Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tamko la Polisi kwa anayetajwa kuwa ‘afande’

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi lasema jalada la uchunguzi limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limesema uchunguzi wa kina umefanyika na jalada limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DDP) kuhusu Fatuma Kigondo anayetajwa kuwa ni afande akidaiwa kuwatuma vijana waliombaka kwa kundi na kumlawiti binti mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam.

“Jeshi la Polisi lingependa kutoa taarifa juu ya Afisa wa Polisi anayetajwa kwa jina la Fatuma Kigondo kwamba uchunguzi wa kina ulishafanyika ikiwa ni pamoja na kupata maelezo ya watu mbalimbali pamoja na ya kwake na jalada limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka,” imeeleza taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime iliyotolewa kwa umma leo Jumamosi Agosti 24, 2024.

Taarifa ya polisi imetolewa zikiwa zimepita siku 20 tangu kusambaa kwenye mitandao ya kijamii picha jongefu (video) ikiwaonyesha vijana watano wakimbaka na kumwingilia binti kinyume cha maumbile.

Kupitia video hiyo vijana, hao walimtaka binti huyo aliyejitambulisha kuwa mkazi wa Yombo Dovya kumuomba msamaha mtu waliyemwita kwa jina la  ‘afande’ kwa kosa la kutembea na mume wake.

Video hizo zilisambaa Jumapili ya Agosti 4, 2024 na kuzua taharuki kwenye jamii, wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu wakipaza sauti wakitaka hatua kali zichukuliwe kwa wote waliohusika ikiwemo aliyetambuliwa kwa jina la ‘Afande’

Hata hivyo,  tamko la Polisi limekuja wakati ambao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kuna shauri kuhusu mtu anayetajwa kwa jina la Fatma Kigondo akidaiwa kuwa ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP). 

Mahakama hiyo imetoa wito wa kufika mahakamani (samansi) kwa Kigondo anayelalamikiwa kwa kosa la kubaka kwa kundi.

Mahakama imetoa samansi hiyo baada ya ile ya awali iliyomtaka kuhudhuria mahakamani Agosti 23, 2024 kutotekelezwa.

Shauri hilo la malalamiko limefunguliwa na Paulo Kisabo na lipo mbele ya Hakimu Mkazi Francis Kishenyi na limepangwa kutajwa Septemba 5, 2024.

Mbali ya hayo, katika mahakama hiyo kuna kesi nyingine inayowakabili askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105 Clinton Damas maarufu Nyundo, askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba wanaokabiliwa na makosa ya ubakaji wa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti, mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Salaam.

Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Zabibu Mpangule. Washtakiwa walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Jumatatu, Agosti 19, 2024.

Tayari mashahidi watatu wameshatoa ushahidi akiwamo binti anayedaiwa kubakwa na kuingiliwa kinyume cha maumbile, akiwa shahidi wa tatu wa upande wa Jamhuri.