Sweden yajitosa kupunguza saratani Tanzania

Muktasari:
- Matumaini ya kushinda vita ya saratani yameendelea kuonekana baada ya Ubalozi wa Sweden kujitokeza katika harakati za kudhibiti ugonjwa huo kupitia kampeni maalumu.
Dar es Salaam. Matumaini ya kushinda vita ya ugonjwa wa saratani yameendelea kuonekana baada ya Ubalozi wa Sweden kujitokeza katika harakati za kudhibiti ugonjwa huo kupitia kampeni maalumu.
Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Ozaki Macias imeandaa matembezi yatafanyika Oktoba 21, mwaka huu wakati wa kampeni ya wiki ya uhamasishaji wa uelewa wa Saratani ya matiti.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 13, 2023 jijini Dar es Salaam, Balozi Macias ametaja sababu sita za kampeni hiyo ikiwamo kukuza uelewa wa umuhimu wa kupima saratani hiyo.
Pia kusaidia elimu kwa wanaume kutambua wanaweza kuathirika pia, kujifunza kuhusu teknolojia ya kisasa zaidi katika uchunguzi, kuonyesha mshikamano kwa wasaidizi na wahudumu wa afya ya saratani.
“Pia tunakusudia kusaidia wale walioathirika na saratani ya matiti na kuangazia umuhimu wa utafiti, kuzuia, matibabu na kuponakupitia matibabu,” amesema Balozi Macias akifafanua:
“Lengo ni kutoa tahadhari juu ya pengo la huduma za saratani. Tunataka kufanya sehemu yetu kwa kuwezesha wanawake kupata huduma bora ya saratani. Kwa kufanya kazi pamoja, tunaweza kuweka mkazo katika kuziba pengo la kuwafikia, kuwatunza na kuwapatia huduma,” amesema.
Matembezi hayo yanafanyika pia kwa kushirikiana na Taasisi ya Shujaa Cancer Foundation, Wizara ya Afya, Kampuni ya Elekta, Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Amesema inasikitisha takribani asilimia 80 ya wagonjwa wa saratani ya matiti kugundulika na ugonjwa huo katika hatua ya juu kutokana na upatikanaji mdogo wa programu za uchunguzi. Utambuzi wa awali na upatikanaji duni wa matibabu ikiwamo upasuaji na tiba ya mionzi.
Kampeni hiyo inafanyika wakati takwimu za Wizara ya Afya zikionyesha saratani hiyo kuwa chanzo kikuu cha vifo vinavyohusisha Saratani kwa wanawake duniani.
Aidha, zaidi ya vifo 600,000 vikiripotiwa kila mwaka, asilimia 62 vinatokeza katika nchi zinazoendelea. “Makadirio ya hivi karibuni yanaonyesha wagonjwa wapya milioni 2.1 kwa mwaka duniani,”amesema.