Tamisemi kinara taarifa za rushwa Takukuru Mwanza

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Mamlaka ya Serikali za Mitaa mkoani Mwanza zimekuwa kinara ya taarifa za matukio ya rushwa zilizotolewa katika Ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) Mkoa wa Mwanza kati ya Oktoba hadi Desemba, 2022.

Mwanza. Mamlaka ya Serikali za Mitaa mkoani Mwanza zimeibuka kinara ya taarifa za rushwa zilizowasilishwa katika Ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) Mkoa wa Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza leo Jumatano Machi 22, 2023, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, James Ruge amesema Tamisema imekuwa kinara kwa kutolewa taarifa katika matukio 24 kati ya taarifa 137 zilizopokelewa kati ya Oktoba Mosi hadi Disemba 31, 2022.

“Katika kipindi hicho, Takukuru tulipokea taarifa 137, na kati ya hizo, taarifa 80 zilihusu vitendo vya rushwa huku taarifa 57 zikihusu matukio mengine. Majalada 54 ya taarifa za rushwa yako katika hatua za mwisho za uchunguzi huku mengine 26 yako katika hatua za awali,” amesema Ruge  

Wakati Tamisemi ikionekana kinara kwa taarifa za matukio ya rushwa, Asasi zisizo za Kiserikali, taasisi za dini, vyama vya ushirika, Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) na sekta ya biashara zimekuwa na taarifa kwa kutolewa taarifa za tukio moja moja ya rushwa.

Taasisi, idara na mamlaka zingine na idadi ya taarifa za matukio ya rushwa zilizoripotiwa Takukuru kwenye mabano ni sekta ya Fedha (4), Ardhi (9), Tarura (1), Ujenzi (5), Afya (7) misitu (3), Kilimo (2), Polisi (2), NGO's (1), Dini (1), Ushirika (1) Uvuvi (2), Mahakama (2), Biashara (1) na sekta ya Elimu yenye matukio 15.