Brela watakiwa kujiimarisha mtandaoni kudhibiti vishoka

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba akiwa kwenye moja ya banda la mjasiliamali katika maonyesho yaliyoandaliwa na Brela katika viwanja vya Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Brela watakiwa kuimarisha mifumo ya kimtandao kwa kuwasaidia wafanyabiashara katika urasimishaji na kutumia maonyesho waliyoandaa kushirikiana na wadau kwa kupokea maoni yao ikiwepo taasisi za Serikali.
Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba amewataka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) kuimarisha mifumo ya kimtandao katika usajili ili kuepukana na vishoka.
Kwa mujibu wa DC hyo, teknolojia imewasaidia wananchi wengi kuepukana na dhuluma na utapeli lakini katika usajili wa biashara na kampuni, watu wengi wamekuwa wakionyesha kana kwamba kusajili biashara ni gharama kubwa.
Komba ameyasema hayo jana Jumanne Oktoba 24, 2023 wakati wa ufunguzi wa maonyesho yaliyoandaliwa na Brela katika viwanja vya Mlimani City jijini Dar es Salaam, yaliyokutanisha wadau mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Komba amesema ameagizwa kuwaambia Brela kuangalia namna ya kuendelea kusaidia wafanyabiashara ili kurasimisha biashara zao.
"Kama mnavyofahamu Mkuu wa Mkoa, Albert Chalamila anatoa kipaumbele kwenye masuala ya uchumi hivyo amewataka yasiishie hapa bali yafanyike na sehemu nyingine ili kuwahusisha wadau wengi zaidi," amesema Komba.
Amesema Serikali inatambua uwepo wa wafanyabiashara wakubwa na wadogo katika kuhakikisha wanakuza sekta ya uchumi ni lazima warasimishe biashara zao kwa kusajili katika taasisi husika.
Amesema maonyesho hayo yatumike kufanya tathimini ya kina kupitia wadau kwa kufuata maoni yao ili kuboresha shughuli za wafanyabiashara kwa wale ambao bado hawajarasimisha biashara zao hivyo Brela wanatakiwa kufanya kazi kwa karibu na wadau hao.
"Watu wanahangaika katika usajili katikati ya biashara wapo watu wanajitoa halafu wanakwenda kutoa bidhaa ambayo mwenzao amesajili kwa kuwa wanajua namna ya kutengeneza bidhaa hizo kiukweli hiyo inaumiza sana," amesema Komba.
Pia, amesema maonyesho hayo yatumike kuimarisha uhusiano na sekta mbalimbali za serikali ili kurahisisha shughuli za Brela kwa urahisi ikiwepo Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).
Awali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Godfrey Nyaisa amesema maonyesho hayo yamefanyika kwa mara ya kwanza kwa lengo la kukutanisha wadau wote ambao wanafanyanao kazi na itakuwa mwendelezo kuona ni namna gani wanasaidia wafanyabiashara wanarasimisha biashara zao kwa kusajiliwa.
"Kwa kuwa ni maonyesho yetu ya kwanza na tulionankuna haja ya kuwa karibu na wadau wetu tulikaa na kuamua tufanye hivi lakini tupo tayari kupokea maelekezo kutoka kwako kwenu kwa ajili ya kufanyia kazi," amesema Nyaisa.
Amesema hadi sasa wana taasisi 11 ambao wapo katika maonyesho hayo na wajasiriamali zaidi ya 100, pia wanatarajia kuwa na mkutano wa wadau wote utakaokutanisha wafanyabiashara na kampuni mbalimbali utakaofanyika Oktoba 27 mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa The Chill Republik, Anyamlye Mtetemela amesema maonyesho hayo yatawasaidia kujitangaza na kulinda majina yao katika kufanya biashara zao.
Amesema maonyesho hayo yasifanyike mara moja endapo kutakuwa na uwezekano yafanyike mara tatu kutokana na wingi wa wafanyabiashara ambao wanahitaji mialiko ili kujitangaza kama ilivyo wao.
"Wapo wafanyabiashara huko mkoani hawajui utaratibu wa kufuata katika usajili hivyo wanaposikia fursa za namna hii wanatembelea mabanda na kufahamu kinachoendelea na itamtengenezea mazingira ya kujiamini zaidi,"alisema Mtetemela.
Pia amesema kujisajili kupitia Brela imerahisisha kwa wao kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha kwa kuwa biashara zao zinatambulika kisheria na imewapa nguvu ya kuendelea kulinda majina ya kampuni zao.
Msimamizi wa kampuni ya Woiso Original Product, Justine Msigwa amesema faida ambayo wanaipata ni kutambulika kwenye taasisi mbalimbali na hivyo kupewa tenda kwa kuaminika.
"Licha ya kulinda jina lakini ukishakuwa kwenye usajili inatoa fursa ya kupata wateja kwenye sekta muhimu kwa kuwa biashara inakuwa inatambulika kisheria baada ya kusajiliwa na taasisi inayotambulika.
Mkurugenzi wa Mpanda, Neema Batiki amesema amekuwa akishiriki kwenye maonyesho mbalimbali huku swali kubwa akiulizwa kama amejisajili kwenye mamlaka husika ili apewe tenda za kupeleka bidhaa zake sehemu mbalimbali.
"Maonyesho yanakutanisha watu wengi hivyo wanapofika kwenye banda langu walitaka kufahamu kama nimesajiliwa ukijibu ndiyo wanachukua mawasiliano kwa ajili ya kukutafuta kwa kufanya nao kazi ndani na nje ya nchi," amesema Neema.