Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DC Malisa kuwashughulikia ‘vishoka’ ardhi Mbeya

Wananchi Kata ya Iduda jijini Mbeya wakimsikiliza mkuu wa Wilaya hiyo, Beno Malisa (hayupo pichani) wakati wa mkutano wa kusikiliza na kutatua kero ya ardhi kupitia kampeni ya 'Kliniki ya ardhi' iliyoanza leo.

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa ameanzisha kampeni ya ‘Kliniki ardhi’ inayolenga kusikiliza na kutatua kero za wananchi na kutoa elimu kuhusu umiliki wa ardhi na kuongeza ufanisi wilayani humo.

Mbeya. Halmshauri ya Jiji la Mbeya inakusudia kukamilisha malipo ya fidia kwa wananchi 152 ifikapo Februari mwakani, ambao maeneo yao yamepimwa kwaajili ya ujenzi wa miundombinu.

Wananchi hao ni kati ya 695, ambapo halmashauri hiyo ilikuwa inahitaji Sh1.5 bilioni, kwa ajili ya fidia hiyo, hata hivyo, wananchi 543 tayari wamelipwa stahiki zao.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 27, 2023; katika kampeni ya ijulikanayo kama ‘kliniki ya ardhi’ inayoendeshwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa; ikiwa na lengo la kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi, sambamba na utoaji wa elimu ya umiliki wa ardhi, na hivyo kuongeza ufanisi.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye kliniki hiyo, Mkuu wa Idara ya Mipango Miji katika Halmashauri hiyo, Dickley Nyato, amesema hadi kufikia mwezi Februali watakuwa wamemaliza malipo hayo.

“Jumla ya wananchi walikuwa 695, ambapo fidia yao ilikuwa ni zaidi ya Sh 1.5 bilioni, ambapo hadi sasa watu 543 tayari wamelipwa huku wakisalia 152 ambao tulipanga kuanza kuwalipa mwezi huu wa Oktoba, lakini kutokana na deni wizarani, hatukufanikiwa,” amesema na kuongeza;

“Kwa maana hiyo wananchi hawa watalipwa kwa awamu tatu ambazo ni ile ya Novemba, kisha Desemba na tutakamilisha Januari mwakani. Na kuhusu orodha ya majina ili kila mmoja ajue analipwa awamu ipi, tutaiweka hadharani Jumanne wiki ijayo.”

Kuhusu fidia upande wa umeme, wananchi wametakiwa kuwasilisha malalamiko yao kwa Meneja wa Shirika la Umeme (Tanesco) mkoani humo, ambao watayachakata na kuaywasilisha makao makuu ya shirika hilo kwa hatua ya utekelezaji.

DC Malisa kwa upande wake anaona kuna umuhimu wa kampeni hiyo kuwa endelevu na kwamba kila Ijumaa, watapita kila kata jijini humo, huku akitilia mkazo wa kujikita zaidi katika utatuzi wa migogoro ya ardhi ambayo ndio kinara wa changamoto wilayani humo.

“Tutapita katika kata zote 36, tukihakikisha tunatatua kero za wananchi, leo tumeanza na Iduda, eneo la ardhi ndio lenye kero nyingi lakini nyingine zinasababishwa na vishoka ila tutapambana nao. Katika kliniki hii tutatoa elimu ya umiliki ardhi, kusikiliza na kutatua kero za wananchi na kuongeza ufanisi kwa viongozi kwani nitaambatana na wakuu wa idara zote,” amesema Malisa.

Mmoja wa wananchi katika kata hiyo, Vumilia Suha ambaye pia ni Mjumbe wa Mtaa wa Mwale, amesema wamepewa matumaini katika mkutano huo na kwamba wanachosubir ni utekelezaji.

“Baadhi ya wananchi walishaonesha dalili za kukata tamaa wakitutupia lawama, hivyo kwa kuwa Mkuu wa Wilaya na kamati yake wametamka, basi tunasubiri utekelezaji,” amesema na kuongeza;

“Tulianza kudai fidia mwaka 2019 wapo ambao walipata lakini wengine zaidi ya 100 walikuwa bado wanasotea haki yao hivyo iwapo watalipwa amani kwa Serikali itaendelea.”