Takukuru yataja taasisi nne vinara wa rushwa

Muktasari:
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imezitaja sekta zinazoongoza kwa vitendo vya rushwa nchini, huku Jeshi la Polisi likishika nafasi ya kwanza kwa asilimia 45.6 kati ya nne vinara.
Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imezitaja sekta zinazoongoza kwa vitendo vya rushwa nchini, huku Jeshi la Polisi likishika nafasi ya kwanza kwa asilimia 45.6 kati ya nne vinara.
Taasisi nyingine ni zile za afya asilimia 17.9, Mahakama ikishika nafasi ya tatu kwa asilimia 11.9 na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) nafasi ya nne, ikiwa na asilimia 6.1 ikionyesha mwingiliano wa karibu kati yake na sekta ya biashara.
Katika utafiti wa mwaka 2020 umeonyesha waathirika wanaokutana na vitendo hivyo katika sekta ya afya, wanawake walikuwa na uwezekano mkubwa wa kutoa hongo (asilimia 4.8 ikilinganishwa na asilimia 3.1 kwa wanaume) katika kutafuta huduma za afya kwa ajili yao wenyewe au za watoto.
Wakati upande wa Jeshi la Polisi wanaume walikuwa kwenye nafasi kubwa ya kuombwa hongo ikilinganishwa na wanawake, upande wa Mahakama idara ya ardhi ilikuwa inaongoza kwa kupatiwa hongo na wananchi ili wapewe huduma.
Katika utafiti huo wananchi waliohojiwa walikuwa na mtazamo tofauti katika uelewa wao wa maana ya rushwa.
Asilimia 63.6 walisema rushwa ni uhitaji wa malipo yasiyokuwa rasmi.
Asilimia 56.2 walisema kuomba rushwa kwa ajili ya kutoa huduma, huku asilimia 38.9 walidai utoaji wa huduma kwa upendeleo.
Kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2020 uliotolewa hivi karibuni, Takukuru imesema taasisi hizo zimetajwa kama zilivyotambuliwa na kuripotiwa na utafiti mwingine wa mwaka 2009 kuhusu hali ya Utawala na Rushwa Tanzania Bara.
Katika utafiti wa mwaka 2009, Jeshi la Polisi kwa jumla lilibainika kuongoza kwa vitendo vya rushwa kwa asilimia 63.5.
Kwa upande wa polisi wa usalama barabarani (Trafiki) walibainika kuwa na asilimia 66.9, mahakama kwa jumla asilimia 58.1 asilimia na ofisi ya ardhi (asilimia 41.4).
Akizungumzia utafiti wa mwaka 2020, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda alisema taasisi zilizotajwa ni zile zinazohusika na wananchi wa kawaida moja kwa moja.
“Nimegundua katika utafiti huo unazungumzia rushwa ndogondogo, kama Jeshi la Polisi huwa wanabambikia watu kesi na watu wakipigana wakipelekwa polisi ili watoke ni lazima watozwe faini ndiyo maana ni rahisi kutajwa,” alisema.
Dk Mbunda alisema kwa miaka mitano iliyopita vuguvugu la kupambana na rushwa lilianza hadi kufikia hatua ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Mafisadi, huku akieleza kwenye ripoti hiyo hata Takukuru wametajwa.
“Kama nchi hakuna mipango ya kupambana na rushwa ambayo kimsingi inapaswa kupambanwa kwa kujenga utamaduni wa watu kuchukia rushwa, katika nchi hii mtu akipatikana na hatia ya kupokea rushwa na watu wakajua wanampa sifa, ni kama wanamsifia kuliko kumchukia,” alisema Dk Mbunda.
Alisema kwa Tanzania mtu anayeishi kwa ujanja ujanja anasifiwa kuliko kuchukiwa na wananchi, huku akieleza kungekuwa na utamaduni wa kupambana na vitendo hivyo watu wanaoendelea na tabia hiyo wangekoma.
Dk Mbunda anaungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga akisema taasisi hizo ni kweli, huku akieleza hata Jeshi la Polisi kwenye ripoti zao wamekuwa wakitajwa zaidi, hasa kitengo cha usalama barabarani.
Hivyo basi wanapaswa kuzitumia tafiti hizo kujitafakari upya; na wanapaswa kuwa waadilifu kwa kuwa ni taasisi muhimu katika kutoa huduma kwa Watanzania kila siku.
“Wanapaswa kupewa mafunzo ya mara kwa mara ya uadilifu kuanzia kwenye ngazi ya chini hadi kwenye vyuo ili wajue namna ya kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya haki,” alisema.
Kauli ya Polisi
Kutokana ripoti hiyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime alisema wanauchukulia utafiti wa Takukuru kama moja ya mrejesho wa kuwasaidia kuweka mikakati endelevu zaidi na kuchukua hatua kali dhidi ya askari wenye kuendekeza tamaa binafsi.
“Kujihusisha na vitendo vya rushwa ni kwenda kinyume na sheria za nchi, kanuni za Jeshi la Polisi na miongozo ya dini.
“Tunatoa wito kwa wananchi na wadau wengine tuendelee kushirikiana katika kuzuia na kupiga vita vitendo vya rushwa, kutoa taarifa kwa wanaodai rushwa lakini pia wasiwe chanzo cha kushawishi kutoa rushwa,” alisema Misime.
Pia, alisema tatizo la rushwa linaisumbua dunia kwa muda mrefu kutokana na mtu binafsi akiwa mwajiriwa au si mwajiriwa kwa sababu lina pande mbili la mpokea na mtoaji.
Mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipa kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alisema ili kupambana na vitendo vya rushwa wanatoa barua pepe katika machapisho mbalimbali kutoa taarifa endapo mwananchi atakuwa na taarifa yoyote inayohusiana na rushwa pamoja na maadili.
“TRA tumeongeza kasi ya kuelimisha walipa kodi kutunza kumbukumbu kwa usahihi na kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati ili kuepuka kushawishika kutoa rushwa pale wanapokutwa na makosa,” alisema Kayombo.
Alisema taasisi hiyo imeweka mazingira rafiki ya kujadiliana na walipakodi kupata muafaka kwa njia ya kiungwana, hivyo kuondoa hofu na uwezekano wa kushawishika kutoa rushwa.
Pia, alisema wamewekeza katika mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili kupunguza sababu za walipakodi kuonana na watumishi kwa kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji. “Mfano Tin (Namba) inapatikana kwa njia ya mtandao, nyaraka za forodha kwa ajili ya mizigo inayoingia nchini au kutoka inawasilishwa TRA na kushughulikiwa kwa njia ya mtandao badala ya njia ya zamani ya kuja ofisini,” alisema.
Alichokisema Jaji Mkuu
Akizungumzia utafiti huo, Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Profesa Ibrahim Juma alisema Mahakama imekuwa ikitajwa kushika nafasi ya pili au ya tatu katika masuala ya utovu wa kimaadili, lakini hali ni tofauti.
Profesa Juma ambaye ni Jaji Mkuu alisema hayo Jumatatu hii, wakati tume hiyo ilipokutana na wajumbe wa kamati ya maadili ya maofisa wa mahakama ya mkoa wa Dodoma
Alisema Tanzania kuna changamoto ya tuhuma za kimazoea na hata ukimuuliza mtu ambaye hajakutana na changamoto za utovu wa kimaadili kuwa taasisi ipi inaongoza kwa utovu wa maadili kwa sababu ya kuambiwa atakutajia.
“Hata ripoti za Takukuru wao (Takukuru)wanapokea mara nyingi malalamiko ambayo hayajachambuliwa kuhusu masuala ya rushwa, lakini mara nyingi wanatuambia wameanza kuona mabadiliko makubwa ya uadilifu,” alisema Profesa Juma.
Akizungumzia utafiti huo na mikakati ya wizara kukabiliana na vitendo vya rushwa, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Afya, Edward Mbanga alisema: “Kila unapoandaa bajeti ya mwaka lazima uonyeshe ni mpango gani utafanya kwenye kudhibiti rushwa, kwa hiyo rushwa ni tabia, huwezi kusema utaimaliza ndani ya muda mfupi.”
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Stanslaus Nyongo alisema kukosekana kwa uadilifu kwa wafanyakazi wengi na sekta ya afya inaonekana kwa sababu kuna watu wengi wanatafuta huduma hiyo.
“Katika sekta ya afya hata matendo maovu yakiwamo ni rahisi kutajwa, kuna changamoto hiyo kwa wahudumu kutokujali kwenye hospitali mbalimbali kwa wale wanaohitaji huduma ya haraka au upendeleo,” alisema.