Sh1.1 bilioni kutatua kero ya maji Maswa

Kaimu Meneja Ufundi MAUWASA, Martin Masanja akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji katika kijiji cha Hinduki. Picha na Samwel Mwanga
Muktasari:
- Kero ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Maswa inatarajiwa kuwa historia, utakapokamilika mradi unaogharimu Sh1.1 bilioni.
Simiyu. Zaidi ya Sh1.1 bilioni zinatarajiwa kutatua changamoto ya maji kwa wananchi wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.
Fedha hizo zinazotumika kugharimia ujenzi wa mradi wa tanki la maji litakalokuwa na ujazo wa lita milioni mbili na kuwanufaisha jumla ya wananchi 102,682.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (Mauwasa), tayari ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 90.
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa mradi huo, leo Aprili 9, 2025, Kaimu Meneja Ufundi wa Mauwasa, Martin Masanja amesema kazi zilizosalia ni kufunika tanki na kufunga mifumo ya mabomba kwa ajili ya kuingiza na kusambaza maji.
“Tumebakiza kufunika tanki kwa zege na kuunganisha mfumo wa mabomba ya kuingiza na kutoa maji, kwani tayari tumeshafukia ardhini bomba kutoka hapa na tayari tumeshaliunganisha kwenye bomba kuu linalotoa maji kwenye chanzo ili kusambaza kwa wananchi,” amesema.
Ujenzi huo, amesema ni moja ya utekelezaji wa mipango ya mamlaka hiyo iliyojiwekea katika bajeti ya mwaka 2024/25 ili kuwapatia wananchi huduma bora.
“Katika bajeti yetu mwaka 2024/25 ambayo itafika ukomo Juni 30,2025 tuliweka ujenzi wa matanki mawili moja ambalo limekamilika lipo katika kilima cha Nyalikungu mjini Maswa lenye ujazo wa lita milioni moja za maji," amesema.
Amesema mradi huo utasaidia kupunguza gharama za uendeshaji kwa mamlaka hiyo kwani, walikuwa wakisukuma maji moja kwa moja kutoka katika chanzo cha Bwawa la New Sola lililoko katika kijiji cha Zanzui wilayani humo.
“Kwa sasa tutakuwa tunasukuma maji na kuyajaza kwenye haya matanki kwa muda wa saa mbili, halafu tunazima mashine na baadaye tunayaruhusu kwenda kwa wananchi,” amesema.
Mkazi wa mjini Maswa, Juma Ally ameiomba mamlaka hiyo kumaliza mradi huo kwa wakati ili mji huo na vitongoji vyake vinufaike nao.
“Huduma ya maji haina mbadala, naiomba Mauwasa ikamilishe huu mradi wa tanki la maji ili tuanze kunufaika nao,” amesema.