Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Brela, FCC zaweka mkazo usajili alama, urasimishaji biashara

Baadhi ya wananchi wakipata huduma za usajili wa biashara na elimu katika banda la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) baada ya kutembelea maonesho ya 18 ya biashara ya Afrika Mashariki katika Uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela Mkoa wa Mwanza. Picha na Damian Masyenene

Muktasari:

Usajili wa majina ya biashara, alama, huduma, makampuni, kutoa hataza (patent), leseni za biashara kundi A, leseni za viwanda, kuhuisha taarifa za makampuni na majina ya biashara huwezesha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza na kufanya biashara nchini


Mwanza. Wawekezaji, wajasiriamali na wananchi wanaofanya biashara nchini wametakiwa kusajili na kurasimisha majina, alama za biashara na huduma ili kujiendesha kihalali.

Akizungumza na Mwananchi Digital Septemba 2, 2023 kwenye maonesho ya 18 ya biashara Afrika Mashariki katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza; Ofisa Leseni wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Fransice Filimbi amesema kwa kufanya hivyo bidhaa zao zitashindana, kutambulika katika masoko ya kitaifa na kimataifa pamoja na kulisaidia taifa kukuza uchumi wake.

Filimbi amesema wafanyabiashara wengi wamekuwa wakiendesha biashara zao na kutumia majina ya biashara bila kuyasajili na kuyarasimisha, pindi wanapopata zabuni kubwa na kutakiwa kupeleka uthibitisho wa umiliki na usajili wa biashara zao, wanakuta majina hayo yamesajiliwa na watu wengine.

“Tuko hapa kuwapa elimu wateja wanaokuja kwetu na kutoa huduma saidizi ikiwamo leseni, kujua namna ya kurasismisha viwanda vyao na alama zao za biashara na huduma (trademark) kwahiyo tunawapa usaidizi wa kuwasajilia na kuwarasimishia hapa hapa na wanaondoka na vyeti vyao,”

“Kutokana na elimu ambayo inaendelea kutolewa kwa sasa wengi wamehamasika wanakuja kuhakikisha kwamba hilo jina halipo na anaanza kulisajili….kwa ambao tayari wako huko wanatumia majina bila kuyarasimisha tunawashauri wafike kwetu wajisajili na kurasimisha majina yao, kampuni zao, alama zao za biashara pamoja na huduma, kusajili viwanda na kupata leseni za biashara kundi A,” amesema Filimbi

Ofisa Habari wa Brela, Gloria Mbilimonywa amewataka wananchi wenye vumbuzi, bunifu, alama za biashara na hataza kufanya usajili wa umiliki ili kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana katika mfumo rasmi na Brela inasaidia kuzipa biashara zao uhai wa kisheria.

“Tunaendelea kufanya maboresho ili kutoa huduma rahisi na za uhakika ambazo zinatolewa kwa haraka na ni rafiki kila mwananchi anaweza kufikiwa bila usumbufu wowote,” amesema Gloria

Mmoja wa wafanyabiashara waliofika kusajili kampuni, Ochieng James ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi, amewataka wafanyabiashara kujitahidi kusajili kampuni zao kwa sababu wanapofanya biashara bila kusajiliwa wanakwenda kinyume na sheria.

“hata biashara haitaeleweka kutokana na kushindwa kuiweka wazi na unapokuwa umedhulumiwa unashindwa kupata haki yako kwahiyo tuache kuchukua leseni za wenzetu kusajilia kampuni,”amesema

Naye, Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) Kanda ya Ziwa, Frank Mdimi amewataka wajasiriamali wanapotengeneza bidhaa zao wakumbuke kusajili alama zao za bidhaa kwa mamlaka husika na kuhakikisha bidhaa hizo zinakidhi viwango vilivyowekwa kitaifa na kimataifa, huku wananchi wakitakiwa kuongeza umakini wanapofanya manunuzi ili wasiwe wahanga wa bidhaa bandia.

 “Tunashauri pia wakandarasi wanapokwenda kununua bidhaa ambazo wamezishindia zabuni zao wanunue kutoka kwa wasambazaji ama wagavi ambao ni sahihi na halisi wa bidhaa husika kwa sababu tumeshapata kesi ambazo zinahusiana na makampuni ya umma ambao bidhaa hizo zinauzwa kwao tu na wameuziwa bidhaa bandia kwahiyo tunashauri wawe makini katika eneo hilo,” amesema Mdimi