Tamu, chungu teknolojia ya kuotesha nywele au zisiote

Muktasari:
- Umewahi kuwaza kupata tiba ya kuondoa nywele kichwani au kama una kipara kuotesha nywele. Hilo linawezekana, lakini madaktari wameeleza uchungu na utamu wa tiba hiyo.
Dar es Salaam. Umewahi kuwaza kupata tiba ya kuondoa nywele kichwani au kama una kipara kuotesha nywele. Hilo linawezekana, lakini madaktari wameeleza uchungu na utamu wa tiba hiyo.
Teknolojia ya uondoaji nywele ijulikanayo kama Laser Permanent hair remover ambayo hutumia mionzi hutoa matokea kwa mhusika baada ya kufanya huduma kuanzia mara tatu na kuendelea. Daktari bingwa wa upasuaji Hospitali ya Bugando, Francis Tegete alisema teknolojia hiyo hutumia mionzi kuua seli zinazofanya nywele kuota.
Mionzi hiyo inapopigwa katika sehemu husika hufanya uharibifu wa seli zinazosababisha ukuaji wa nywele na kukomaa kuanzia katika shina (mzunguko wa nywele unapoanzia) na kuifanya isiweze kukua tena ikiwa mtu huyo atafanya zoezi hilo kuanzia mara tatu hadi saba.
“Hii hutumiwa na watu tofauti kama wanawake wanaoota ndevu na hawazitaki, huwasaidia kuziondoa moja kwa moja, kama mtu hazihitaji nywele za sehemu fulani,” alisema Dk Tegete.
Pia, alisema katika uondoaji wa nywele hizo ipo dawa maalumu inayopakwa eneo husika ili kusaidia upatikanaji wa matokeo yaliyokusudiwa.
“Mionzi inayotumika si kama ile inayotumika kutibu saratani, ni teknolojia ambayo bado hakuna utafiti unaoonyesha kama kuna madhara ya muda mrefu mtu huweza kuyapata,” alisema Dk Tegete.
Katika kliniki inayotoa huduma hii Dar es Salaam, wateja wengi wameelezwa kuondoa nywele za kwapani, sehemu za siri, ndevu kwa wanawake na hata baadhi ya wanaume ambao wana ndevu nyingi wameonekana wakizitengenezea muonekano mzuri.
Kuhusu gharama za huduma, mteja atatakiwa kulipia kulingana na huduma anayohitaji. Kwa wanaohitaji kuondoa nywele za kwapa na sehemu za siri watatakiwa kulipia Sh100,000 kwa kila huduma na atalipa kila atakapotembelea kliniki hiyo kwa ajili ya huduma.
Na ili mtu kupata matokeo mazuri ya uondoshaji nywele hizo hutakiwa kupata huduma walau kuanzia mara nne na kuendelea kila baada ya wiki nne hadi sita.
Lakini madaktari wanabainisha kuwa nywele za sehemu za siri hazipaswi kuondolewa kutokana na umuhimu wake, hasa kuzuia bakteria na wadudu mbalimbali kuingia mwilini, husaidia kupunguza hatari ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa na kuzuia uchafu na vimelea.
“Kuondoa nywele sehemu za siri kunaweza kuongeza hatari ya magonjwa ya zinaa, mara nyingi wengi wakinyoa wanapata vipele au vidonda, hapo inakuwa rahisi kupata maambukizi, unanyoa na kuziacha kidogo lakini ukiziondoa kabisa umeondoa ulinzi,” alisema daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo kwa mwanamume, Erasto Wambura alipozungumza na Mwananchi, Mei 12.
Kuotesha nywele
Dk Tegete alisema uoteshaji nywele hufanyika kwa aina tofauti, ikiwamo kunyofoa nywele kuanzia mzizi wake na kuipandikiza upya au kuchakata virutubisho vinavyotokana na mwili wa mhusika na kuviingiza katika sehemu ambayo nywele huoteshwa.
“Hii hufanyika kwa wale wenye vipara ambavyo kitaalamu huwa tunavigawa katika classification saba na mtu anapohitaji huduma hii huwa tunaangalia yupo hatua gani,” alisema Dk Tegete.
Kwa mujibu wa mmoja wa wahudumu katika kliniki hiyo alipozungumza na mwandishi kwa njia ya simu, alisema ili mtu aweze kuotesha nyusi ni Sh400,000, kuotesha nywele kwenye kipara ni Sh400,000 ambazo zote huweza kuleta matokeo chanya baada ya huduma moja.
Kujaza nywele kwa wale ambao hawana (kipara) au ziko chache kichwani gharama ilitajwa kuwa Sh550,000, huku akitakiwa kulipia Sh300,000 katika hatua ya kwanza.
Wananchi wazungumza
Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili walionyesha wasiwasi wao kuhusu teknolojia hiyo, huku wakitaka tafiti zaidi kufanyika.
“Ninavyojua mionzi hata kama haina madhara inabidi ichunguzwe kama ni kweli, kwa sababu hata mionzi ya X-ray katika hospitali huwa haina madhara lakini mtu asiyehusika huwa haruhusiwi kuingia na kuamriwa kukaa mbali, vipi kwa mionzi hii, tahadhari gani zimechukuliwa,” alisema Maxence Urio, mkazi wa Tabata.
Matirda Kwayu alisema huduma hizo huenda zikawa nzuri lakini gharama inayotozwa itakuwa ni kwa ajili ya watu wachache.
“Gharama kubwa halafu kama zina madhara ya muda mrefu unakuwa umetafuta magonjwa kwa gharama, ni vyema tutolewe hofu kama ni salama,” alisema Matirda.
Hata hivyo, Dk Tegete alisema licha ya kutokuwepo kwa tafiti zinazoonyesha madhara ya teknolojia hizo, ikiwamo ya uondoshaji nywele, lakini mhusika huweza kupata maumivu wakati wa huduma, uvimbe na wekundu sehemu husika.
“Hivyo kutokana na hili, tunachoweza kushauri ni mtu kutokaa karibu na mwanga wa jua baada ya procedure hii,” alisema Dk Tegete.