinku Singida.
Vilevile ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka fedha kwenye sekta ya nishati kuhakikisha watanzania wanaendelea kuwa na umeme wa kutosha.
Azingumzia hali ya upatikanaji wa umeme kwa sasa, Naibu Waziri wa Nishati ambaye ameambatana kwenye ziara hiyo, Judith Kapinga amesema wameendelea na jitihada za kupunguza mgawo nchini lengo ikiwa ni kuumaliza.
"Tumeendelea kutekeleza maelekezo ya Rais Samia aliyetaka kufanyika matengenezo ya mitambo ya kuzalisha umeme.
Kapinga amesema wanaendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji wa umeme kama Bwawa la la Nyerere ambalo kwa sasa limefikia asilimia 94.
"Niwahakikishie azma yetu ni kulitoa taifa kwenye mgawo ili Watanzania wapate umeme wa uhakika ambao unatumika katika shughuli za uzalishaji," amesema Kapinga.
Kauli ya Kapinga inaungana na Mkurugenzi wa Uzalishaji umeme Tanesco,Pakaya Mtamakaya aliyesema kuwa kwa sasa wanasubiri kuenea kwa mvua kote nchini ili wazidi kuzalisha.
"Ukiangalia mvua imenyesha Ukanda wa Pwani Tanga ambapo kuna kituo cha uzalishaji kilichoongeza megawati 68 lakini Dodoma mvua bado ambapo kuna kituo cha Mtera, hata Kihansi, kwahiyo tunasubiri mvua zisambae tuongeze uzalishaji," amesema Mtamakaya alipoulizwa na Mwananchi.
Akijibu swali kuhusu kuanza kwa treni ya SGR, Mkurugenzi wa Shirika la Reli nchini, Masanja Kadogosa amesema suala la kuanza kwa treni hiyo ni mchakato 'process' kwakuwa kuna kuhusisha hatua kama vile kujaribu mitambo ambayo wanaendelea kuipokea.
Kagodosa amesema kwa sasahivi kuna ujaribishaji wa miundombinu ya reli pamoja na umeme ambayo inaendelea vyema.
"Tumechelewa kwakuwa tulikuwa hatuna vichwa vya treni lakini kwasasahivi tumeshapokea Kichwa na vingine vitatu vinakuja na nafikiri hadi katikati ya Desemba vitaingia vingine vitatu na tutakuwa navyo vinne," amesema.
Amesema kwasasa wanaendelea kujaribu kichwa kilichokwishakuja waone kama kinaenda km160 kama inavyotakiwa. Kadhalika amesema wataendelea kutoa taarifa za majaribio.