Taarifa ya kifo cha mume ilivyoua mke

Muktasari:
- Wazikwa siku moja, mke aliwaaga watoto akitabasamu na kuwapiga shavuni.
Njombe. Elizabeth Sawala, mkazi wa mtaa wa Mji Mwema wilayani Njombe amefariki dunia kwa shinikizo la damu baada ya kupata taarifa za kifo cha mumewe, Inyasi Hongoli.
Sawala (63) amefariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitalini mkoani Mbeya kwa matibabu zaidi baada ya kuanguka nyumbani kwake.
Lenard Hongoli, mtoto wa marehemu alieleza hayo jana, Desemba 28,2023 wakati wa ibada ya mazishi ya wazazi wake hao waliozikwa siku moja kwenye makaburi ya mtaa wa Mji Mwema wilayani Njombe.
Amesema kwa takribani miezi miwili amekuwa akiwauguza wazazi wake, lakini Desemba 25, 2023 siku ya Sikukuu ya Krismasi akiwa kanisani alipigiwa simu na jirani yake kuwa hali ya baba yake ni mbaya.
Hongoli amesema wakiwa njiani, saa mbili asubuhi wakimpeleka baba yake hospitali alifariki dunia akiwa katika miguu yake.

Waombolezaji wakishiriki mazishi ya wanandoa waliofariki na kuzikwa pamoja kwenye makaburi ya Mji Mwema mkoani Njombe. Picha na Seif Jumanne
"Tuliporudi nyumbani kwa ajili ya maombolezo, mama akapata presha ikabidi tumpeleke Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, alilazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi," amesema Hongoli.
Amesema baadaye alirudishwa kwenye wodi ya wagonjwa wa kawaida na wakaenda kumangalia.
Ameeleza alipowaona watoto wake watatu alitabasamu na kuwataka wote waende alipokuwa amelala.
Hongoli amesema walipofika aliwapiga shavuni mara tatu kila mmoja huku akitabasamu, lakini hali yake ilibadilika ghafla, hivyo kutakiwa kupelekwa Hopsitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya. Hata hivyo, amesema akiwa njiani kupelekwa Mbeya mama yake alifariki dunia.
Michael Myamba, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Yerusalemu Mji Mwema, aliyeongoza ibada ya mazishi amesema kifo cha wanandoa hao ni miujiza kwake.
Amesema yeye ndiye alifungisha ndoa yao mwaka 1987, ameshiriki ibada ya mazishi ya wawili hao waliofariki na kuzikwa siku moja.
"Mimi nasema ilikuwa mpango wa Mungu, mchungaji niliyewafungisha ndoa na ndiyo anaongoza ibada ya mazishi, kwa kweli ni jambo la kushukuru," amesema Myamba.
Mbunge wa Njombe Mjini, Deo Mwanyika ametoa wito kwa wananchi kuwa na imani na uvumilivu kutokana na tukio hilo lililowaumiza watu wengi kutokana na namna lilivyotokea.
Amesema kifo kwa mwanadamu ni funzo kubwa.
Mwanyika amesema Mkoa wa Njombe bado una matukio ya mauaji ya wenyewe kwa wenyewe, jambo ambalo halina afya.
"Nitoe pole kwa wafiwa wote, kwa watoto wa marehemu, wajukuu na ndugu mbalimbali wa pande zote. Msiba huu una utofauti, tuendelee kumtegemea Mungu," amesema.
Daktari wa tiba asili zitokanazo na mimea, Titas Mabula ameshauri wenye shinikizo la damu kufuata njia za kitaalamu ikiwamo kupata muda mzuri wa kupumzika na kunywa maji ya vuguvugu angalau glasi moja baada ya kupokea taarifa yenye kushtusha.