Tamisemi yawaita wahitimu wanaotaka kubadilisha tahasusi

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa akizungumza na waandishi wa habari
Muktasari:
- Serikali imetoa mwezi mmoja kubadilisha tahasusi kwa wahitimu wa kidato cha nne mwaka 2024, huku ikiwaonya kuwa baada ya matokeo ya kujiunga na kidato cha tano na vyuo kutangazwa, ofisi haitashughulikia changamoto hizo.
Dodoma. Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ametangaza kuwa zoezi la kubadilisha tahasusi (combination) kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na vyuo litaanza rasmi Machi 31, mwaka 2025 hadi Aprili, 30, mwaka 2025.
Mbali na hilo, amesema baada ya matokeo ya kujiunga na kidato cha tano na vyuo kutangazwa, ofisi haitashughulikia changamoto hizo kwa kuwa fursa ya kufanya mabadiliko hayo imeshatolewa.
Kwa mwaka wa kwanza Serikali inakwenda kufundisha tahasusi mpya zilizoanzishwa mara baada ya kufanyika marekebisho kwa mtalaa, uliokwenda sambamba kuboresha Serikali ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014.
Sera hiyo ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023 ilizinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Februari Mosi mwaka 2025, ambayo inalenga katika kuyapa kipaumbele mafunzo ya amali nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Aprili 2, 2025, Mchengerwa amesema wahitimu wa kidato cha nne mwaka 2024 wanayo fursa ya kubadilisha machaguo ya tahasusi za kidato cha tano na vyuo vya kati na elimu ya ufundi kwenye mfumo wa kielektroniki wa uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha tano na vyuo.

Amesema utaratibu huo ni maandalizi ya awali ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga kidato cha tano na vyuo vya Serikali Mwaka, 2025.
“Itakumbukwa kuwa Serikali imekuwa ikitoa fursa kwa wahitimu wa kidato cha nne kufanya mabadiliko ya machaguo ya Tahasusi (combination) na kozi mbalimbali walizozichagua kupitia fomu ya Uchaguzi (Selform),”amesema.
Amesema fursa hiyo huwawezesha wanafunzi kurekebisha machaguo yao kulingana na ufaulu waliopata kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).
Mchengerwa amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais-Tamisemi imekamilisha zoezi la awali la kuingiza kwenye kanzidata taarifa zilizo kwenye Fomu za Uchaguzi za wanafunzi kama zilivyojazwa na wanafunzi wakiwa shuleni.
"Kukamilika kwa zoezi hili kunatoa fursa kwa wanafunzi kuweza kufanya mabadiliko ya machaguo/ tahasusi/ kozi kwa njia ya mtandao (online),”amesema.
Amesema kwa umuhimu huo, wahitimu wote wanahimizwa kufanya marekebisho ya machaguo ya tahasusi na kozi kulingana na ufaulu wao, kwa kuingia kwenye Mfumo wa Uchaguzi wa Wanafunzi (Student Selection MIS) unaopatikana kupitia kiunganishi cha selform.tamisemi.go.tz.
Mchengerwa amesema maelekezo kwa wahitimu na jinsi ya kufanya mabadiliko watayapata kwenye mfumo kupitia “user manual” pamoja na video ya youtube zilizopo kwenye mfumo huo.
Amesema ili kuingia kwenye mfumo itabidi mhitimu atumie bamba ya Mtihani wa kuhitimu Kidato cha Nne mwaka 2024, Jina lake la mwisho, mwaka wa kuzaliwa na alama ya ufaulu aliyopata kwenye somo atakaloulizwa na mfumo au swali lolote atakaloulizwa wakati wa kujaza.
"Ninawasisitiza wanafunzi, wazazi/walezi kutumia muda huo vyema ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza mara baada ya matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano na vyuo kutangazwa," amesema.
Hata hivyo, utekelezaji wa mtaala mpya wenye elimu ya amali ambao unatekelezwa kwa awamu ulianza na elimu ya awali, darasa la kwanza, kidato cha kwanza na mwaka wa kwanza wa ualimu ulianza mwaka 2024.
Julai 26, 2024, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda alisema Serikali ilisitisha utekelezaji wa mtalaa mpya kwa wanafunzi wa kidato cha tano mwaka 2024/25 ambao uliongeza tahasusi kutoka 16 hadi 65, huku 49 zikiwa ni mpya.
Profesa Mkenda alitaja sababu za kusitisha kuwa ni kutokana na changamoto za kiufundi ikiwemo kuchelewa kuchapishwa kwa nakala ngumu za vitabu.