Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Takukuru yasimamisha ukarabati wa madarasa Tabora, yaonya hatari kwa wanafunzi

Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa, Takukuru mkoa wa Tabora, Azza Mtaita akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Taasisi hiyo zilizopo kata ya Cheyo Manispaa ya Tabora.

Muktasari:

  • Hatua hiyo imekuja baada ya kubainika kuwa ukuta wa madarasa hayo umekuwa chakavu kiasi cha kuhitaji kubomolewa na kujengwa upya.

Tabora. Wakati zaidi ya Sh151 milioni zikiwa zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa madarasa katika Shule ya Msingi Mtendeni, Manispaa ya Tabora, kazi hiyo imesitishwa ghafla na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) baada ya kubainika kuwa ukuta wa jengo husika umechakaa kupita kiasi na haukidhi kuendelea kufanyiwa marekebisho.

Akizungumza leo Jumanne Machi 3, 2026, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tabora, Azza Mtaita, amesema uchunguzi umeonesha kuwa ukuta wa madarasa hayo ni chakavu na unaweza kuhatarisha usalama wa wanafunzi iwapo ukiendelea kutumika.

“Tumebaini wanakarabati jengo ambalo ukuta wake haupaswi kuendelea kusimama. Ni hatari kwa watoto waliopo darasani. Tumezuia ukarabati huo na wahusika wamekubali kujenga madarasa mapya badala yake,” amesema Mtaita.

Amesema ukarabati huo uliokuwa unatarajiwa kugharimu Sh151 milioni usingekuwa na tija, ikizingatiwa hali halisi ya jengo hilo, na kwamba fedha hizo zinaweza kuelekezwa katika ujenzi mpya utakaodumu na kuwa salama kwa wanafunzi.

Mtaita ametoa kauli hiyo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025, akibainisha kuwa Takukuru imegundua mapungufu katika baadhi ya miradi ya sekta za elimu na afya mkoani humo.

Katika hatua nyingine, amesema uchunguzi umeonesha ongezeko la takribani asilimia 15 ya wanafunzi wa sekondari walioripoti shuleni Januari mwaka huu, tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita ambapo baadhi ya wanafunzi walikuwa hawajitokezi kwa wakati.

“Safari hii wanafunzi wamejitokeza kwa wingi na wako shuleni wakisoma. Hili ni jambo la kupongezwa,” amesema.

Wakazi wa Tabora wamepongeza hatua ya Takukuru

Juma Mkamia amesema ni muhimu hatua kali zichukuliwe kwa mujibu wa sheria ili kuzuia uzembe katika utekelezaji wa miradi ya umma.

Naye Mwajuma Hemedi ameitaka Serikali kuongeza kasi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu, hususan katika shule za vijijini ambazo bado zina mazingira duni.

“Miundombinu mingi sasa inavutia, lakini bado vijijini kuna changamoto. Tunahitaji maboresho yaende kila mahali,” amesema.